Sehemu ya sasa:
Somo Maana ya Surat Al-Fatiha
Kusoma Suratul-Fatiha ni moja ya nguzo muhimu za swala, ambayo bila hiyo, swala haiwezi kuwa sahihi.
Ninamhimidi Mwenyezi Mungu kwa sifa zake zote, matendo yake na baraka zake za dhahiri na zilizofichika, kwa mapenzi na kumtukuza. Mola Mlezi ni yule ambaye ndiye Muumbaji, Mmiliki, Mlinzi na Mpaji. Nao walimwengu ni kila kitu kisichokuwa Mwenyezi Mungu kama vile ulimwengu wa wanadamu, majini, malaika, wanyama, na vitu vinginevyo.
Mwingi wa rehema na Mwingi wa kurehemu ni majina mawili miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu: Mwingi wa rehema linamaanisha Mwenye rehema za jumla ambazo zilikienea kila kitu. Na Mwingi wa kurehemu linamaanisha yule ambaye rehema zake zinawafikia waja wake waumini.
Yaani Mmiliki, mwenye kusimamisha Siku ya Malipo na Hesabu. Katika hayo kuna ukumbusho kwa Muislamu juu ya Siku ya Mwisho na kumhimiza kufanya mambo mema.
Tunakufanyia ibada Wewe peke yako, ewe Mola wetu Mlezi, wala hatukushirikishi Wewe na mwengine katika ibada ya aina yoyote. Pia tunakuomba Wewe peke yako msaada katika mambo yetu yote. Kwani mambo yote yako mkononi mwako, na hakuna hata moja asiyekuwa Wewe ambaye anamiliki hata uzito wa chembe katika hilo.
Tuonyeshe, utuongoe, na utuwezeshe kufikia njia iliyonyooka na utujaalie tuwe imara juu yake mpaka tukutane nawe. Njia iliyonyooka ni Dini ya Uislamu iliyo wazi inayofikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo, ambayo iliashiriwa na mwisho wa Manabii na Mitume, Muhammad rehema na amani zimshukie, na hakuna njia ya kumfikisha mja kwenye furaha isipokuwa kwa kunyooka kwenye njia hii.
Yaani, njia ya wale uliowaneemesha kwa wongofu na unyoofu, miongoni mwa Manabii na watu wema walioijua haki na wakaifuata. Na utuweke mbali na utuokoe kutokana na njia ya wale uliowakasirikia, kwa sababu walijua haki lakini hawakuifanyia kazi. Na pia utuepushe na njia ya wale waliopotea. Na hao ndio wale ambao hawakuongoka kwenye haki kwa sababu hawakuijua.