Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Namna ya kuswali

Sheria imebainisha njia sahihi ya kuswali ili ikubalike kwa Mwenyezi Mungu. Katika somo hili, utajifunza kuhusu namna ya kuswali.

  • Kujua jinsi ya kuswali.

1. Nia

Niya ni sharti la kufanya swala iwe sahihi, yaani mwenye kuswali akusudie kwa moyo wake kumwabudu Mwenyezi Mungu katika swala yake hiyo huku akijua kuwa ni swala ya Maghrib - kwa mfano - au swala ya Ishaa, wala hairuhusiki kuitamka niya hii, bali nia ya moyoni na ya kiakili ndiyo inayotakiwa, na kuitamka ni makosa. Kwa sababu hilo halikupokewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wala maswahaba zake watukufu.

2. Takbira

Atasimama kwa ajili ya kuswali na aseme, "Allahu Akbar (Mwenyezi Mungu ndiye Mkubwa zaidi)" na atanyanyua mikono yake hadi urefu wa mabega yake au chini ya masikio yake, huku akivinyoosha vidole vyake, huku ameweka viganja vya mikono yake kuelekea Qibla.

Maana ya Takbira

Haifai kusema takbira isipokuwa kwa neno hili "Allahu Akbar (Mwenyezi Mungu ndiye Mkubwa zaidi)." Na maana yake ni ukuu na utukufu ni wake Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ndiye Mkubwa zaidi kuliko kila kitu. Ni Mkubwa zaidi kuliko dunia pamoja na kila kilichomo cha matamanio na starehe zake. Basi na tutupe starehe hiyo yote kando na tumgeukie Mwenyezi Mungu Mkubwa, Mtukufu katika swala kwa mioyo yetu na akili zetu kwa unyenyekevu.

3. Baada ya kusema “Allahu Akbar,” ataweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto juu ya kifua chake, na afanye hivyo hali ya kuwa amesimama wima.

4. Atafungua swala kwa yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, miongoni mwa dua za kufungua swala, na miongoni mwake ni, "Umetakasika ewe Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zako, na jina lako ni lenye baraka nyingi, na umetukuka utukufu wako, na hakuna mungu isipokuwa Wewe."

5. Atasema: "Najikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na Shetani aliyelaaniwa," na huko ndiko kumkimbilia Mwenyezi Mungu, na maana yake ni: Ninajikinga kwa Mwenyezi Mungu na ninajilinda kwake kutokana na shari ya Shetani.

6. Atasema: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwingi wa Kurehemu" na maana ya kusema hivi ni: Ninaanza kwa kutafuta msaada na baraka kwa jina la Mwenyezi Mungu.

7. Atasoma Suratul-Fatiha, ambayo ndiyo sura kubwa kabisa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu aliiteremsha sura hii kwa Mtume wake kama neema kutoka kwake. Alisema: "Na hakika tumekupa Aya saba zinazosomwa mara kwa mara, na Qur-ani Tukufu." (Al-Hijr: 87) Sura hii imeitwa hivyo kwa sababu ina Aya saba zinazorudiwarudiwa katika swala mara kadhaa kila siku.

Inamlazimu Muislamu kuihifadhi Surat Al-Fatihah. Kwa sababu kuisoma ni nguzo ya swala kwa anayeswali peke yake au ikiwa ni maamuma katika swala ambayo imamu hasomi kwa sauti kubwa.

Surat Al-Fatiha

8. Inajuzu kwake, baada ya kusoma Al-Fatihah au kuisikiliza wakati wa kisomo cha imamu, kusema: (Amin), na maana yake ni: Ewe Mwenyezi Mungu, tukubalie.

9. Baada ya Al-Fatiha katika rakaa ya kwanza na ya pili, atasoma sura nyingine au aya kadhaa kutoka katika sura nyingine. Ama rakaa ya tatu na ya nne, atasoma Al-Fatihah peke yake.

Kisomo cha Al-Fatihah na sura inayofuata kinafanywa kwa sauti kubwa katika Swala ya Alfajiri na rakaa ya kwanza na ya pili ya Swala ya Maghrib na Isha, na inasomwa kisiri kimya kimya adhuhuri na alasiri, na katika Swala ya Dhuhr na Asr, na katika rakaa ya tatu ya Maghrib, na katika rakaa ya tatu na ya nne katika swala ya Isha.

10. Kisha atasema takbira ya kwenda kwenye rukuu, akiinua mikono yake juu hadi mwenye mabega yake au juu zaidi, huku sehemu za ndani za viganja vyake zikielekea Kibla, kama alivyofanya katika takbira ya kwanza.

11. Atarukuu, kwa kuukunja mgongo wake kuelekea Kibla, na kuuweka mgongo wake kuwa katika kiwango sawa na kichwa chake, na ataweka mikono yake kwenye magoti yake, kisha atenganishe kati ya vidole vyake, na aseme: "Ametakasika Mola wangu Mlezi, Mkuu" na inapendekezwa kurudia kusema hivi mara tatu, lakini la wajibu ni mara moja tu. Na mtu anapaswa kumfanyia taadhima Mwenyezi Mungu katika rukuu na kumtukuza .

Maana ya "Ametakasika Mola wangu Mlezi, Mkuu" ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakasika na ametukuka kutokana na mapungufu. Haya atayasema kwenye kuswali hali ya kuwa amerukuu.

12. Atainuka kutoka kwenye rukuu asimame wima huku amenyanyua mikono yake sambamba na mabega yake na huku sehemu ya ndani ya vidole hivyo ikielekea Kibla, kama ilivyotangulia, akisemwa: "Mwenyezi Mungu amemsikia anayemhimidi" - ikiwa yeye ni imamu au ikiwa yuko peke yake - kisha wote watasema: "Mola wetu Mlezi, sifa njema zote ni zako".

Na inapendekezwa kwamba azidishe kusema: "..sifa nyingi, nzuri, zenye baraka, zenye kuijaza mbingu, na zenye kuijaza ardhi, na zenye kukijaza utakacho baada ya hayo".

13. Baada ya hayo, atashuka chini kwenye ardhi huku akisema Allahu akbar na asujudu juu ya viungo vyake saba, ambavyo ni: paji la uso pua, mikono miwili, na magoti mawili. Anapaswa kutenganisha kati ya mapaja na miguu katika hali anapokuwa amesujudu, na pia anainua mikono yake isilalale juu ya ardhi.

14. Katika sijda yake atasema: "Ametakasika Mola wangu Mlezi, Aliye juu zaidi" mara moja ambayo ndiyo wajibu, lakini inapendekezwa kurudia mara tatu. Maana ya "Ametakasika Mola wangu Mlezi, Aliye juu zaidi" ni kwamba ninamtakasa Mwenyezi Mungu, Aliye juu kwa ukuu na uwezo wake, na Aliye juu ya mbingu zake, aliye mbali na mapungufu na kasoro zote. Katika hili kuna tanabahisho kwa mtu aliyesujudu aliyeushikisha uso wake kwenye ardhi kwa kunyenyekea na kujidhalilisha kwamba akumbuke tofauti iliyo baina yake na Muumba wake aliye juu zaidi, kwa hivyo anakuwa ni mwenye kumnyenyekea Mola wake Mlezi.

Fadhila ya kusujudu

Kusujudu ni miongoni mwa aina kubwa kabisa za kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambapo Muislamu huomba humo baada ya kusema nyiradi za wajibu za hapo kwa kitu chochote anachokitaka cha duniani na Akhera. Amesema: “Mja huwa karibu zaidi na Mola wake Mlezi hali ya kuwa amesujudu, kwa hivyo, ombeni dua sana hapo.” (Muslim 482).

15. Kisha atasema: "Allahu Akbar", na akae baina ya sijda mbili, na imependekezwa kwamba aketi juu ya mguu wake wa kushoto, na ausimamishe mguu wake wa kulia, na aiweke mikono yake juu ya sehemu ya mbele ya mapaja yake, ambayo iko karibu na magoti yake.

Jinsi ya kukaa katika swala

Katika vikao vyote vya swala inapendekezwa njia ya kukaa iliyotangulia hapo awali, isipokuwa katika tashahhud ya mwisho, ambayo inapendekezwa ausimamishe mguu wake wa kulia kama ilivyotangulia, lakini autoe wa kushoto kutokea chini ya mguu wa kulia, kisha akae chini kwenye ardhi kwa makalio.

Dhikr ya baina ya sijda mbili

16. Atakapokuwa amekaa baina ya sijda mbili, aseme: "Mola wangu Mlezi, nisamehe", na inapendeza kuyarudia haya mara tatu.

17. Kisha atasujudu mara ya pili kama alivyosujudu mara ya kwanza.

18. Kisha atainuka juu kutoka kwenye sijda ya pili hadi kwenye hali ya kusimama, akisema (Allahu Akbar).

19. Ataswali rakaa ya pili sawa na ile ya kwanza.

20. Baada ya sijda yake ya pili katika rakaa ya pili, atakaa kwa ajili ya tashahhud kana kwamba amekaa baina ya sijda mbili, na ataashiria kwa kidole cha shahada cha mkono wake wa kulia kuelekea Kibla na aseme: "Maamkuzi mema, na rehema na mazuri yote, ni kwa Mwenyezi Mungu. Amani zishuke juu yako ewe Mtume, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake. Amani ishuke juu yetu, na juu ya waja wa Mwenyezi Mungu walio wema. Ninashuhudia kwamba hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu tu, na ninashuhudia kwamba Muhammad ni mja wake na ni mtume wake.”

21. Ikiwa swala hiyo ni rakaa mbili, kama vile alfajiri, basi atasoma swala ya Ibrahim, kisha atatoa salamu, na ufafanuzi wa hilo utakuja. Lakini ikiwa swala hiyo ni rakaa tatu, au rakaa nne, basi atanyanyuka amalize swala yake iliyobakia, isipokuwa atasoma Al-Fatiha tu katika rakaa ya tatu na ya nne.

22. Kisha katika rakaa ya mwisho baada ya sijda ya pili atakaa katika tashahhud ya mwisho. Atayakalia makalio yake na ausimamishe mguu wake wa kulia, na autoe nje mguu wake wa kushoto kutokea chini ya mguu wake wa kulia, na aseme aliyoyasema katika tashahhud ya kwanza, kisha atasema swala ya Ibrahim: “Ewe Mwenyezi Mungu, mrehemu Muhammad na jamaa zake Muhammad, kama ulivyowarehemu jamaa zake Ibrahim, hakika Wewe ni Mwenye kusifika Mtukufu. Na mbariki Muhammad na jamaa zake Muhammad, kama ulivyowabariki Ibrahim na jamaa zake, hakika Wewe ni Mwenye kusifika Mtukufu.”

Inapendekezwa aseme baada ya hayo: "Ninajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya Jahannamu, na kutokana na adhabu ya kaburini, na kutokana na majaribio ya uhai na ya kufa, na kutokana na majaribio ya Masihi-ddajjal.” kisha aombe chochote atakacho.

23. Kisha ataelekea upande wa kulia na aseme: "Assalamu alaikum, warahmatullah" kisha upande wa kushoto na aseme hivyo hivyo. Basi kwa kutoa salamu hizi Muislamu huwa amemaliza swala yake, kama alivyosema Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, “Kuianzisha kwake huwa kwa kusema takbira, na kumalizika kwake huwa kwa kutoa salamu” (Abu Dawud: 618, Tirmidhi: 3)

24. Inapendekezwa baada ya salamu ya swala ya faradhi kusema:

١
"Ninaomba msamaha kwa mwenyezi Mungu" mara tatu
٢
"Ewe Mwenyezi Mungu Wewe ndiye amani, na kwako ndiko kutokako amani. Umetukuka ewe mwenye utukufu, na ukarimu.”
٣
"Ewe Mwenyezi Mungu, hapana anayeweza kukizuia ulichokitoa, na wala kutoa ulichokizuia, na wala haumnufaishi mwenye utajiri, kwani Wewe ndiye mwenye utajiri."
٤
Kisha atasema "Ametakasika Mwenyezi Mungu" mara 33, "Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu" mara 33, na "Allahu akbar" mara 33.
٥
Atakamilisha mara mia kwa kusema: "Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke yake hana mshirika wake, ni wake Ufalme, na ni zake sifa njema, na Yeye juu ya kila kitu ni Mueza."

Je, afanye nini mtu ambaye hajahifadhi Al-Fatihah na dhikri za swala?

Ni lazima ajitahidi sana kukariri Al-Fatihah katika lugha ya Kiarabu kwa sababu haijuzu katika lugha nyingine yoyote, na pia ajitahidi kuhifadhi dhikri za faradhi katika Swala, nazo ni: 1. Al-Fatihah 2. Takbir 3. Ametakasika Mola wangu Mlezi, Mkuu 4. Mwenyezi Mungu amemsikia anayemsifu. Mola wetu Mlezi, sifa njema ni zako 5. Ametakasika Mola wangu Mlezi aliye juu kabisa 6. Mola wangu Mlezi, nisamehe 7. Tashahhud na kumswalia Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake 8. Kutoa salamu ya kumaliza swala.

Mpaka ahifadhi, inamlazimu arudie wakati wa Swala yale anayoyajua ya utukufu, sifa, na ukubwa, au arudie aya aliyoihifadhi atakapokuwa amesimama, kwa mujibu wa kauli yake Mola Mtukufu: "Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo." (At-Taghabun: 16).

Ama Muislamu mpya

Awe na hima kubwa - kiasi awezavyo - kuswali pamoja na mkusanyiko wa watu ili aishike sawasawa swala yake na kwa sababu imamu anambebea mamuma kiwango fulani cha upungufu katika swala.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani