Sehemu ya sasa:
Somo Mambo yanayodhibiti uhusiano wa jinsia mbili hizi (wanaume na wanawake)
Sheria ya Kiislamu imelipa kipaumbele suala la kupangilia mambo ya watu katika nyanja mbalimbali, ikiwa miongoni mwa hayo ni upande wa kuamiliana kati ya wanaume na wanawake. Mwenyezi Mungu Mtukufu, ameumba katika wanaume na wanawake kuvutiana. Matokeo ya mvuto huu yanakuwa ya kusifiwa na halali kwa kuoana, na yasiyokuwa hayo, basi ni katika mlango wa uovu na majaribio makubwa sana. Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema, “Sijaacha nyuma yangu majaribio yenye kuwadhuru zaidi wanaume kuliko wanawake." (Al-Bukhari 5096, Muslim 2741)
Kitu hatari zaidi ambacho uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke unaweza kusababisha ni kuanguka katika uzinzi. Sheria iliyotakaswa haikukataza tu uchafu huu, lakini ilitahadharisha dhidi ya kuukaribia, na kufanya vitangulizi vyake, na chochote kinachoweza kuusababisha. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya." [Al-Israa: 32] Naye Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akasema, “Zina ya macho ni kutazama, na zina ya masikio ni kusikia, na zina ya ulimi ni kuzungumza, na zina ya mkono ni kushika, na zina ya mguu ni kutembea hatua, nao moyo unatamani sana, nayo tupu inayasadikisha hayo yote na unakadhibisha." (Al-Bukhari 6243, Muslim 2657, na lafudhi ya hadithi hii ni yake).
Ili kuhakikisha kuwa hakuna kupotoka au makosa ambayo yanaweza kusababisha matokeo makubwa, Sheria imeweka udhibiti kadhaa katika kuamiliana kati ya wanaume na wanawake katika kile kinachohitajika, kama vile kuuza, kununua na shughuli nyingine zinazoruhusiwa, au kile kinachohitajika mno, kama vile mwanamke kutibiwa na daktari wa kiume wakati daktari wa kike anapokosekana. Miongoni mwa vidhibiti hivi ni:
Kuinamisha chini macho
Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, "Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za wanayoyafanya. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao." [An-Nur: 30, 31]
Kujiepusha kugusa au kusalimiana mkononi
Aisha - Mwenyezi Mungu awe radhi naye - alisema, akielezea namna Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alivyokuwa akichukua ahadi ya utii kutoka kwa wanawake, "Hapana, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, mkono wa Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - haukuwahi kugusa mkono wa mwanamke." (Al-Bukhari 5288, Muslim 1866). Naye Ma'qil bin Yasar - Mwenyezi Mungu awe radhi naye - alisema, "Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alisema, "Mmoja wenu kudungwa kichwani kwake kwa sindano ya chuma ni bora kwake kuliko kumgusa mwanamke ambaye si halali kwake." (Al-Tabarani katika Al-Kabir 486, na Al-Albani alisema ni hadithi sahihi).
Kuepuka kuwa peke yao hata kidogo
Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alisema, "Kamwe mwanamume asikae peke yake na mwanamke yeyote isipokuwa pamoja na Mahramu wake." (Al-Bukhari 5233, and Muslim 1341) Pia alisema, "Kamwe mmoja wenu asibaki peke yake na mwanamke. Kwa maana, shetani ni wa tatu wao." (Musnad Ahmad 115) Kwa hivyo, wao kukaa peke yao ni mlango wa shari inayoenea sana ambayo shetani anatumia kuwatumbukiza wanaume na wanawake katika yale ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha.
Kuna mambo maalumu ya kumdhibiti mwanamke wa Kiislamu, ambayo ni lazima kwake kuyazingatia wakati anahitajika kuamiliana na wanaume.
Ni lazima kwa mwanamke wa Kiislamu kuzingatia mambo yanayodhibiti mavazi ya kisheria, kwa kufuata amri ya Mwenyezi Mungu kwanza, kisha kuwalazimisha wanaume wamheshimu na wasimdhuru; kwa vitendo, kauli au macho. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao." [An-Nur: 31] Na Mwenyezi Mungu akasema, "Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu." [Al-Ahzab: 59]
Kuepuka manukato mbele ya wanaume
Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - amesema, "Mwanamke yeyote atakayepaka manukato, kisha akapita kwa watu ili wapate katika harufu yake, basi yeye ni mzinzi." (An-Nasai 5126)
Kuzungumza kwa umakini na kutolainisha na kulegeza sauti
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu, “Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu, basi msilegeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.” [Al-Ahzab: 32]
Kutembea kwa heshima na staha
Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema juu ya binti wa Shu'ayb alipomjia Musa, amani iwe juu yake, ili amfikishie ujumbe wa baba yake, "Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya." [Al-Qas: 25] Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaambia wanawake, "Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha." [An-Nur: 31]