Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Waqf

Katika somo hili, tutajifunza kuhusu maana ya waqf na hukumu zinazofungamana nayo katika sheria ya Kiislamu.

  • Kujua maana ya waqf na hekima ya kuiweka katika sheria.
  • Kujua hukumu zinazofungamana na waqf.

Baadhi ya wale ambao Mwenyezi Mungu amewapa wasaa miongoni mwa matajiri wanapenda kwamba waweke baadhi ya mali zao fulani, - ambazo zenyewe na manufaa yake yataendelea kuwepo - ziwe Waqf ambazo manufaa yake yatapeanwa katika njia za heri; ili wapate mazuri kwa sababu ya hilo katika maisha yao na baada ya kifo, na ili kwa sababu ya waqf hiyo watu wahitaji waweze kupata manufaa mengi.

Maana ya waqf

Ni kuzuilia mali yenyewe, na kuyafanya manufaa yake kuwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, ili kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye, Nguvu Mtukufu.

Hukumu ya Waqf

Kufanya Waqf ni jambo linalopendekezwa, nalo ni katika sadaka bora zaidi, na matendo makubwa zaidi ya kujiweka kwayo karibu na Mwenyezi Mungu. Waqf ni wema na hisani, na ni yenye manufaa mengi zaidi na ya kujumuisha zaidi, kwa sababu ni katika matendo yanayonufaisha hata baada ya kifo.

Hekima ya Waqf

Mwenyezi Mungu amehalalisha Waqf kwa sababu ya masilahi yake katika dini, dunia na Akhera. Kwa maana, mja anakuza malipo yake kwa kutoa Waqf ya mali yake kwa kutafuta uso wa Mwenyezi Mungu, na mazuri yake yanaendelea hata baada ya kifo chake. Mwenye kupewa Waqf hiyo ananufaika na mali hiyo, na anamwombea mwenye waqf hiyo, kwa hivyo jamii inaendelea kuwa na mshikamano zaidi.

Na waqf ni katika sadaka bora zaidi, kwa sababu ni sadaka ya kudumu iliyo dhabiti katika njia za wema na hisani.

Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, “Kabisa hamtafikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachokitoa, basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua vyema." (Al-Imran: 92)

Imesimuliwa kutoka kwa Ibn Umar, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema, "Umar alipata ardhi fulani huko Khaybar, kisha akamjia Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na akasema, 'Nimepata ardhi ambayo kamwe sijawahi kupata mali ya thamani zaidi yake. Basi unaniamrisha nifanyeje?" Mtume akasema, "Ukitaka, izuilie asili yake, na uitoe kama sadaka." Basi Umar akaitoa kama sadaka kwamba asili yake isiuzwe, wala isipeanwe kama zawadi, wala hairithiwi. Itumike kwa ajili ya masikini, jamaa wa karibu, katika kukomboa mateka (wafungwa), katika njia ya Mwenyezi Mungu, wageni, na wasafiri. Hakuna ubaya kwa mwenye kuisimamia kula humo kwa wema, au kumlisha rafiki yake, bila ya kujitengenezea mali kutoka humo. (Bukhari 2772, Muslim 1632)

Aina za Waqf

١
Kuweka Waqf kwa ajili ya masilahi ya kidini.
٢
Kuweka waqf kwa ajili ya masilahi ya kidunia.

Kuweka Waqf kwa ajili ya masilahi ya kidini

Kwa mfano, mtu anaweza kuweka waqf ya msikiti, shule, au nyumba kwa ajili ya wanyonge, maskini, mayatima, wajane, na mfano wa hao.

Kuweka waqf kwa ajili ya masilahi ya kidunia

Kama vile kujenga nyumba na kuifanya kuwa waqf kwa warithi wake, au afanye shamba kuwa waqf na kuyafanya mavuno yake kuwa yao.

Waqf inatimia na ni sahihi kwa moja ya mambo mawili:

١
Kauli: Kama vile kusema: Nimeweka waqf, au nimekizuilia, na mfano wa hayo.
٢
Kitendo: Kama vile ajenge msikiti na awaruhusu watu kuswalia ndani yake, au kujenga makaburi yenye ukuta na kuwaruhusu watu kuzikwa ndani yake, au kuanzisha shule na kuwaruhusu watu kusoma ndani yake, au kuchimba kisima na kuwaruhusu watu kunywa ndani yake.

Masharti ya Waqf

١
Mwenye kuweka waqf awe ana uwezo wa kutoa zawadi, na awe mmiliki wa kile anachokiweka kuwa waqf.
٢
Kile kinachowekwa kuwa waqf kinafaa kiwe ni mali ya kukaa kwa muda, inayojulikana, na inayomilikiwa na mtu anayeiweka kuwa waqf.
٣
Waqf hiyo iwe kitu kinachojulikana na inawezekana kufaidika kwacho bila ya kumalizika kwa chenyewe.
٤
Waqf hiyo iwe kwa ajili ya kitu cha wema kama vile misikiti, visima, jamaa za mtu na mafukara.
٥
Waqf hiyo iwe kwa kitu maalumu, kama vile msikiti, au aina maaulumu ya vitu, kama vile maskini, au mtu maalumu, kama vile Zaid, kwa mfano.
٦
Iwe waqf hiyo ni ya milele isiyo ya muda mfupi fulani, na iwe imeshahitimishwa siyo ile iliyofungamanishwa na kitu fulani, isipokuwa kama ataifungamanisha na kifo chake, basi hiyo itakuwa sahihi na inakuwa wasia.

Waqf haina kiasi maalumu, lakini hutofautiana kulingana na hali za watu katika utajiri na wasaa. Kwa hivyo, yule ambaye ni tajiri na hana mrithi, huyo anaweza kuweka mali yake yote kuwa waqf. Na yule ambaye ni tajiri na ana warithi, huyo anaweza kuzuia baadhi ya mali yake na awaachie hiyo nyingine warithi wake.

Waqf huwa bila ya kipimo na ni ya kudumu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mwenye Nguvu, Mtukufu na haina kipimo kuhusiana na muda wake. Kwa hivyo mwenye kuweka waqf ardhi yake, au nyumba, au shamba kwa ajili ya Mwenyezi Mwenye Nguvu, basi hiyo imeshatoka katika miliki yake na uendeshaji wake. Kwa hivyo, haiwezi kuuzwa wala kutolewa kama zawadi wala kurithiwa, wala kurudishwa, na warithi wake hawawezi kuiuza, kwa sababu iko nje ya umiliki wa maiti wao.

Ikiwa mtu atatamka kitu kwa matamshi ya kutoa waqf, au akatenda kitendo kinachoashiria kutoa waqf, basi waqf hiyo inamlazimu, na wala kuthibiti kwa waqf hakuhitaji kwamba waliowekewa waqf hiyo waikubali, wala hilo halihitaji idhini ya mtawala. Waqf inapothibiti, basi hairuhusiki kuitumia kwa njia inayoondoa sifa yake ya kuwa waqf.

Mwenyezi Mungu aliyetakasika, Mtukufu, ni mzuri, na hapokei isipokuwa vilivyo vizuri. Kwa hivyo, ikiwa Mwislamu anataka kutoa kitu kiwe waqf kwa kutafuta uso wa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu, Mtukufu, basi ni bora kwake kuchagua kilicho kizuri katika mali yake, na chenye thamani kwake na anachokipenda zaidi. Hilo ni katika ukamilifu wa wema na hisani.

Miongoni mwa milango bora zaidi ya kufanya waqf ni ile ambayo manufaa yake ni ya kujumuisha zaidi Waislamu katika kila wakati na mahali, kama vile kuweka waqf ya misikiti, wanafunzi, wapiganaji Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu Mtukufu, jamaa za mtu, Waislamu masikini na wanyonge wao, na mfano wa hao.

Miongoni mwa hukumu za Waqf

١
Ni sahihi kufanya waqf kwa ajili ya matajiri na maskini, walio karibu na walio mbali, na taasisi mbalimbali na watu binafsi.
٢
Inaruhusika kuweka waqf kwa ajili ya zaidi ya upande mmoja, kama vile kwa ajili ya masikini, wanazuoni, wanafunzi, na mfano wao.
٣
Si sahihi kuweka waqf kwa kitu ambacho kinaisha kinapotumika kama vile pesa, chakula, na vinywaji, na vile visivyoruhusika kuuzwa, kama vile rehani na kitu kilichoporwa.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani