Sehemu ya sasa:
Somo Hadathi kubwa na kuoga
Sababu zinazomlazimu mtu kuoga
Ni mambo ambayo yakimtokea Muislamu, atasifika kwamba ana hadathi (uchafu) kubwa, na itamlazimu kuoga kabla ya kuswali na kufanya Tawaaf (kuzunguka kando ya Al-Kaba).
1. Kutoka manii
Kutoka manii kwa mtiririko kwa raha kwa njia yoyote ile, na katika kila hali, katika hali ya mtu kuwa macho au katika hali ya kulala. Na manii ni kioevu kinene cheupe ambacho hutoka wakati wa kilele cha matamanio ya kijinsia na raha.
2. Kufanya ngono
Kinachomaanishwa na tendo la ndoa ni kuingiza uume wa mwanaume ndani ya uke wa mwanamke, hata kama manii hayakutoka. Na inatosha kufanya kumlazimu mtu kuoga kwa kuingiza kichwa cha uume tu katika uke wa mwanamke.
3. Kutokwa damu ya hedhi na nifasi
Hedhi ni damu ya kawaida ambayo inamtoka mwanamke kila mwezi, na inaendelea kwa siku saba. Mara huzidi au kupungua kulingana na maumbile ya mwanamke. Nayo nifasi ni damu inayomtoka mwanamke kwa sababu ya kuzaa, na inaendelea kutoka kwa siku kadhaa.
Haiwalazimu wanawake wenye hedhi na wale walio katika nifasi kuswali na kufunga saumu muda wa kutokwa na damu. Watalazimika kulipa saumu baada ya kusafika, lakini hawalazimiki kulipa swala.
Kujamiiana na wanawake walio katika hedhi na nifasi
Hairuhusiki kwa wanaume kuingiliana na wake zao wakati wa hedhi au baada ya kuzaa, lakini inaruhusika kustarehe nao bila ya kujamiiana nao. Wanatakiwa kuoga pindi damu inapokatika. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watahirike. Wakishatahirika basi waendeeni alivyokuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha." (Al-Baqara: 222) Na maana ya kauli yake, "Wakishatahirika," ni wakishaoga.
Inamtosha Muislamu kukusudia kujisafisha na kuosha mwili wake wote kwa maji.
Njia kamili zaidi ya kuoga ni kuoga kama alivyooga Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Kwa hivyo, Mwislamu anapotaka kuoga kutokana na janaba, ataosha viganja vyake, kisha aoshe sehemu zake za siri na uchafu wowote uliomuendea kutokana na janaba. Kisha atatawadha wudhuu kamili, kisha ataosha kichwa chake kwa maji mara tatu, kisha ataosha mwili wake wote.
Muislamu akioga kwa sababu ya janaba, hilo linamtosha na hahitaji kutawadha. Bali lililo bora zaidi ni kutawadha kisha aoge, kama ilivyo katika Sunna ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.