Sehemu ya sasa:
Somo Mauzo
Maana ya Mauzo
Kuuza katika lugha ya Kiarabu kunamaanisha kubadilishana kitu kwa kitu. Na katika istilahi ya kisheria ni kubadilishana mali kwa mali kwa njia ya kumilikisha na kumiliki.
Hukumu ya mauzo
Kuuza na kununua ni mkataba unaoruhusiwa; kwa Kitabu, Sunna na maafikiano ya wanazuoni. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, "Na Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara." [Al-Baqarah: 275]
Hekima ya kuruhusu mauzo
1- Mwanadamu anahitaji kile ambacho wengine wanakimiliki kama vile chakula, kinywaji, mavazi, makazi na mengineyo. Mmiliki wa vitu hivi hawezi kuvitoa bila malipo. Katika mauzo kuna njia ya mtu kufikia kile anachotaka; muuzaji apate thamani, naye mnunuzi apate bidhaa.
2- Kuendelea kwa maisha ya watu kwa njia bora zaidi; kwa sababu mwanadamu hawezi kukidhi mahitaji yake isipokuwa kwa kununua.
3. Kuzuia wizi, unyang'anyi, ulaghai na mambo mengine ambayo yanaharibu jamii, kwa sababu mwanadamu anaweza kupata mahitaji yake kwa kununua.