Sehemu ya sasa:
Somo Kushuhudia ya kwamba hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu
Uislamu ulilipa neno la Tauhid, yaani “Hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu" cheo kikubwa zaidi na kitukufu zaidi.
Cheo cha "Laa ilaaha illallah (Hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu)
Na kwa sababu ya hilo, kushuhudia kuwa, "Hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu," ndiyo wajibu mkuu zaidi na muhimu zaidi.
Maana ya Laa ilaha illa Allah "Hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu"
Inamaanisha kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na hilo ni kukataa uungu kwa kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu, aliyetakasika, Mtukufu, na kumthibitishia hilo Mwenyezi Mungu peke yake, asiyekuwa na mshirika.
Neno 'mungu' linamaanisha mwabudiwa ambaye nyoyo zinamnyenyekea zikimtukuza, kumuomba, kumwogopa, na kumtaraji. Kwa hivyo, atakayenyenyekea kitu, akakidhalilikia, akakipenda na akakitaraji, basi hakika atakuwa amekichukulia kuwa ni mungu na mwabudiwa. Na waabudiwa hao wote ni batili isipokuwa mungu mmoja tu. Naye ni Mola Mlezi, Muumbaji, aliyetakasika, Mtukufu.
Yeye aliyetakasika, Mtukufu, ndiye anayestahiki kuabudiwa na si mwingine. Naye ndiye ambaye nyoyo zinamuabudu kwa upendo, heshima, kumtukuza, kujidhalilisha, kumnyenyekea, kumhofu, kumtegemea, na kumuomba dua. Basi hapaswi kuombwa yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, na wala hauombwi msaada isipokuwa kwake, wala hategemewi isipokuwa Yeye tu, wala haiswaliwi swala isipokuwa kwa ajili yake tu, wala hakichinjwi chochote isipokuwa kwa ajili yake tu. Kwa hivyo, ni wajibu kumuabudu Yeye aliyetakasika, Mtukufu kwa ikhlasi. Kama alivyosema Mtukufu, "Na hawakuamrishwa isipokuwa kwamba wamwabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Yeye Dini." (Al-Bayyinah: 4)
Na mwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ikhlasi, akihakikisha maana ya "hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu," atapata furaha kubwa, na kufungukiwa, na maisha matukufu na mema. Kwani, nyoyo hazina utulivu wa kweli, wala kutua na kupata raha ya kiakili isipokuwa kwa kumfanyia Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake ibada. Kama alivyosema Yeye Mtukufu, "Mwenye kufanya mema, naye ni mwanamume au mwanamke, hali ya kuwa ni Muumini, basi tutamhuisha maisha mema." (An-Nahl: 97).
Nguzo za Laa ilaaha illa Lllah (hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu)
Na kila aina ya ibada inapaswa kufanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake, ambaye hana mshirika. Kwa hivyo, mwenye kumfanyia asiyekuwa Mwenyezi Mungu kitu, basi atakuwa amemshirikisha Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Yeye Mtukufu; "Na anayemuomba pamoja na Mwenyezi Mungu, mungu mwinginewe; hana ushahidi wa hili, basi bila ya shaka hesabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika, makafiri hawafanikiwi." (Al-Mu’minun: 117)
Maana ya "hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu" na nguzo zake ilikuja katika kauli yake Mola Mtukufu, "Basi anayemkufuru Taghut, na akamuamini Mwenyezi Mungu, bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika." (Al-Baqara: 256) Kwa hivyo, kauli yake, "Basi anayemkufuru Taghut," ndiyo maana ya nguzo ya kwanza "hakuna mungu." Na kauli yake, "na akamuamini Mwenyezi Mungu" ndiyo maana ya nguzo ya pili, "isipokuwa Mwenyezi Mungu."