Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Kuamini Vitabu

Kuamini Vitabu vilivyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni nguzo katika nguzo za imani. Katika somo hili, utajifunza kuhusu maana ya kuamini Vitabu, na umuhimu wake, na majina ya baadhi yake, na msimamo wetu juu ya Vitabu hivyo vilivyopo leo.

  • Kujua maana ya kuamini Vitabu na umuhimu wake.
  • Kujua msimamo wa Muislamu kuhusu Vitabu vinavyopatikana leo.
  • Kujua  wajibu wa Waislamu kuhusiana na Qur-ani Tukufu.

Maana ya kuamini Vitabu

Ni kusadiki kimadhubuti kwamba Mwenyezi Mungu aliteremsha Vitabu kwa Mitume wake ili wavifikishe kwa waja wake, na kwamba Vitabu hivi ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyoyasema kwa uhakika kama inavyomfailia Yeye, utakatifu ni wake. Na kwamba vitabu hivi ndani yake kuna haki, nuru, uwongofu na furaha kwa watu wote katika Nyumba mbili hizi.

Umuhimu wa kuamini Vtabu

Kuamini vitabu ni moja ya nguzo za imani. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Enyi mlioamini, muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha kwa Mtume wake na Kitabu alichokiteremshwa hapo kabla." (An-Nisaa: 136). Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akaamrisha kumwamini Yeye, na Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha kwa Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ambacho ni Qur-ani. Kama vile alivyoamrisha pia kuamini katika vitabu vilivyoteremshwa kabla ya Qur-ani.

Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake: “Ni kwamba umwamini Mwenyezi Mungu, na Malaika Wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na uamini katika majaaliwa ya heri na ya shari.” (Muslim 8)

Kuamini Vitabu kunajumuisha nini?

١
Kuamini kwamba kuteremka kwake kulitoka kwa Mwenyezi Mungu kihakika.
٢
Kuamini kwamba ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika, Mtukufu.
٣
Kuamini katika vitabu alivyovitaja kwa majina yake, kama vile Qur-ani Tukufu iliyoteremshwa kwa Mtume wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Taurati iliyoteremshwa kwa Musa, amani iwe juu yake, na Injili, iliyoteremshwa kwa Isa, amani iwe juu yake.
٤
Tunasadiki habari za vitabu vilivyotangulia miongoni mwa habari zile ambazo Qur-ani Tukufu au Sunna sahihi zilizithibitisha, na tunakanusha yale ambayo Qur-ani na Sunna zilikanusha, na tunanyamazia mengineyo, kwa hivyo hatuyaamini wala hatuyakanushi.

Je, msimamo wetu ni upi kuhusu vitabu vilivyotangulia?

Muislamu anaamini kuwa Taurati iliyoteremshwa kwa Musa, amani iwe juu yake, na Injili iliyoteremshwa kwa Isa, amani iwe juu yake, ni Vitabu vya kweli kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na vilijumuisha hukumu mbalimbali, mawaidha mbalimbali, habari zenye uongofu na nuru kwa watu wote katika maisha yao, uhai wao na akhera yao. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu alituambia ndani ya Qur-ani Tukufu kwamba Watu wa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wakristo, walivipotosha vitabu vyao, wakaviongezea na kuvipunguzia, kwa hivyo havikubakia kama alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu.

Hivyo basi, Taurati iliyopo sasa sio Taurati iliyoteremshwa kwa Musa, amani iwe juu yake, kwa sababu Mayahudi waliipotosha, wakaibadilisha na wakacheza na hukumu zake nyingi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na hakika miongoni mwao lipo kundi linalopindua ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema: 'Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu.' Na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uongo na wao wanajua." (Al-Imran: 78).

Vile vile, Injili iliyopo sasa sio Injili iliyoteremshwa kwa Isa, amani iwe juu yake. Kwa sababu Wakristo waliipotosha Injili na wakabadilisha hukumu zake nyingi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Wakristo: "Na miongoni mwa wale waliosema: “Hakika Sisi ni Wakristo.” Tulichukua ahadi yao, lakini wakasahau sehemu ya yale waliyokumbushwa kwayo, basi tukaweka kati yao uadui na chuki mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia yale waliyokuwa wakiyafanya.” (Al-Maida: 14).

Ndiyo maana tunapata kwamba ile inayoitwa Bibilia Takatifu iliyo mikononi mwa Wakristo leo, ambayo ina Taurati na Injili, ina itikadi nyingi potovu, na habari batili, na hadithi za uongo.

Ingawa tunaamini kuwa Taurati na Injili zilizopo leo zimepotoshwa na kubadilishwa, jinsi Qur-ani ilivyojulisha, Muislamu anaviheshimu vitabu hivi na havidunishi wala havichafui. Kwa sababu yanaweza kuwa ndani yake baadhi ya mabaki ya maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo hayajapotoshwa.

Je, ni nini wajibu wetu kwa Qur-ani Tukufu?

١
Inatulazimu tuipende Qur-ani, tukitukuze cheo chake na kuiheshimu, kwani ni maneno ya Muumba Mwenye Nguvu, Mtukufu, na ndiyo maneno ya kweli zaidi na bora kabisa.
٢
Inatulazimu tuikariri na kuisoma, tukizingatia aya zake na surah zake kwa kutafakari juu ya mawaidha yake, habari zake, na hadithi zake, na tuyaweke maisha yetu mbele yake ili tuweze kutofautisha haki kutokana na batili.
٣
Na inatulazimu tuifanyie kazi, tufuate hukumu zake, tutii amri zake, tuepuke makatazo yake, tushikamane na adabu zake, na tuifanye kuwa njia yetu ya maisha.

Alipoulizwa Aisha kuhusu tabia ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Tabia yake ilikuwa ni Qur-ani.” (Ahmad 24601)

Maana ya Hadithi hii ni kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika maisha yake, matendo yake na maneno yake yote yalikuwa ni utekelezaji wa kivitendo wa hukumu za Qur-ani na sheria zake. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa hakika alifikia ukamilifu wa kufuata uongofu wa Qur-ani, naye ndiye kiigizo kizuri mno kwa kila mmoja wetu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtakatifu: "Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.” (Al-Ahzab: 21)

Kurahisisha kuhifadhi na kusoma Qur-ani Tukufu katika sehemu mbalimbali za dunia, licha ya utofauti wa lugha na hali za wenye kuihifadhi, ni katika uthibitisho mkubwa zaidi kwamba Mwenyezi Mungu amekihifadhi kitabu hiki kitukufu.

Faida na Sifa maalumu za Qur-ani Tukufu:

Hakika Qur-ani Tukufu ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu yaliyoteremshwa kwa Nabii wetu na kiigizo chetu Muhammad, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani. Kwa hivyo, Muumini anapaswa kukiheshimu kitabu hiki na ajitahidi kushikamana na hukumu zake, kukisoma na kukitafakari. Na inatutosheleza kuwa hii Qur-ani ndiyo mwongozo wetu hapa duniani na ndiyo sababu ya kufaulu kwetu katika maisha ya akhera. Qur-ani Tukufu ina faida nyingi na sifa mbalimbali inazotofautiana kwazo na vitabu vya kimbinguni vilivyotangulia, zikiwemo:

1- Qur-ani Tukufu ilijumuisha muhtasari wa hukumu za Mwenyezi Mungu

Qur-ani Tukufu ilikuja kuunga mkono na kusadikisha yale yaliyosemwa katika vitabu vilivyotangulia kuhusu amri ya kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tumekuteremshia Kitabu kwa Haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Kitabu, na kinachoyadhibiti." (Al-Maida: 48). Na Maana ya: "kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Kitabu" ni inakubaliana na yale yaliyokuja katika habari za vitabu vilivyotangulia, na yaliyokuja humo miongoni mwa itikadi mbalimbali. Na maana ya "na kinachoyadhibiti." Yaani, ni cha uaminifu na ni shahidi juu ya vitabu vilivyokuja kabla yake.

2- Kwamba watu wote, bila kujali lugha zao na makabila yao, lazima wakiamini.

Na kutenda matendo kwa mujibu wake, haijalishi muda wao umechelewa kiasi gani tangu wakati wa kuteremshwa kwa Qur-ani, tofauti na vitabu vilivyotangulia, ambavyo ni kwa ajili ya watu mahsusi katika wakati maalumu.” Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na nimefunuliwa Qur-ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayomfikia." (Al-An'am: 19)

3- Mwenyezi Mungu Mtukufu alichukua dhamana ya kuihifadhi Qura-ni Tukufu.

Na Mkono wa upotovu haukukifikia, wala hautakifikia abadan. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Sisi ndio tuliouteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakaoulinda." (Al-Hijr: 9) Na kwa sababu ya hilo, habari zake zote ni sahihi na ni lazima zisadikiwe.

Kuamini vitabu kuna matunda mengi, ikiwa ni pamoja na:

١
Kujua kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anawajali waja wake na kujua ukamilifu wa rehema yake, kwani aliwatumia kila kaumu kitabu cha kuwaongoza na kuwaletea furaha duniani na akhera.
٢
Kujua hekima ya Mwenyezi Mungu mtukufu katika Sheria yake, ambapo aliuwekea kila kaumu sheria inayofaana na hali zao na inayolingana na nafsi zao. Kama Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyosema: "Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sheria yake na njia yake." (Al-Maida: 48)
٣
Kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya kuteremsha vitabu hivi, kwani vitabu hivi ni nuru na uongofu katika dunia na akhera, kwa hivyo ni lazima kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hizi kubwa.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani