Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Swala ya Ijumaa

Swala ya Ijumaa ni mojawapo ya swala muhimu zaidi za faradhi juu ya Waislamu na iliyosisitizwa zaidi. Katika somo hili, utajifunza kuhusu fadhila za swala ya Ijumaa na hukumu zake.

  • Kujua fadhila za swala ya Ijumaa.
  • Kujua namna na hukumu za swala ya Ijumaa.
  • Kujua wale ambao wamepewa udhuru wa kutohudhuria swala ya Ijumaa.

Swala ya Ijumaa

Siku ya Ijumaa, wakati wa sala ya adhuhuri, Mwenyezi Mungu aliwajibisha swala ambayo ni moja ya ibada kubwa zaidi za Uislamu na iliyosisitizwa zaidi kati ya mambo yake ya wajibu, ambayo Waislamu hukutana mara moja kwa wiki, husikiliza mawaidha na maelekezo ambayo wanaambiwa na Imamu wa Ijumaa, kisha wanaswali swala ya Ijumaa.

Fadhila ya siku ya Ijumaa

Siku ya Ijumaa ndiyo siku kuu zaidi kati ya siku za wiki na tukufu zaidi kati yake. Mwenyezi Mungu aliichagua juu ya siku nyinginezo, na akaipendelea zaidi kuliko nyakati nyinginezo kwa sifa maalumu kadhaa, kama vile:

1- Mwenyezi Mungu aliuteua umma wa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa ajili ya siku hii, na hakuuteulia umma mwingineo. Kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, "Mwenyezi Mungu aliwapoteza wasipate siku ya Ijumaa wale waliokuwa kabla yetu, kwa hivyo Wayahudi wakapata Jumamosi, na Wakristo wakapata Jumapili, kisha Mwenyezi Mungu akatuleta, na Mwenyezi Mungu akatuongoa tukaipata siku ya Ijumaa." (Muslim 856).

2- Kwamba Adam, amani imshukie, aliumbwa siku ya Ijumaa, na ambayo ndani yake Saa itasimama. Kama alivyosema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, "Siku bora zaidi ambayo jua linachomoza ndani yake ni Ijumaa; ndani yake Adam aliumbwa, na ndani yake aliingizwa Peponi, na ndani yake alitolewa humo, na Saa haitasimama isipokuwa siku ya Ijumaa." (Muslim 854)

Swala ya Ijumaa inampasa nani?

١
Mwanamume, na siyo wajibu kwa mwanamke.
٢
Mtu anayejukumika kisheria, na siyo mwendawazimu, wala mtoto mdogo ambaye hajabalehe.
٣
Mkazi, na siyo msafiri wala mtu anayeishi jangwani mbali na miji.

Namna ya kuswali Swala ya Ijumaa

Kujiandaa kwa ajili ya Swala ya Ijumaa

Inapendekezwa kwa Muislamu kuoga kabla ya swala ya Ijumaa, na kwenda mapema msikitini kabla ya kuanza kwa khutba, na kupaka manukato, na kuvaa mavazi mazuri.

Khutba ya Ijumaa

Waislamu hukutana msikitini, na imamu anakwenda mbele yao, kisha anapanda juu ya mimbari na kuwaelekea wanaoswali, kisha anawatolea khutba mbili, huku akitenganisha kati yake kwa kikao kifupi. Anawakumbusha kumcha Mwenyezi Mungu, anawanasihi na kuwapa mawaidha na kuwasomea aya mbalimbali.

Inawalazimu wanaoswali kusikiliza khutba, na ni haramu kwao kuzungumza au kujishughulisha wakakosa kufaidika nayo, hata kama ni kwa kuchezacheza na mazulia au changarawe na mchanga.

Kisha imamu anateremka chini kutoka kwenye mimbari na anawaswalisha watu rakaa mbili, ambamo anasoma kwa sauti kubwa.

Mwenye kupitwa na swala ya Ijumaa

Swala ya Ijumaa inalazimu tu watu wanapokutana misikitini. Kwa hivyo anayekosa au kupitwa nayo kwa sababu ya udhuru fulani, basi anapaswa kuswali Adhuhuri badala yake, na akiswali Ijumaa haikubaliki kutoka kwake.

Mwenye kuchelewa akapitwa na swala ya Ijumaa

Yeyote atakayechelewa kuswali swala ya Ijumaa na hakukuta isipokuwa chini ya rakaa moja, basi ataendelea kuswali swala hiyo kwa nia ya adhuhuri.

Kila asiyewajibika kuswali Ijumaa kama vile mwanamke na msafiri, ikiwa ataiswali pamoja na jamaa ya Waislamu, basi itakuwa sahihi, na haitamlazimu kuswali swala ya Dhuhr.

Ulazima wa kuhudhuria Ijumaa

Sheria ilisisitiza ulazima wa kuhudhuria swala ya Ijumaa kwa wale ambao ni wajibu kwao, na ikatahadharisha dhidi ya kujishughulisha na kuiacha kwa ajili ya kufuata dunia. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Enyi mlioamini! Ikiadhiniwa Swala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye utajo wa Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua." (Al-Jumaa 9)

Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alitishia kwa kitu gani mwenye kukosa kuiswali Swala ya Ijumaa?

Alimtishia mwenye kubaki nyuma akakosa kuiswali bila ya udhuru wa kisheria kwamba moyo wake utazibwa. Alisema, "Mwenye kuacha Ijumaa tatu kwa kuzembea tu bila ya udhuru, Mwenyezi Mungu ataziba kwenye moyo wake." (Abu Dawud 1052, Ahmad 15498) Na maana yake ni kwamba atauziba na kuufunga, na atie humo ujinga, ugumu kama vile nyoyo za wanafiki na waasi.

Je, udhuru upi unaoruhusiwa ili kukosa kuswali Ijumaa?

Udhuru unaoruhusu kuacha kuswali Ijumaa kwa yule ambaye inamlazimu ni kila chenye kusababisha shida kubwa isiyo ya kawaida, au kinahofiwa kusababisha madhara makubwa juu ya maisha ya Mwislamu au afya yake.

Je, kazi ya kuendelea ni udhuru wa kuacha kuswali swala ya Ijumaa?

Kazi ya kudumu na ya kurudiarudia haizingatiwi kama ni kisingizio cha kuacha kuswali swala ya Ijumaa kwa yule ambaye inamlazimu, isipokuwa katika hali mbili:

1. Kwamba kazi hiyo iwe ina masilahi makubwa ambayo hayawezi kupatikana isipokuwa kukaa kazini na kuiacha swala ya Ijumaa, na kwamba kama ataacha kazi yake, utatokea uharibifu mkubwa, na wala hakuna mtu mwingine wa kumwakilisha katika kazi hii.

Mifano

١
Daktari katika ambulensi ambaye hutibu hali na majeraha ya dharura.
٢
Mlinzi na polisi ambao huhifadhi mali za watu na nyumba zao kutokana na wizi na vitendo vya uhalifu.
٣
Mtu anayesimamia na kufuatilia kazi za viwanda vikubwa na mfano wake, ambazo zinahitaji kufuatiliwa kila dakika wala haziwezi kusimamishwa.

2. Kwamba kazi hiyo iwe ndiyo chanzo pekee cha riziki yake na hana kile kinachotosha matumizi yake muhimu kama vile chakula, vinywaji na vitu vingine muhimu kwake na familia yake. Kwa hivyo ni lazima kwake kukaa kazini na kuacha swala ya Ijumaa kwa maana inamlazimu hadi atakapopata kazi nyingine, au kupata kile kinachomtosheleza miongoni mwa chakula, vinywaji na vitu muhimu kwake na wategemezi wake. Walakini, lazima atafute kazi kila wakati na chanzo kingine cha riziki.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani