Sehemu ya sasa:
Somo Haki za wazazi
Uislamu uliwaheshimu wazazi kwa heshima kubwa, na ukaunganisha kuwafanyia wema na amri kubwa zaidi katika Uislamu, ambayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema." [Al-Israa: 23] Mwenyezi Mungu Mtukufu amewafanya wazazi kuwa sababu ya kuwepo kwa wana wa kiume na mabinti, na hata wana wakifanya watakachofanya ili kurudisha chochote katika wema wao juu yao, kamwe hawataweza kurudisha chochote katika wema huo wa wazazi wao juu yao, wala kuwalipa kwa taabu, uchovu, madhara, kukesha, na ukosefu wa raha waliopata kwa ajili ya furaha ya watoto wao, ili kuwatunza na kuwalinda.
Katika uadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwamba aliwapa wazazi haki juu ya wana wao, ziwe malipo kwao kwa sababu ya juhudi nzuri ambazo walifanya kwa wingi katika kuwatunza. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Na tumemuusia mwanadamu awatendee wema wazazi wake wawili." [Ankabut: 8] Na akasema, "Lakini kaa nao kwa wema duniani." [Luqman: 15] Na wakati mmoja wa maswahaba alipomuuliza Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, - 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni nani anayestahiki zaidi nikae vyema naye?' Akasema, "Mama yako." Akasema, 'Kisha nani?' Akasema, "Kisha mama yako." Akasema, 'Kisha nani?' Akasema, "Kisha mama yako." Akasema, 'Kisha nani?' Akasema, “Kisha baba yako.” (Al-Bukhari 5971, Muslim 2548)
Fadhila ya kuwafanyia wema wazazi
Kuwafanyia wema wazazi ni wajibu kwa watoto, na katika kuwafanyia wema kuna malipo makubwa, na ni sababu ya kubarikiwa na kuruzukiwa, na kupata heri nyingi katika dunia hii, na ni sababu ya kuingia Peponi huko Akhera. Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alisema, "Limeangamia pua lake, kisha limeangamia pua lake, kisha limeangamia pua lake." Ikasemwa: Ni nani huyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema, "Ni yule aliyewapata wazazi wake katika uzee, mmoja wao, au wote wawili, kisha asiingie Peponi." (Muslim 2551)
Kuwafanyia wema wazazi ni mojawapo ya matendo bora zaidi na ambalo ni pendwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Abdullah bin Masud, Mwenyezi Mungu amridhie, alimuuliza Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - 'Ni kazi gani inayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu?' Akasema, "Swala kwa wakati wake." Akasema, 'Halafu nini?' Akasema, "Halafu kuwafanyia wema wazazi." Akasema, 'Halafu nini? 'Akasema, “Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.” (Al-Bukhari 527, Muslim 85)
Kwa hivyo, kuwafanyia wema wazazi ni bora kuliko jihadi ya sunna. Mwanamume mmoja alimjia Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - na akasema, 'Niende katika Jihadi?' Akasema, "Una wazazi?" Akasema, 'Ndiyo.' Akasema, "Basi fanya jihadi katika hao." (Al-Bukhari 5972, Muslim 2549)
Kuwatotii wazazi
Kutotii wazazi ni moja ya dhambi kubwa zaidi. Katika hadithi, Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alisema, "Madhambi makubwa zaidi ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na kuwaasi wazazi..." hadi mwisho wa hadithi. (Al-Bukhari 6919, Muslim 87)