Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Fadhila za Qur-ani Tukufu

Qur-ani Tukufu ina fadhila nyingi zinazoonyesha heshima na hadhi ya kitabu hiki kikuu. Katika somo hili, utajifunza kuhusu baadhi yake.

  • Fadhila za Qur-ani Tukufu

Fadhila za Qur-ani Tukufu

Qur-ani Tukufu ina fadhila kubwa, na miongoni mwake ni kama ifuatavyo:

1. Heri iliyo katika kujifunza na kufundisha Qur-ani

Imesimuliwa kutoka kwa `Uthman bin 'Affan kuwa: Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema, "Mbora wenu ni yule aliyejifunza Qur-ani na akaifunza (wengine)." (Al-Bukhari 5027)

2. Watu wa Qur-ani ndio watu maalumu wa Mwenyezi Mungu

Imesimuliwa kutoka kwa Anas bin Malik, Mwenyezi Mungu amridhie, kutoka kwa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa alisema: "Hakika Mwenyezi Mungu ana watu wake miongoni mwa watu." Wakasema: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni akina nani hao?' Akasema: "Hao ni watu wa Qur'ani, watu maalumu wa Mwenyezi Mungu." (Ibn Majah 215)

3. Kuzidishiwa thawabu mizidisho mingi kwa kusoma herufi moja katika Qur-ani

Imesimuliwa kutoka kwa Abdullah bin Masud, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: "Mwenye kusoma herufi moja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi anaandikiwa tendo jema moja. Na tendo jema linalipwa mfano wake mara kumi. Sisemi kwamba Alif Laam Miim ni herufi moja, bali Alif ni herufi, Laam ni herufi na Miim ni herufi." (Imepokelewa na Tirmidhi 2910)

4. Kuteremka kwa malaika, utulivu na rehema katika mabaraza ya kusomea Qur-ani na kuidurusu:

Imesimuliwa kutoka kwa Abu Huraira, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Watu hawatakusanyika ndani ya nyumba mojawapo ya nyumba za Mwenyezi Mungu wakikisoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu na wakifundishana kitabu hicho, isipokuwa utulivu utawateremkia, na rehema itawagubika, na malaika watawafunika, na Mwenyezi Mungu atawataja mbele ya wale walioko kwake." (Muslim, 2699)

5. Uombezi wa Qur-ani kwa watu wake

Imesimuliwa kutoka kwa Abu Umama Al-Bahli, kuwa alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akisema: “Isomeni Qur-ani; kwa sababu itakuja Siku ya Kiyama kama mwombezi kwa watu wake.” (Muslim 804)

6. Mwenye ustadi mkubwa katika Qur-ani yu pamoja na malaika, na mwenye kupata shida katika kuisoma atapata malipo mara mbili

Imesimuliwa kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: "Mwenye ustadi mkubwa katika kusoma Qur-ani yu pamoja na (malaika) waandishi watukufu wema. Na anayeisoma Qur-ani huku anapata uzito katika hilo, huku ni ngumu kwake, ana malipo mara mbili." (Muslim 798)

7. Qur-ani humuinua mtu wake

Imesimuliwa kutoka kwa 'Umar bin Khattab, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Hakika, Mwenyezi Mungu huwainua baadhi ya watu kwa Qur-ani hii, na huwaangusha wengine kwayo.” (Muslim 817)

8. Mwenye kuhifadhi Qur-ani, atainuka juu katika daraja za Peponi kwa kiasi alicho nacho cha Qur-ani

Imesimuliwa kutoka kwa Abdullah bin Amr bin Al-Aas, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, kuwa alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema: "Mwenye (kuhifadhi) Qur-ani ataambiwa: Soma, panda, na ukariri kama ulivyokuwa ukikariri katika dunia. Kwani mashukio yako yatakuwa kwenye aya ya mwisho utakayoisoma." (Abu Daawud 1464)

9. Mwenye Qur-ani atavaa mapambo na taji la heshima Siku ya Kiyama

Imesimuliwa kutoka wa Abu Huraira Mwenyezi Mungu amridhie kuwa: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Qur-ani itakuja Siku ya Kiyama na itasema: 'Ewe Mola Mlezi, mvishe mapambo.' basi atavishwa taji la heshima. Kisha itasema: 'Ewe Mola Mlezi, mzidishie' kwa hivyo, atavalishwa pambo la heshima. Kisha itasema: 'Ewe Mola Mlezi, mridhie' basi atamridhia. Kisha ataambiwa: 'Soma na upande' na ataongezwa jema moja kwa kila aya." (Tirmidhi 2915)

10. Mwenyezi Mungu Mtukufu atawatukuza wazazi wa mtu aliyehifadhi Qur-ani kwa aina mbalimbali kubwa

Imesimuliwa kutoka kwa Sahl bin Mu'adh kutoka kwa baba yake, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Mwenye kuisoma Qur-ani na akafanya yaliyomo ndani yake, wazazi wake watavishwa taji Siku ya Kiyama. Mwangaza wake utakuwa bora kuliko mwangaza wa jua katika nyumba za dunia kama ingekuwa miongoni mwenu. Basi mnamuonaje yule aliyeifanyia hii Qur-ani kazi?" (Abu Dawud 1453)

11. Kuihifadhi Qur-ani na kujifunza ni bora kuliko dunia na vilivyomo ndani yake

Imesimuliwa kutoka kwa 'Uqba bin Amir, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa alisema: Tulipokuwa As-Suffa, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alitoka nje na akasema, "Ni nani miongoni mwenu angependa kwamba akwende kila asubuhi huko But-han au Al-'Aqiiq na aje na ngamia wawili wa kike wakubwa kutoka huko bila ya kupata dhambi yoyote wala kukata mahusiano ya kijamii?" Tukasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tungependa hilo." Akasema, "Kwa nini asiende mmoja wenu asubuhi katika msikiti na akajifunza au akasoma aya mbili katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu. Hilo ni bora kwake kuliko ngamia wawili wa kike. Na aya tatu ni bora kwake kuliko ngamia watatu wa kike. Na aya nne ni bora kwake kuliko ngamia wanne wa kike. Na aya zaidi ya aya nne ni bora kwake kuliko idadi kama hiyo ya ngamia wa kike." (Muslim 803)

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani