Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Msingi wa kuchagua mume na mke

Katika somo hili, tutajifunza kuhusu kanuni muhimu zaidi za kuchagua mwanandoa.

  • Kujua hadhi ya mkataba wa ndoa katika Uislamu.
  • Kujua vidhibiti muhimu zaidi katika kuchagua mwanandoa.
  • Kubainisha uadilifu wa Uislamu kwa mwanamke katika utaratibu wa kuchagua mume.

Mkataba wa ndoa ni miongoni mwa mikataba muhimu na yenye hadhi ya juu kabisa katika Uislamu. Sheria ya Uislamu imeuzunguka mkataba huu kwa hatua za awali, ambazo hutayarisha kila mhusika kwa yale yanayofikia masilahi yake na manufaa yake kutokana na mkataba huo, na kusaidia kuendelea kwa ndoa na utulivu katika nyumba ya Mwislamu.

Nguzo za familia

Nguzo mbili kuu katika kujenga familia ni mume na mke. Sheria imefanya bidii kudumisha uhusiano mzuri kati yao, na ikafanya kutimia hilo kuwa miongoni mwa ishara za (Mwenyezi Mungu) na neema zake ambazo amewaneemesha vyazo waja wake.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na katika Ishara zake ni kuwa amewaumbia wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejalia mapenzi na rehema baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaotafakari." [Ar-Rum: 21]

Uchaguzi mzuri wa mwanandoa

Kuchagua mwenza wa maisha ni hatua muhimu zaidi ya kufikia ndoa yenye furaha na kujenga familia thabiti.

Kanuni muhimu zaidi katika kuchagua wanandoa

١
Unyoofu wa dini na maadili
٢
Kuridhika kisaikolojia
٣
Kujitosheleza

Unyoofu wa dini na maadili

Hii ndiyo kanuni ambayo mume na mke wanapaswa kuzingatia wakati wa kuchagua mwenza wa maisha. Unyoofu wa dini na maadili, Mwenyezi Mungu akipenda, huhakikisha furaha katika nyumba hizi mbili.

Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amehimiza kuchagua mke mchamungu na mwenye dini. Alisema: “Mwanamke huolewa kwa vitu vinne: mali yake, nasaba yake, urembo (uzuri) wake na dini yake. Basi mchague mwenye dini, na ila, mikono yako itajaa vumbi.” (Al-Bukhari 5090 na Muslim 1466) Mwanamke wa dini humcha Mwenyezi Mungu na huzingatia haki za nyumba yake na mume wake, akiwapo na pia asipokuwapo.

Kuhusiana na kuchagua mume, Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Akikujieni mtu ambaye mmeridhika na tabia yake na dini yake, basi muozesheni. Msipofanya hivyo kutakuwa na majaribio katika ardhi na uharibifu ulioenea.” (Ibn Majah 1967) Baadhi ya waliotangulia walikuwa wakisema: 'Ukimwoza binti yako, muozeshe kwa mtu mwenye dini. Kwani akimpenda, atamheshimu na akimchukia, hatamdhulumu.'

Kuridhika kisaikolojia

Amesema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Roho (nafsi) ni kama mkusanyiko wa majeshi: Zile ambazo zinafanana katika sifa zake, basi hizo huingiliana (huelewana), lakini zile ambazo zinatofautiana katika sifa zake, basi hizo hutofautiana." (Al-Bukhari 3336, na Muslim 2638) Hili linasisitiza umuhimu wa kuridhika kisaikolojia na utangamano mzuri kati ya wanandoa, ili muungano uweze kutokea, na maisha ya ndoa yenye furaha yaendelee.

Kwa hivyo, Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alimuamrisha mtu anayetaka kumchumbia mwanamke akisema: “Mtazame. Kwani hilo huleta uwezekano mkubwa wa kuwepo maelewano baina yenu.” (Tirmidhi 1087) Maana yake ni kwamba mapenzi baina yao hudumu. Kumtazama mwenza wakati wa kuposa ni haki ya mwanamume na mwanamke pia; ili kila mmoja wao amjue mwenzake na atulizane kuhusiana na hilo.

Kujitosheleza

Kinachokusudiwa hapa ni kuwepo ukaribu na kuafikiana baina ya wanandoa katika hali zao za kifedha na kijamii. Baadhi ya wanazuoni wanaona kwamba hili ni sharti, huku wengine wakaona kinachozingatiwa ni dini tu na maadili. Lakini hakuna shaka kwamba ikiwa hakuna ukaribu katika kiwango cha kijamii, kielimu na kifedha kati ya wenzi wa ndoa, basi hilo huenda likawa sababu ya kutikisa na kutishia maisha ya kindoa na kupelekea kuvunjika kwake.

Kuridhika na kukubali

Pamoja na kuzingatia kufanya uchaguzi mazuri wa mwenza, ni lazima ndoa itimie kwa ridhaa na kukubali kwa pande zote mbili, bila shinikizo kutoka kwa mtu yeyote, hata kama ni kutoka kwa mmoja wa watu wa karibu zaidi nao.

Uislamu umemtendea haki mwanamke na ukaweka sharti kwamba ni lazima amridhie na amkubali mume huyo. Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: “Mjane (mwanamke ambaye amewahi kuoleka) hapaswi kuozeshwa isipokuwa baada ya kushauriana naye. Naye bikira hapaswi kuozeshwa ila baada ya kutafuta ruhusa yake." Watu waliuliza, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ruhusa yake huwa vipi?" Akasema, "Ni akinyamaza." (Al-Bukhari 5136, na Muslim 1419) Na katika kisa cha Khansa bint Khudham al-Ansariyya kuwa kwamba, “Baba yake alimwozesha ilhali ni mjane, kwa hivyo akalichukia hilo. Basi akamjia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, naye akaibatilisha ndoa yake hiyo." (Al-Bukhari 5138)

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani