Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Haki za wanawake katika Uislamu

Katika somo hili, tutajifunza kuhusu baadhi ya haki za wanawake katika Uislamu.

  • Tutaeleza tofauti iliyoko kati ya Uislamu kuwaheshimu wanawake na kudunishwa kwao na mataifa yaliyopita.
  • Tutafafanua misingi ya kiujumla jinsi Uislamu unavyoshughulikia suala la usawa wa kijinsia.
  • Tutawasilisha idadi ya haki za wanawake walizohakikishiwa na sheria za Kiislamu katika nyanja mbalimbali.

Uislamu kuwajali wanawake

Dini tukufu ya Kiislamu, pamoja na mafundisho yake matakatifu na mwongozo wake wa busara, ilimtunza mwanawake wa Kiislamu, ikahifadhi hadhi yake, ikahakikisha utukufu wake na furaha yake, na ikampa njia za kuishi vizuri, mbali na maeneo ya tuhuma, majaribio, uovu, na uharibifu. Haya yote ni katika rehema kubwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mwanamke haswa, na kwa jamii yote kwa ujumla. Utunzaji huu ni wa sampuli nyingi.

Heshima na hadhi ya juu

Uislamu umemhakikishia mwanamke hadhi yake na ubinadamu wake, na umempa nafasi yake anayostahili katika daraja yoyote anayoweza kuwa kama vile: mama, mke, binti, na daraja nyinginezo. Uliamrisha kwamba afanyiwe wema na kujaliwa kwa njia mahususi. Vile vile ulipigana dhidi ya itikadi mbovu zilizorithiwa za kidini, kiakili, na kijamii ambazo hupunguza hadhi ya mwanamke, kumdhalilisha na kumdunisha.

'Umar bin Khattab - Mwenyezi Mungu amridhie - alisema, “Wallahi (Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu), hakika sisi hatukuwa katika zama za Jahiliyya tukiwazingatia wanawake kuwa ni chochote, mpaka Mwenyezi Mungu alipoteremsha yale aliyoteremsha kuhusiana nao, na akawapa yale aliyowapa.” (Al-Bukhari 4913, Muslim 1479) Nuru ya Uislamu iliangaza kabla ya miaka 1400 iliyopita, ikiinua hadhi ya mwanamke, na kumuondolea udhalimu mwingi uliokuwa ukifanywa na mataifa na umma nyingi. Miongoni mwa hayo ni kwamba mwanamke hakuwa na haki ya kumiliki, wala kurithi, na alikuwa akirithiwa au kuchomwa moto pindi mumewe anapokufa, na vile vile alikuwa akiuzwa na kununuliwa. Desturi hii ilibakia imeenea - nchini Uingereza, kwa mfano - hadi mwanzo wa karne ya ishirini.

Kufanya uadilifu kati ya wanawake na wanaume

Uislamu ni dini ya Mola Mlezi wa walimwengu wote, Mwenye kujua yote, Mwenye hekima yote. Katika uadilifu wake na hekima yake ni kutosawazisha mambo mawili tofauti, na kutofautisha kati ya mambo mawili yanayofanana. Ndiyo maana tunapata sheria ya Kiislamu imesawazisha kati ya wanaume na wanawake katika yale wanayofanana na wako sawa ndani yake, na kutofautisha kati yao katika yale yaliyo tofauti, ambayo yalifanya haki na majukumu kulingana na maumbile ya kila mmoja wao na mahitaji yake na uwezo wake, na maumbile yao ya asili ambayo Mwenyezi Mungu aliwaumba kwayo. Uislamu umempa mwanamke nafasi yake inayomfaa katika nyanja zote, na ukasawazisha kati yake na wanaume katika nyanja nyingi, ikiwa ni pamoja na:

Chanzo cha uumbaji

Dharau ya mataifa yaliyotangulia ilifikia kumtoa mwanamke nje ya mipaka ya ubinadamu kamili. Aristoteli anasema: Mwanamke ni mwanamume ambaye ni mkamilifu, na maumbile asili yamemwacha katika ngazi ya chini ya ngazi za viumbe. Naye Sokrates anamfananisha na mti wenye sumu. Mkutano mkubwa ulifanyika Roma ambapo waliamua kwamba mwanamke hana roho wala hawezi kuishi milele, na kwamba hatarithi maisha ya Akhera, na kwamba yeye ni mchafu, na hapaswi kula nyama, wala kucheka, wala kuzungumza! Kwa upande wa Kifaransa, wao walifanya mkutano mnamo mwaka wa 586 kujadili suala "muhimu" ambalo ni: Je, mwanamke ni mwanadamu au si mwanadamu? Na je, ana roho au hana roho? Na ikiwa ana roho, je, ni roho ya kinyama au roho ya mwanadamu? Na ikiwa ni ya mwanadamu, je yeye yuko katika ngazi ya roho ya mwanamume au chini yake? Mwishowe, waliamua kwamba alikuwa mwanadamu, lakini aliumbwa kumtumikia mwanamume tu. Ama Uislamu, huo unakubali usawa wa jinsia mbili hizi katika asili ya uumbaji. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema, "Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliyewaumba kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume wengi na wanawake. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaomba, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalia." [An-Nisaa: 1]

Usawa wa kidini

Uislamu umefanya usawa baina ya mwanamume na mwanamke katika majukumu ya kisheria, na katika malipo na thawabu kwa hayo hapa duniani na Akhera. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, "Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyokuwa wakiyatenda." [An-Nahl: 97] Mwenyezi Mungu Mtukufu pia alisema, "Na anayefanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kiasi cha tundu ya kokwa ya tende." [An-Nisaa: 124] Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, - aliulizwa kuhusu mwanamume mmoja ambaye anapata unyevu (katika nguo zake), lakini hakumbuki kama alitokwa na manii usingizini. Akasema, "Aoge." Na akaulizwa kuhusu mwanamume ambaye anaona kwamba alitokwa na manii usingizini, lakini sasa haoni unyevu. Akasema, "Halazimiki kuoga." Basi, Ummu Sulaim akasema, "Mwanamke akiona hayo, je, ni lazima aoge?" Akasema, "Ndiyo. Hakika, wanawake ni washirika wa wanaume.” (Abu Dawud 236)

Wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume alikuwa ni mwanamke, ambaye ni mama wa waumini, Khadija, Mwenyezi Mungu amridhie. Vile vile wanawake walikuwa miongoni mwa wale waliohamia Uhabeshi mara ya kwanza. Vile vile walikuwa miongoni mwa wajumbe wa kwanza waliokuja kutoka Yathrib (Madina) na wakampa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ahadi ya utii.

Katika historia ya Uislamu, wanawake waliandika mifano angavu, ambayo walijulikana kwa sifa zao nzuri, wingi wa elimu yao na uelewa wao wa ujumbe wa Uislamu. Bali mara nyingi walikuwa watangulizi katika uwanja huu, kwani Waislamu walichukua mambo mengi ya dini yao kutoka kwa wanawake wa Kiislamu wa kupigiwa mifano, wenye elimu na watangulizi katika elimu na kufundisha, haswa mama wa waumini, Aisha, Mwenyezi Mungu awe radhi naye.

Mwanamke hushirikiana na mwanamume katika ibada za pamoja, za lazima, za kupendekezwa, na zinazoruhusiwa, kama vile 'Umrah, Hija, swala ya kuomba mvua inyeshe, Iddi mbili, swala ya Ijumaa na swala za mkusanyiko. Pia ameamrishwa kulingania Uislamu kwa kuamrisha wema na kukataza maovu. Na kuna mifano mingine iliyo wazi inayoonyesha usawa ilioko kati ya jinsia mbili hizi katika majukumu ya kisheria, na wala hawatofautishwi katika hayo isipokuwa katika mambo yanayohusiana na tofauti zilioko katika maumbile yao.

Ingawa Uislamu ulitambua kanuni ya usawa katika majukumu kama msingi wa ujumla, ulizingatia tofauti iliyoko katika maumbile ya jinsia mbili hizi, na majukumu tofauti yanayosababishwa na hilo. Kwa hivyo, Uislamu ukapanga majukumu haya na ukamweka kila mtu katika nafasi yake sahihi, jambo ambalo linasababisha kukamilishana katika maisha. Mwanamume anawajibika katika kutoa matumizi ya mkewe na watoto wake, na anapaswa kuwalinda na kuwashughulikia mambo yao yote ya kifamilia. Naye mwanamke anawajibika juu ya nyumba yake, mumewe na watoto wake, na ana majukumu ambayo anapaswa kuyabeba.

Uislamu umemhakikishia mwanamke haki zake za kiraia, kijamii na kibinafsi, ambazo ni haki alizohakikishiwa mwanamke tangu mwanzo wa ujumbe wa Uislamu zaidi ya miaka 1,400 iliyopita, na kabla ya kuanza kulinganiwa na mashirika ya kiraia na ya haki za binadamu katika zama za kisasa.

Haki za kiraia na za kijamii za mwanamke

١
Haki ya mwanamke ya kusoma na kufunza: Uislamu unahimiza juu ya elimu kwa wanaume na wanawake kwa njia sawa.
٢
Haki ya mwanamke ya kufanya kazi: Kanuni ya asili ni kwamba ni mwanamume anayelazimika kufanya kazi na kutoa matumizi ya familia yake, lakini hakuna chochote katika Uislamu kinachomzuia mwanamke kufanya kazi ikiwa anahitaji kuifanya, mradi tu ifanyike kwa mujibu wa hukumu za Kiislamu, mafundisho yake na maadili yake.
٣
Haki ya mwanake ya kurithi: Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Sunna za Mtume wake, na vitabu vya fiqh vimejaa maneno yanayozungumzia aina mbalimbali za urithi wa wanaume na wanawake.
٤
Haki ya mwanamke ya kumiliki mali: Mwanamke ana haki kamili ya kumiliki mali, ima kwa kile anachochuma kwa kufanya kazi au kwa kile anachorithi. Ana uhuru kamili wa kutumia kile anachomiliki, na ana dhima maalumu ya kimali, ambayo hafuati katika hilo baba, wala mume, wala wengineo.

Haki za mwanamke katika mambo ya kibinafsi na ndoa

١
Haki yake ya kuchagua mume sahihi, na kumkubali au kumkataa yule anayemposa.
٢
Haki yake ya mahari.
٣
Haki yake ya kutunzwa kimali, na mumewe kumpa matumizi, yeye na watoto wake.
٤
Haki yake ya kuishi pamoja na mumewe kwa wema, na kuamiliwa kwa maadili mema: kwa maneno na matendo.
٥
Haki yake ya kutendewa uadilifu katika ndoa ya zaidi ya mke mmoja.
٦
Haki yake ya kujitegemea kimali, na dhima yake ya kumiliki mali mbali na mumewe.
٧
Haki yake ya khul'u na haki yake ya kutafuta talaka na kuipata wakati yanapopatikana masharti yake na akawa anaistahiki.
٨
Haki yake ya kuwalea watoto wake baada ya talaka, isipokuwa akiolewa kwingine.

Hayo yaliyotangulia ni mifano tu ya kubainisha baadhi ya haki za mwanamke katika Uislamu. Vinginevyo, haki ambazo sheria ya Kiislamu imempa mwanamke ni nyingi sana.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani