Sehemu ya sasa:
Somo Kufariji na kuomboleza kwa sababu ya kufiwa.
Kuwafariji waliofiwa
Inapendekezwa kuwafariji familia ya maiti, kuwaliwaza jamaa zake na kuwatia nguvu kwa sababu ya yale yaliyowasibu kwa maneno yoyote mazuri, ambayo yanajumuisha kumuombea dua maiti, kuwaimarisha na kuwasubirisha watu wa familia yake na jamaa zake na kuwakumbusha kutaraji malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie alisema huku akimfariji binti yake, Zainab mwanawe alipokufa: “Hakika, ni cha Mwenyezi Mungu alichokichukua, na ni chake Yeye alichopeana, na kila mmoja ana muda maalumu kwake Yeye. Na asubiri na atarajie malipo.” (Al-Bukhari 1284, Muslim 923)
Ndugu wa marehemu wanaweza kufarijiwa kabla na baada ya kuzika, mahali popote iwe msikitini, makaburini, nyumbani, kazini na penginepo.
Maandalizi ya mazishi hayafai kuwa kwa njia ya kupita kiasi kwa kuweka mahema, au kufanya karamu na kukusanya watu kwa ajili ya hilo. Hilo si katika Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na maswahaba zake watukufu. Tena hili sio tukio la furaha na raha ndiyo yafanywe hayo yote.
Kuhuzunika na kuomboleza kwa sababu ya kufiwa
Kulia ni huruma ya maumbile ya asili na kitu cha kuelelezea hisia ya kupoteza mtu na kuhuzunika. Macho ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, pia yaliwahi kutoa machozi kwa sababu ya kifo cha mwanawe, Ibrahim. (Al-Bukhari 1303, Muslim 2315)
Uislamu umeweka sheria kadhaa za kuhuzunika na kuomboleza juu ya maiti:
Kipindi cha kusubiri (Eda) kwa mwanamke ambaye mume wake amefariki.
Ni miezi minne na siku kumi. Ikiwa ni mjamzito, basi kipindi hicho kitaisha anapozaa.
Je, ni nini kinachomlazimu mwanamke katika kipindi cha kusubiri (Eda) baada ya kifo cha mumewe?
Ziara za makaburini: Ziara za makaburini zimegawanyika katika sehemu tatu:
Ziara zinazopendekezwa
Ni kuzuru makaburi ili kukumbuka mauti, kaburi na nyumba ya akhera. Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: “Nilikukatazeni kuzuru makaburi, lakini sasa yazuruni.” Na katika riwaya nyingine: “Kwa maana ziyara hiyo inakumbusha Akhera.” (Muslim 977, Tirmidhi 1054) Ziara hizi za makaburini zilizoruhusiwa ni zile ambazo huwa katika nchi hiyo aliyomo mtu, na haihusishi kusafiri kwa ajili ya kwenda kuzuru kaburi. Safari kama hizo zinaruhusika tu ikiwa ni kwenda katika ile misikiti mitatu, jambo ambalo linachukuliwa kwamba ni ibada.
Ziara inayoruhusiwa.
Ni kuzuru kwa ajili ya makusudio yanayoruhusiwa, si kwa ajili ya kukumbuka mauti, na wala hakujumuishi chochote kilichoharamishwa, kama vile kuzuru kaburi la jamaa au rafiki, na siyo katika nia na makusudio yake kukumbuka nyumba ya Akhera.
3. Ziara iliyoharamishwa.
Ni ziara ambayo huambatana na baadhi ya mambo haramu, kama vile; kukaa juu ya kaburi, kutembea juu yake, kujipiga makofi, kulia kwa kuinua sauti juu, au ziara iliyoambatana na mambo ya uzushi, kama vile kumuomba Mwenyezi Mungu kupitia mwenye kaburi hilo, au kutafuta baraka kutoka kwa kaburi hilo na kujipangusa juu yake, au vitendo vya ushirikina kama vile kumtaka mwenye kaburi atimize haja zake na kutafuta msaada wake.
Ziara ya Mwislamu kwenye makaburi inapaswa kuwa na madhumuni kadhaa:
Wakati wa kutembelea makaburi, mtu anafaa kutahadhari kutoketi au kutembea juu ya makaburi ili kumheshimu maiti huyo na kumkirimu. Ndiyo maana Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, akaelezea adhabu ya hili akisema: "Mmoja wenu kukaa juu ya kaa na likachoma nguo zake hadi likafikia ngozi yake, ni bora kwake kuliko kukaa juu ya kaburi." (Muslim 971)
Dua ya kuomba makaburini
Miongoni mwa dua zinazotajwa wakati wa kuzuru makaburi ni: “Amani iwe juu yenu, nyumba ya watu waumini, na hakika Mwenyezi Mungu akipenda tutawafuata.” (Muslim 249) Au: “Amani iwe juu ya wakazi wa makazi haya, miongoni mwa Waumini na Waislamu. Mwenyezi Mungu awarehemu waliotangulia miongoni mwetu na waliobakia. Na hakika Mwenyezi Mungu akipenda tutawafuata.” (Muslim 974) “Amani iwe juu yenu, enyi wakazi wa nyumba hii miongoni mwa Waumini na Waislamu. Na sisi tutafuata Mwenyezi Mungu akipenda. Ninamuomba Mwenyezi Mungu salama kwa ajili yetu na kwa aliji yenu.” (Muslim 975)