Sehemu ya sasa:
Somo Kuamini umola wa Mwenyezi Mungu
Maana ya Tauhidi ya umola
Ni kukiri na kusadiki kwa uthabiti kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Mola Mlezi wa kila kitu, Mmiliki wake, Muumba wake, Mlinzi wake, Mwenye kuwaruzuku, na kwamba Yeye ndiye Mwenye kuhuisha, Mwenye kufisha, Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru, ambaye mambo yote ni yake, na kwamba heri iko mkononi mwake, na kwamba ni Muweza juu ya kila kitu wala hana mshirika yeyote. Kwa hivyo, Tauhidi ya umola ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika matendo yake, na hilo ni kwa kuitakidi mambo kadhaa:
Kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Muumba wa kila kitu kilicho katika ulimwengu, na hakuna muumbaji asiyekuwa Yeye, kama alivyosema Yeye Mtukufu, "Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu." (Az-Zumar: 62) Ama kuumba kwa mwanadamu, hilo ni kubadilisha kitu kutoka katika sifa moja hadi nyingine, au kukusanya na kuunganisha, na mfano wa hayo, na si uumbaji halisi, wala kuleta kitu baada ya kutokuwepo kwake, wala kufufua baada ya kufa.
Na kwamba Yeye ndiye Mwenye kuwaruzuku viumbe vyote, na hakuna mwenye kuruzuku asiyekuwa Yeye. Kama alivyosema Yeye Mtukufu, "Na hakuna mnyama yeyote katika ardhi isipokuwa riziki yake ni juu ya Mwenyezi Mungu." (Hud: 6).
Na kwamba Yeye ndiye Mmiliki wa kila kitu, na hakuna mmiliki halisi asiyekuwa Yeye. Kama alivyosema Yeye Mtukufu, "Ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi na vile vilivyomo."(Al-Ma'idah: 120)
Na kwamba Yeye ndiye mwendashaji wa kila kitu, na hakuna mwendashaji mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mtukufu, "Anapitisha mambo yote yaliyo baina mbingu na ardhi." (As-Sajdah: 5)
Uendeshaji wa Mwenyezi Mungu, na uendeshaji wa mwanadamu
Ama uendeshaji mambo wa mwanadamu katika mambo yake, maisha yake, na kuyapangilia kwake, hayo yana mipaka tu kwa kile kilicho chini ya mkono wake, na kile anachomiliki na anachoweza. Na huo uendeshaji wake huenda ukuzaa matunda na huenda ukafeli. Lakini uendeshaji wa Muumba, aliyetakasika, Mtukufu ni kwa jumla, na hakuna chochote kinachotoka ndani yake, nao ni wa kutekelezeka, hakuna chochote kinachoweza kuuzuia, na wala hakuna kinachoweza kuupinga. Kama alivyosema Mtukufu, "Fahamuni! Kuumba ni kwake, na amri. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote." (Al-A’raf: 54)
Washirikina wa Kiarabu katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakikiri Umola wa Mwenyezi Mungu:
Walikiri makafiri katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumbaji, Mmiliki na Mwendeshaji mambo. Amesema Mtukufu, "Na ukiwauliza: Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu." (Luqman: 25) Lakini hilo pekee halikuwaingiza katika Uislamu. Kwa sababu, hawakumfanyia Mwenyezi Mungu peke yake ibada. Bali waliabudu wengine pamoja naye. Basi mwenye kukiri kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu - yaani, Muumba wao, Mmiliki wao, na Mlezi wao kwa neema zake - inamlazimu ampwekeshe Mwenyezi Mungu katika ibada, na azielekeze kwake peke yake, bila ya mshirika.
Basi inawezekanaje kuingia akilini kwamba mtu akiri kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Muumba wa kila kitu na mwendeshaji wa ulimwengu, Mwenye kuhuisha, Mwenye kufisha, kisha akaelekeza kitu katika aina za ibada kwa asiyekuwa Yeye? Huu ndio udhalimu mbaya zaidi na kubwa zaidi ya dhambi zote. Na ndiyo maana Luqman akamwambia mwanawe alipokuwa akimnasihi na kumuelekeza, "Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani, hakika ushirikina bila ya shaka ni dhuluma iliyo kubwa." (Luqman: 13)
Na alipoulizwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, "Ni dhambi ipi iliyo kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu? Akasema, "Ni umfanyie Mwenyezi Mungu mwenza ilhali Yeye ndiye aliyekuumba.” (Bukhari 4477, Muslim 86)
Mja atakapojua kwa yakini kwamba hakuna hata mmoja katika viumbe anayeweza kutoka katika mipangilio ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mtukufu, Aliye juu ndiye Muumba wake vyote, na hakuna muumba isipokuwa Yeye, na kwa sababu Yeye ndiye Mmiliki wao. Anawaendesha namna atakavyo kulingana na hekima yake. Na anapojua kuwa jambo lote liko mkononi mwake, Yeye Mtakatifu, na hakuna mwendesha ulimwengu isipokuwa Yeye peke yake, na wala haisogi chembe moja isipokuwa kwa idhini yake, na wala haitulii isipokuwa kwa amri yake. Na anapojua kwa elimu ya yakini kwamba hakuna mwenye kuruzuku isipokuwa Mwenyezi Mungu, hilo linamletea utulivu wa moyo, na kufungamana na Mwenyezi Mungu peke yake, na kumuomba na kumhitaji Yeye, na kumtegemea Yeye pekee katika mambo yote ya maisha yake.