Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Mtume mume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie

Katika somo hili, tutajifunza kuhusu upande wa maisha ya Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - nyumbani kwake na jinsi alivyoamiliana na wake zake.

  • Tutajua hali ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, nyumbani kwake.
  • Tutajua maadili mema ambayo Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alikuwa akiamiliana kwayo watu wa nyumba yake.
  • Kumfuata Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, katika kuamiliana na wake zake.

Ni hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba aliwafanya Mitume wake kuwa wanadamu, ili wawe hoja dhidi ya watu katika kufuata mfano wao, na kuwa na maadili yao, na kufanya sawa na matendo yao. Furaha ya Muislamu katika dunia yake na akhera yake iko katika kufuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, na kufuata nyayo zake. Kwa hivyo, Muislamu anapaswa kuhakikisha kwamba anayajua maisha ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, na Sunna zake, ili ajitahidi kuzifuata katika hali zake zote.

Maisha ya Mtume nyumbani kwake na pamoja na wake zake ndiyo kielelezo cha hali ya juu kabisa kwa binadamu wote. Yeye ndiye kielelezo ambaye anapaswa kuigwa na kila mume anayetaka familia yake kuwa na maisha mema duniani, na kufaulu kuingia Peponi Akhera. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana." [Al-Ahzab: 21]

Miongoni mwa maadili makuu ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, akiwa pamoja na wake zake:

Imesimuliwa kutoka kwa Aisha - Mwenyezi Mungu awe radhi naye - kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema, "Mbora wenu ni mbora wenu kwa familia yake. Nami ndiye mbora wenu kwa familia yangu." (Tirmidhi 3895) Basi Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, anawaamrisha wanaume katika umma wake kuwatendea wema wanawake wao, na anamsifu mwenye kufanya hivyo, kisha anabainisha kuwa yeye ndiye kiigizo chao katika hilo.

Kujali kwa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, wanawake wake na kutimiza matamanio yao ya halali

Imesimuliwa kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema, "Nilimwona Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - akinisitiri kwa vazi lake, ilhali ninawatazama Wahabeshi wakicheza msikitini, mpaka niwe mimi mwenyewe nimechoka kuangalia. Basi thaminini thamani ya msichana mdogo ambaye ana hamu kubwa juu ya pumbao." (Al-Bukhari 5236, and Muslim 892) Na katika kumuiga Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, ni kwamba mume anapaswa kuwa na utambuzi, na ajali matamanio ya mke wake, na athamini mahitaji yake halali ya kisaikolojia na ayatimizie.

Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, aliona kuwa mwanamume kucheza na familia yake ni katika pumbao iliyoidhinishwa, na akakanusha kuwa hilo si katika pumbao mbaya. Alisema, "Kila kitu ambacho mwanadamu anafanyia pumbao ni batili, isipokuwa pumbao tatu: Kutupa kwake upinde, kumfunza adabu farasi wake, na kucheza kwake na familia yake. Kwani hayo yote ni katika haki."(Musnad Ahmad 17337)

Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, alithibitisha kuwa alikuwa pamoja na Nabii, - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - katika safari moja. Akasema: Mimi nikashindana naye na nikamtangulia juu ya ngamia wangu. Lakini nilipozidi kunenepa, nikashindana naye, naye akanitangulia. Kwa hivyo akasema, "Kukutangulia huku kunalipa kule ulikonitangulia."(Abu Dawud 2578) Kwa hivyo Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alikuwa akicheza na wake zake na akifanya mzaha nao. Kwa hivyo maisha ya ndoa hayaendelei kuwa ya namna moja tu na ya kuchosha.

Hekima ya Nabii, - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, katika kuamiliana na matatizo ya kifamilia

Hakuna nyumba miongoni mwa nyumba ambayo haina shida kati ya watu wake. Nabii, - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alitupigia mifano mizuri zaidi ya jinsi ya kukabiliana na matatizo haya. Anas, Mwenyezi Mungu amridhie, alisimulia kuwa: Nabii, - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alikuwa kwa baadhi ya wake zake, kisha mmoja wa mama za waumini akatuma huko chombo chenye chakula ndani yake. Kwa hivyo yule ambaye Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alikuwa katika nyumba yake akaupiga mkono wa mtumishi, na chombo hicho kikaanguka chini na kikapasuka. Basi Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - akavikusanya vipande vya chombo hicho, kisha akakusanyia humo chakula hicho kilichokuwa ndani yake huku akisema, "Mama yenu ameona ghera." Kisha akamzuilia mtumishi huyo mpaka alipokuja na chombo kingine kutoka nyumbani mwa yule ambaye Nabii alikuwa katika nyumba yake, kwa hivyo akapelekewa chombo hicho kilicho sahihi yule ambaye chombo chake kilivunjwa, na akakiacha hicho kilichovunjwa katika nyumba ya yule aliyekivunja. (Al-Bukhari 5225)

Kwa hivyo, Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, hakuwa akifungia kifuani mwake matendo yanayofanyika kwa sababu ya hisia za maumbile ya asili za wake zake au za watu wa nyumba yake. Alikuwa akiamiliana na kila hali kwa ustadi na hekima. Ikiwa hali ilikuwa inaashiria kwamba kuna ugomvi na mzozo, yeye alikuwa akibadilisha mambo kwa hekima yake, kutochemka kwake na kutokasirika kwake, na anapunguza wasiwasi, na anafanyia uadilifu pande zote.

Alikuwa akikubali mke wake amkasirikie, naye anakabiliana na hilo kwa kufanya wema na rehema. Imesimuliwa kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie kuwa alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - aliniambia, "Hakika mimi ninajua unapokuwa umeniridhia, na unapokuwa umenikasirikia." Akasema: Nikasema: Unajuaje? Akasema, "Ama unapokuwa umeniridhia, basi wewe husema: Hapana, ninaapa kwa Mola Mlezi wa Muhammad. Na unapokuwa umenikasirikia, wewe husema: Hapana, ninaapa kwa Mola Mlezi wa Ibrahim." Alisema: Nikasema: Ndiyo, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hapo mimi huwa sijaacha isipokuwa jina lako tu. (Al-Bukhari 5228, Muslim 2439)

Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kuishi kwa wema na wanawake zake

Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alikuwa akiwasaidia wake zake katika mambo ya nyumbani na kazi zake; kama rehema na kuwaepesishia. Na ilikuwa katika maadili yake ni kujitumikia yeye mwenyewe katika mambo yake ya kibinafsi.

Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, aliulizwa: Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alikuwa akifanya nini nyumbani mwake? Alisema: Alikuwa katika kuwahudumia watu wa familia yake, na swala ilipohudhuria, alikuwa akitoka kwenda kuswali. (Al-Bukhari 676) Na akasema katika hadithi nyingine: Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alikuwa akirekebisha ndara zake, na akishona nguo yake, na anafanya kazi katika nyumba yake kama mmoja wenu anavyofanya kazi katika nyumba yake." (Musnad Ahmad 25341)

Miongoni mwa jinsi kuwaonyesha wanawake upendo:

١
Kuwaita kwa maneno ya upendo
٢
Kuwalisha chakula
٣
Kuwaambia moja kwa moja kwamba unawapenda
٤
Kuwasikiliza wanapozungumza na kujali wanachokisema

Kuwaita wake kwa maneno ya upendo

Imesimuliwa katika hadithi kwamba Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alimwambia Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, “Ewe Aish, huyu hapa Jibril anakusalimia.” (Al-Bukhari 3768). Pia alimwita "keupe kangu."

Mume kumlisha mkewe

Imesimuliwa na Sa'd bin Abi Waqqas, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alimwambia, “Chochote utakachokitoa katika matumizi, hicho hakika ni sadaka, hata tonge unaloliinua hadi mdomoni mwa mkeo." (Al-Bukhari 2742)

Kumuambia waziwazi mkewe kwamba anampenda

Imesimuliwa kutoka kwa Amr bin al-Aas, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alimtuma kama kiongozi wa jeshi la wapiganaji wenye minyororo, akasema: Kisha nikamjia na nikasema: Ni mtu gani mpendwa zaidi kwako? Akasema, "Aisha." (Al-Bukhari 3662, Muslim 2384)

Kuwasikiliza wanapozungumza na kujali wanachokisema

Katika yale yanyoonyesha hilo ni hadithi ndefu ya Ummu Zarr, ambamo Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, alihadithia habari za wanawake kumi na mmoja, ambapo walikaa, na kila mmoja wao akaanza kuzungumza juu ya hali yake na mumewe. Kwa hivyo Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - akasalia akimsikiliza Aisha mpaka akamaliza yaliyotokea kati yao wote kabisa.

Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kujipamba na kujirembesha kwa ajili ya wake zake

Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, aliulizwa: 'Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alikuwa akianza na nini alipokuwa akiingia nyumbani kwake?' Akasema: 'Mswaki.' (Muslim 253) Na imethibiti kutoka kwake, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema: Nilikuwa nikimpaka Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, manukato kwa manukato mazuri zaidi ambayo ningeweza kupata, hadi nikawa ninaona mng'ao wa manukato katika kichwa chake na ndevu zake." (Al-Bukhari 5923)

Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kuwatimizia wake zake

Katika mambo yanayodhihirisha zaidi kutimiza huku, ni ile hali aliyokuwa nayo Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - kuhusiana na Khadija, Mwenyezi Mungu amridhie, miaka mingi baada ya kifo chake. Nayo ni kwamba Zainab, binti wa Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alipotaka kumkomboa Abu al-Aas - na alikuwa amemuoa kabla ya Uislamu na akakamatwa kama mateka huko Badr - kwa mkufu wa Khadija, Mwenyezi Mungu amridhie, Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - aliona huruma mno kwa kuona mkufu huo na akasema, “Mkiona kwamba mnaweza kumuachilia mateka wake, na mumrudishie kilicho chake, basi fanyeni." (Abu Dawud 2692) Na kumtimizia kwake kulifikia kile kilichomfanya Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, amwonee wivu, ilhali hata hakuwahi kumuona wala kuishi katika zama zake. Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, alisema: Hakuna yeyote miongoni mwa wanawake wa Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - niliyemwonea wivu zaidi ya Khadija, ingawa sikuwahi kumuona, lakini Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alikuwa akimtaja mara kwa mara. Na labda angeweza kumchinja kondoo kisha akamkatakata vipande, kisha akawatumia rafiki za Khadija, na huenda angemwambia: kana kwamba hakukuwa mwanamke yeyote katika dunia hii isipokuwa Khadija, naye anasema, "Hakika yeye alikuwa, na alikuwa, na nikapata mtoto kutoka kwake." (Al-Bukhari 3818, 2435)

Mambo yanayoonyesha uadilifu wa Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - kati ya wake zake

١
Uadilifu katika makazi na kukaa. Alikuwa akigawanya usiku baina yao kwa usawa, na anawazunguka wote bila ubaguzi. Lakini ikiwa jambo jingine lingetokea, linalohitaji isiwe hivyo, alikuwa akiwaomba ruhusa. Imesimuliwa kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema: Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alipokuwa na uzito mkubwa na maumivu yake yakaongezeka, aliomba wake zake ruhusa kwamba auguziwe nyumbani kwangu, kwa hivyo wakamruhusu. (Bukhari 198, Muslim 418)
٢
Uadilifu kati yao katika safari, ambapo alikuwa akiamua kati ya wanawake wake kwa kura, kwa hivyo yule ambaye mshale wake ulitoka yeye ndiye angesafiri pamoja naye.
٣
Alikuwa anapomuoa mwanamwali, anakaa kwake usiku tatu ili wazoeane, kisha angemgawia kama wake zake wengine wote.
٤
Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alikuwa akifanya uadilifu kati ya wake zake katika kugawanya kwake katika kila kitu alichoweza kuhusiana na matumizi ya nyumbani na mali.

Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - kuwathamini wake zake na kutafuta ushauri wao

Hakuna kilicho wazi zaidi kuhusu hilo kuliko Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, - alipotafuta ushauri wa mkewe, Ummu Salama, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, siku ya Hudaybiya, alipowataka Waislamu wachinje na kunyoa nywele, lakini hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyenyanyuka. Basi akaingia alimokuwa Ummu Salama, na akamtajia yale aliyokumbana nayo kutoka kwa watu, naye Ummu Salama akasema: Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu, je, unayapenda hayo? Toka nje na kisha usizungumze neno na yeyote miongoni mwao, mpaka utakapochinja ngamia wako, na umwite mwenye kukunyoa akunyoe." Basi akatoka nje na hakuzungumza na yeyote miongoni mwao mpaka akafanya hivyo; alimchinja ngamia wake, na akamwita mwenye kumnyoa naye akamnyoa. Kwa hivyo, walipoona hivyo, wakanyanyuka na kuchinja ngamia wao, na wakawa wananyowana wenyewe kwa wenyewe. (Al-Bukhari 2731)

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani