Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Mfungo wa Ramadhani

Kufunga saumu ya mwezi wa Ramadhani ndiyo nguzo ya nne ya Uislamu na majengo yake makubwa. Utajifunza katika somo hili kuhusu maana ya saumu na kuhusu fadhila za mwezi wa Ramadhani.

  • Kujua maana ya kufunga saumu na fadhila yake.
  • Kujua kuhusu fadhila za mwezi wa Ramadhani.

Mwenyezi Mungu aliwafaradhishia waislamu kufunga saumu mwezi mmoja katika mwaka, ambao ni mwezi wa Ramadhani wenye baraka, na akajaalia kufunga kwake kuwa nguzo ya nne miongoni mwa nguzo za Uisilamu na misingi yake mikuu. Amesema Mtukufu: "Enyi mlioamini, mmeandikiwa Saumu, kama walivyoandikiwa wale waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu." (Al-Baqara: 183)

Maana ya kufunga saumu

Maana ya kufunga Saumu katika Uislamu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kuacha na kujizuia kula, kunywa, kujamiiana, na mambo mengineyo yawezayo kumfanya mtu kufungua, kutoka alfajiri ya uhakika - ambayo ni unapoingia wakati wa swala ya alfajiri - hadi machweo, ambayo ni wakati inapoingia swala ya Magharibi.

Fadhila za Mwezi wa Ramadhani

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu, na ndio mwezi bora katika mwaka. Mwenyezi Mungu aliuteua kwa fadhila nyingi kati ya miezi mingine. Na miongoni mwake ni:

1. Kwamba ndio mwezi ambao Mwenyezi Mungu ameuteua, kwa ajili ya kuteremsha ndani yake kitabu chake kitukufu zaidi (Qur-ani Tukufu).

Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Mwezi wa Ramadhani ndio ambao imeteremshwa humo Qur-ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Na yeyote miongoni mwenu atakayeushuhudia mwezi, basi na afunge." (Al-Baqarah:185)

2. Kwamba ni mwezi ambao milango ya Pepo hufunguliwa ndani yake.

Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, “Ramadhani inapoingia, milango ya Pepo inafunguliwa, na milango ya Jahannam inafungwa, na mashetani wanafungwa minyororo.” (Al-Bukhari 3277, Muslim 1079) Kwa hivyo, huu ni mwezi ambao Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake kumrejelea kwa kufanya mambo ya utiifu na kuacha matendo maovu.

3. Kwamba mwenye kufunga mchana wake na kuamka usiku wake, atasamehewa dhambi zake zilizopita.

Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema, “Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na matumaini ya kupata thawabu, atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.” (Al-Bukhari 2104, Muslim 760). Na akasema, “Mwenye kusimama Ramadhani kwa imani na matumaini ya kupata thawabu, atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.” (Al-Bukhari 2009, Muslim 759)

4. Kwamba ndani yake kuna usiku wa cheo (Lailatul-Al-Qadr), ambao ndio usiku mkubwa zaidi wa mwaka.

Ndio usiku ambao Mwenyezi Mungu alijulisha katika kitabu chake kwamba kufanya matendo mema ndani yake ni bora zaidi kuliko kufanya matendo katika miezi elfu moja. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Usiku wa cheo ni bora zaidi kuliko miezi elfu moja." (Al-Qadr: 3) Na ni usiku ambao haujulikani hasa ni upi katika usiku kumi za mwisho wa Ramadhani. Mwenye kusimama ndani yake kwa imani na kwa matumaini ya kupata thawabu, anasamehewa dhambi zake zilizopita.

Fadhila ya kufunga saumu

Kufunga saumu kuna fadhila nyingi zilizokuja katika sheria, miongoni mwake ni:

1. Kusamehewa dhambi

Atakayefunga saumu ya Ramadhani kwa kumwamini Mwenyezi Mungu na kufuata amri zake, na kwa kusadiki yale yaliyokuja kuhusiana na fadhila zake, akitarajia malipo yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Atakayefunga Ramadhani kwa imani na matumaini ya malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia." (Al-Bukhari 2104, Muslim 760)

2. Mtu anayefunga saumu atafurahia thawabu na neema atakayopata atakapokutana na Mwenyezi Mungu.

Kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: “Mtu aliyefunga saumu ana furaha mbili; furaha wakati wa kufungua funga yake, na furaha wakati wa kukutana na Mola wake Mlezi.” (Al-Bukhari 1904, Muslim 1151)

3. Kuna mlango Peponi uitwao Ar-Rayyan, ambao watu waliofunga tu ndio wataingia humo

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema, "Hakika, kuna mlango katika Pepo uitwao Ar-Rayyan ambao watu wanaofunga wataingia humo siku ya Kiyama, na hakuna mwingine atakayeingia humo. Itasemwa: "Wako wapi watu waliofunga saumu?" Kwa hivyo watanyanyuka, na hakuna mtu mwingine atakayeingia humo asiyekuwa wao. Na watakapoingia, utafungwa, na hakuna mtu mwingine atakayeingia humo." (Al-Bukhari 1896, Muslim 1152)

4. Kwamba Mwenyezi Mungu alijinasibishia yeye Mtukufu malipo na thawabu za kufunga saumu.

Na yule ambaye thawabu zake na malipo yake yako kwa yule ambaye ndiye Mkarimu zaidi, Mwenye kutoa kwa wingi, Mwingi wa kurehemu, basi na apate bishara njema ya yale ambayo Mwenyezi Mungu amemwandalia. Amesema Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika hadithi takatifu anayoisimulia kutoka kwa Mola wake Mlezi: "Kila matendo ya mwanadamu ni yake isipokuwa kufunga saumu. Hiyo kwa hakika ni yangu, nami ndiye nitakayeilipa." (Al-Bukhari 1904, Muslim 1151)

Hekima ya kufunga saumu

Mwenyezi Mungu alifaradhisha kufunga saumu kwa sababu ya hekima mbalimbali, na faida nzuri nzuri katika dini na dunia. Na miongoni mwa hizo ni:

1. Kufikia kumcha Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu, Mtukufu

Hii ni kwa sababu kufunga saumu ni ibada ambayo kwayo mja hujikurubisha kwa Mola wake Mlezi, kwa kuacha avipendavyo, na kuzuia matamanio yake yanayoruhusiwa, kwa kufuata amri ya Mola wake Mlezi, na kuepuka makatazo yake.

2. Kujizoesha kuacha maasi na madhambi

Kwa maana, kujizuia kwa mfungaji mbali na mambo yanayoruhusiwa kwa kufuata amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kunamfanya awe na uwezo zaidi wa kuzuia matamanio yake ya maasi na madhambi.

3. Kuwakumbuka wasiojiweza na kuwafariji

Hii ni kwa sababu kufunga ni kujizoesha ugumu wa kutokuwa na kitu na ugumu wa njaa, na ni kuwakumbuka maskini ambao wanateseka kutokana na kutokuwa na kitu katika maisha yao. Kwa hivyo mja anakumbuka ndugu zake maskini na jinsi wanavyoteseka kwa njaa na kiu, kwa hivyo anajitahidi kuwapa mkono wa msaada.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani