Sehemu ya sasa:
Somo Kumswalia maiti na kumzika
Swala ya jeneza ni faradhi kwa waislamu wote waliohudhuria, si kwa kila mmoja miongoni mwao; kwani ni faradhi ya kutoshelezeana, kiasi kwamba baadhi yao wakimswalia, dhambi ya kutomswalia inaondolewa kwa waliobakia. Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipeana bishara nzuri kwa mwenye kuswalia jeneza kwamba atapata mlima mkubwa wa malipo na akasema: “Mwenye kuhudhuria jeneza mpaka maiti aswaliwe, basi atapata thawabu sawa na Qirat moja. Na mwenye kulisindikiza jeneza mpaka maiti azikwe, basi atapata thawabu sawa na Qirat mbili." Iliulizwa (ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu), "Qirat mbili ni nini?" Akasema, "Ni kama milima miwili mikubwa.” (Al-Bukhari 1325, Muslim 945)
Fadhila ya kuhudhuria swala ya jeneza
Kushuhudia swala ya jeneza na kulifuata kuna faida nyingi. Muhimu zaidi ni: kutimiza haki za maiti kwa kumswalia, kumfanyia uombezi, kumuombea dua, kutimiza haki za familia yake, kuwafariji kwa sababu ya msiba wao wa kufa kwa mtu wao, kupata malipo makubwa kwa wanaoshiriki katika mazishi yake, na kupata mawaidha na mazingatio kwa sababu ya kushuhudia jeneza hilo, makaburi na mengineyo.
1. Inapendekezwa kuswali swala ya jeneza katika mkusanyiko, na imamu awe mbele ya wale wanaoswalishwa kama ilivyo katika swala ya jamaa.
2. Maiti anafaa kuwekwa baina ya wale wanaoswali na Kibla, naye imamu atasimama kwenye kichwa cha maiti wa kiume na kwenye kiuno cha maiti wa kike, kama ilivyokuja kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. (Abu Dawud 3194)
-
Takbira ya kwanza
Mwenye kuswali atasema takbira ya kwanza, huku amenyanyua mikono yake mpaka ilingane na mabega yake, au kwenye masikio yake. Kisha atauweka mkono wake wa kulia kwenye sehemu ya juu ya mkono wake wa kushoto juu ya kifua chake, na asisome dua ya kufungua swala. Kisha atasema AudhubillahI mina shaitwanir-rajim (Ninajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutoka na shetani aliyelaaniwa). Kisha atasema Bismillah Rahmani Rahim (Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwingi wa kurehemu). Kisha atasoma suratul-fatiha kwa sauti ya chini.
Takbira ya pili
Kisha atasema takbira ya pili na baada yake atamswalia Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa namna yoyote ile, kama vile kusema: Ewe Mwenyezi Mungu, mpe rehema na amani Mtume wetu Muhammad. Na akimswalia Mtume kwa kamili kama anavyosema katika swala ya kawaida katika tashahhud ya mwisho, basi hivyo ndiyo bora zaidi. Atasema: "Ewe Mwenyezi Mungu, mswalie Muhammad na ukoo ya Muhammad, kama ulivyomswalia Ibrahim na ukoo wa Ibrahim. Hakika wewe ni Mwenye kuhimidiwa, Mwenye kutukuzwa. Ewe Mola, mbariki Muhammad na ukoo wa Muhammad kama ulivyombariki Ibrahim na ukoo wa Ibrahim. Hakika Wewe ni Mhimidiwa, Mwenye kutukuzwa)."
Takbira ya tatu
Kisha atasema Takbira ya tatu kisha atamuombea maiti rehema, msamaha, Pepo, na kuinuliwa daraja, kutokana na yale ambayo Mwenyezi Mungu atamfungulia katika moyo wake na ulimi wake. Iwapo atakuwa amehifadhi baadhi ya dua zilizopokelewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimfikie, kuhusu hilo, basi ni bora zaidi aombe kwa hizo.
Miongoni mwa dua zilizopokelewa ni: "Allahmmaghfirlahu warhamhu wa 'âfihi, wa'fu 'anhu, wa akrim nuzulahu wa was-si' mudkhalahu, waghsilhu bil-mâ-i wath-thalji wal-baradi, wa naq-qihi minal-khatwaayaa kamâ naq-qaytath-thawbal-abyadh minad-danasi, wa abdilhu dâran khayran min dârihi, wa ahlan khayran min ahlihi wa zawjan khayran min zawjihi wa adkhilhul-jannata wa a'idhhu min 'adhâbil-qabri wa min 'adhâbin-nâr. (Ewe Mwenyezi Mungu! Mghufirie na umrehemu na umuafu (umpe afya kutokana na uovu wowote), na umsamehe na umtukuze kushuka kwake (kaburini) na upanue kuingia kwake, na umuoshe kwa maji na theluji na barafu, na mtakase na makosa kama unavyoitakasa nguo nyeupe kutokana na uchafu, na mbadilishie nyumba bora kuliko nyumba yake na jamaa bora kuliko jamaa zake, na mke bora kuliko mke wake, na muingize peponi na mkinge na adhabu ya kaburi (na adhabu ya moto)." (Muslim 963)
Takbira ya nne
Kisha atasema Takbira ya nne na atulie baada yake kwa muda kidogo, kisha atatoa salamu upande wake wa kulia tu.
Inaruhusika kumswalia maiti msikitini, au katika sehemu maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya jambo hilo nje ya msikiti, au makaburini, hayo yote yamepokelewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.
Ni Sunna kuandaa mazishi haraka, kumswalia maiti, kumpeleka makaburini, na kumzika. Abu Huraira, Mwenyezi Mungu amridhie, alisimulia kuwa Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Iharakisheni jeneza. Ikiwa ni mtu mwema, basi ni heri mnayoitanguliza kwake. Na ikiwa ni kinyume chake, basi hiyo ni shari (mliyoibeba, na ambayo mnatakiwa kwa haraka) muishushe kutoka kwenye shingo zenu." (Bukhari 1315, Muslim 944)
Imependekezwa kwa anayefuata jeneza kushiriki katika kulibeba, ila hili litafanywa na wanaume tu, si wanawake. Ni Sunna kwa waendao kwa miguu pamoja na jeneza kuwa mbele yake na nyuma yake. Ikiwa makaburi yako mbali, au ikiwa kuna ugumu, basi hakuna ubaya kulibeba juu ya kipando au gari.
Mambo ya kuzingatia katika kuzika maiti.
Imependekezwa kwa waliohudhuria mazishi kumwombea uimara na msamaha maiti baada ya kuzikwa. Alikuwa Mtume, rehema na amani zimshukie anapomaliza kuzika maiti, anasimama na kusema: “Mtakieni msamaha ndugu yenu, na mumwombee uthabiti, kwani yeye sasa hivi anaulizwa.” (Abu Dawud 3221)