Sehemu ya sasa:
Somo Mambo ya kiimani yanayohusiana na msimu wa baridi
Msimu wa baridi ni msimu wa mwaka uliowekwa na Mwenyezi Mungu kwa hekima kuu.
Neno msimu wa baridi lilitajwa katika Qur-ani Tukufu mara moja tu, katika Surat Quraish. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: "Kwa walivyozoea Maqureshi. Kuzoea kwao safari za siku za baridi na siku za joto." [Quraysh:1-2] Safari ya majira ya baridi ilikuwa ni Safari ya kibiashara ya Maquraishi kwenda huko Yemen, nayo safari ya siku za joto ilikuwa ile ya kwenda Sham.
Majira ya baridi ni kinyume na majira ya joto, nayo majira ya vuli na majira ya kuchipua ni yale yanayotenganisha kati ya misimu hii miwili. Ndiyo sababu baadhi ya wasomi wakasema: Mwaka una misimu miwili tu; majira ya joto na majira ya baridi.
Majira ya baridi ni moja ya udhihirisho wa uwezo, hekima na rehema za Mwenyezi Mungu:
Mwenyezi Mungu aliyetakasika aliyetakasika ndiye anayegeuza usiku na mchana, joto na baridi, majira ya joto na majira ya baridi. Mwenyezi Mungu alisema: "Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kuhitalifiana usiku na mchana, ziko Ishara kwa wenye akili." [Al-Imran: 190] Na hata kama tofauti hizi ni kwa sababu ya maumbile ya asili, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba visababu vyake.
Majira ya baridi ni fursa ya kufanya mazuri katika maisha na kukumbuka neema za Mwenyezi Mungu
Majira ya baridi na mabadiliko ya nyakati ni fursa ya kukumbuka kupita kwa umri, licha ya kwamba mwanadamu anapuuza sana katika kuutumia vizuri. Mtu anapaswa kukumbuka msimu wa baridi uliopita na jinsi ulivyopita haraka, kisha aone katika wakati huu mpya fursa nyingine ya kulipa upungufu uliokuwa katika wakati uliopita.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Naye ndiye aliyefanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anayetaka kukumbuka, au anayetaka kushukuru." (Al-Furqan: 62) Umar bin Khattab, Mwenyezi Mungu amridhie, alisema: "Fanya yale yaliyokukosa usiku wako katika mchana wako. Kwani Mwenyezi Mungu ameufanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anayetaka kukumbuka, au anayetaka kushukuru."
Majira ya baridi ni fursa ya kukumbuka neema za Mwenyezi Mungu kwa kutupa njia za kupata joto kutokana na sufu, vifaa, na mengineyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: "Na nyama hoa amewaumbia. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala." (An-Nahl: 5) Na haki ya neema hizi ni kushukuriwa. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: "Na alipotangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru, hakika nitawazidishia. Na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali." (Ibrahim: 7)
Katika ukali wa baridi kuna mazingatio na mawaidha tunayoyachukua kutoka katika hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Moto wa Jahannamu ulimlalamikia Mola wake Mlezi ukisema, 'Ewe Mola wangu Mlezi! Sehemu zangu zinajila zenyewe kwa zenyewe.' Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akauruhusu (moto huo) kuchukua pumzi mara mbili; moja katika majira ya baridi na nyingine katika majira ya joto. Na hii ndiyo sababu ya joto kali na baridi kali mnayopata (katika hali ya hewa)." (Bukhari 3260, Muslim 617)
Motoni wataadhibiwa kwa baridi kama vile watakavyoadhibiwa na joto. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hawataonja humo chochote kilicho baridi wala kinywaji. Ila maji ya moto sana na usaha. Ndiyo malipo mwafaka." [Al-Nabaa: 24-26] Ghassaq ni baridi kali ambayo inachoma kutokana na ubaridi wake. Wakazi wa motoni wataomba msaada kutokana na joto, lakini watasaidiwa kwa upepo baridi ambao ubaridi wake utavunja mifupa, kwa hivyo wataomba tena wasaidiwe kwa joto la Jahannam... Tunamwomba Mwenyezi Mungu usalama kutokana na hayo.
Baadhi ya watu wanaopenda kumuabudu Mwenyezi Mungu sana walisema: Sikuwahi kuona theluji ikianguka isipokuwa nilikumbuka kupeperuka kwa vitabu vya matendo siku ya kukusanywa watu na kutawanywa.