Sehemu ya sasa:
Somo Kupambana na itikadi potofu za mioyo ya watu
Kabla ya Uislamu, Waarabu na mataifa kwa ujumla walikuwa mateka wa hekaya za kubuni, na itikadi za uongo, na fikira potofu zilizoenea katika pande zote za dunia, na halikusalimika kutokana nazo taifa miongoni mwa mataifa, mpaka Waarabu wakadai - hapo mwanzo - kwamba Qur-ani Tukufu ilikuwa ni aina ya ngano au uchawi.
Uislamu ulipokuja na nuru yake na uwongofu wake, uliikomboa akili kutoka katika utawala wa itikadi za uongo, na hekaya za kubuni, na fikira potofu, kwa sheria mbalimbali, na misingi ambayo inahakikisha usafi wa akili na roho, na inafanya mtu kujifungamanisha na Mwenyezi Mungu pekee na si asiyekuwa Yeye, na katika hayo ni:
Kupambana na uganga na uchawi:
Uislamu uliharamisha uganga, uchawi, na ukuhani kwa aina zake zote, na ukayafanya kuwa ni katika aina za ushirikina na upotofu, na ukajulisha kuwa mganga (mchawi) hawezi kufaulu katika dunia wala katika Akhera. Yeye Mtukufu alisema, "Na wala mchawi hafaulu vyovyote akujavyo." (Taha: 69)
Vile vile umeharamishia Muislamu kwenda kwa waganga, na makuhani na kuwauliza, na kuomba ponya, au tiba, na kuwatatulia matatizo kutoka kwao. Na amemweleza mwenye kufanya hivyo kuwa ni kafiri katika yale yaliyoteremshwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Kwa sababu, manufaa na madhara yamo mkononi mwa Mwenyezi Mungu. Na haijui ghaibu isipokuwa Yeye pekee. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: - "Mwenye kumjia mpiga ramli, au kuhani na akamsadiki katika yale anayoyasema, basi kwa hakika amekufuru katika yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake." (Mustadrak Al-Hakim: 15).
Kunufaisha na kudhuru viko mkononi mwa Mwenyezi Mungu Mtakatifu
Mwenyezi Mungu Mtukufu alibainisha kuwa viumbe vyote, wakiwemo wanadamu, na majini, na miti, na mawe na sayari, hata vikiwa vikubwa vipi, si chochote isipokuwa ni ushahidi juu ya ukubwa wa uumbaji wake, Yeye Mtakatifu, na kwamba hakuna hata mmoja katika wanadamu anayemiliki nguvu zisizo za kawaida zinazoathiri katika ulimwengu. Basi, uumbaji, na amri, na uwezo, na uendeshaji mambo ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Mtakatifu, Mtukufu. Kama alivyosema Yeye Mtukufu, "Fahamuni! Ni kwake kuumba, na amri. Mwenyezi Mungu ni Mwenye baraka nyingi, Mola Mlezi wa viumbe vyote." (Al-A'raf: 54).
Na mwenye kutafakari katika ukubwa wa viumbe hivyo na usahihi mkubwa wa kuumbwa kwao, atajua kwamba Muumba wao ndiye Mola Mlezi, Muweza wa yote, Mwendesha mambo, ambaye ni lazima kumfanyia kila aina za ibada Yeye pasi na asiyekuwa Yeye. Kwani, Yeye ndiye Muumba, na asiyekuwa Yeye ameumbwa. Yeye Mtukufu amesema, "Na katika ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi. Bali msujudieni Mwenyezi Mungu ambaye aliviumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.” (Fussilat: 37).
Hakuna anayejua ghaibu na yajayo isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu alijulisha kwamba ghaibu na yajayo hakuna ayajuaye isipokuwa Yeye, Mtakatifu. Na mwenye kudai kwamba anajua ghaibu miongoni mwa makuhani, na wachawi, basi yeye ni mwongo. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu, “Na ziko kwake funguo za ghaibu, hakuna azijuaye isipokuwa Yeye tu.” (Al-An’am: 59)
Bali, mbora zaidi na mtukufu zaidi wa viumbe, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimfikie, hakuwa anaimilikia nafsi yake madhara wala manufaa, wala hakuijua ghaibu wala yajayo. Basi vipi yule ambaye yuko chini yake katika heshima na hadhi. Kama Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyosema: "Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ningejizidishia mema mengi, wala ovu lisingenigusa. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mbashiri kwa watu wanaoamini.” (Al-A’raf: 188).
Kuharamishwa kwa kuathirika na vitu, na kuona mkosi
Uislamu uliharamisha kuathirika na vitu (Twiyara), na kuona mkosi katika vitu, na rangi, na maneno, na mfano wa hayo, na ukaweka sheria za kuwa na matumaini na mtazamo mzuri juu ya siku zijazo.
Mfano wa kuathirika na vitu ni mtu mwenye kuathirika katika safari yake au safari yake ikiwa ataona aina fulani ya ndege au kusikia sauti yake mwanzoni mwa safari yake, na labda akaikata na asiikamilishe. Na Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alieleza hilo kuwa ni ushirikina na akasema: “Tiyara (kuathirika na vitu) ni shirki” (Abu Dawud 3910, Ibn Majah 3538). Kwa sababu hilo linapingana na imani thabiti ya Muislamu kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwendesha mambo ya ulimwengu, mwenye kujua ghaibu peke yake na hakuna mwingine. Kwa hivyo Uislamu ukakataza kuathirika na vitu na kutarajia maovu kwa sababu ya kuona tu au kusikia aina ya ndege fulani au wanyama.
Na kwa upande mwingine, aliweka sheria ya kuwa na matumaini, na kuchagua maneno yanayoonyesha jambo hilo, na kutazamia heri na kuwa na dhana nzuri kwa Mwenyezi Mungu. Na Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - alikuwa akisema, ”Ninapendezwa na al-fa-al, yaani neno zuri, neno jema.” (Al-Bukhari: 5776, Muslim: 2224)