Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Uhakika wa ibada

Ibada ina nafasi kubwa katika dini ya Kiislamu. Somo hili litazungumzia maana yake, uhakika wake, nguzo zake, na hekima iliyo nyuma ya kuwepo ibada mbalimbali.

  • Kujua maana na uhakika wa ibada.
  • Kujua nguzo na aina zake.
  • Kujua baadhi ya hekima za kuwepo ibada mbalimbali.

Maana ya ibada

Ibada ni jina linalojumuisha kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu anakipenda na kuridhia miongoni mwa maneno na vitendo, ya ndani na ya nje. Kwa hivyo, kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu anakipenda miongoni mwa matendo na maneno kinachukuliwa kuwa ni ibada.

Uhakika wa ibada

Ibada ni utiifu wa kila aina kwa Mwenyezi Mungu, kwa upendo, utukufu, na kunyenyekea. Nayo ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya waja wake, na ni mahsusi kwake pekee. Ibada inajumuisha kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu anakipenda na anachoridhia miongoni mwa maneno na vitendo alivyoviamrisha na akawaamrisha watu kufanya, sawa yawe ni katika matendo ya dhahiri kama vile swala, zaka, na Hija, au katika matendo ya ndani kama vile kumdhukuru Mwenyezi Mungu kimoyomoyo, kumhofu, kumtegemea, kumuomba msaada na mengineyo.

Katika rehema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni kwamba aliwawekea aina mbalimbali za ibada, ikiwa ni pamoja na:

١
Ibada za moyoni: Hizi ni kama vile kumpenda Mwenyezi Mungu, kumhofu, kumtegemea. Na hizi ndizo ibada na bora zaidi.
٢
Ibada za kimwili: MiongoNi mwake kuna zile ambazo huwa kwa ulimi tu, kama vile kumdhukuru Mwenyezi Mungu, kusoma Qur-ani na kusema maneno mazuri. Na baadhi yake huwa kwa viungo viginevyo kama vile wudhuu, saumu, swala, na kuondoa udhia kwenye barabara.
٣
Ibada za kimali: Nayo ni kama vile zaka, sadaka, na kutoa matumizi katika njia za heri.
٤
Na miongoni mwake kuna zile zinazojumuisha hayo yote kama vile Hija na Umra.

Hekima ya kuwepo ibada tofauti tofauti

Miongoni mwa hekima za Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwamba aliwawekea waja wake ibada mbalimbali na nyingi, ili mtu apate nguvu ndani yake na shauku ya kufanya ibada, ili asichoke, na pia ili mtu aelekee kufanya ibada ambayo anaiona moyo wake ukiielekea.

Kama vile matendo ya ibada yanavyotofautiana, watu pia hutofautiana katika mielekeo yao na uwezo wao. Baadhi yao hupata ukakamavu na bidii katika ibada moja kuliko nyingine. Pengine mmoja wao anawezafanya kupenda kuwafanyia watu wema, naye mwingine huenda amerahisishiwa kufunga saumu za hiari; naye wa tatu huenda moyo wake umefungamana na kusoma na kuhifadhi Qur-ani.

Amesema Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Kwa hivyo, yeyote aliyekuwa miongoni mwa wale wenye kudumisha swala, basi ataitwa kutoka kwenye mlango wa swala. Na yeyote aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa wakishiriki katika Jihadi, basi ataitwa kutoka kwenye mlango wa Jihadi. Na yeyote aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa wakifunga swaum, basi ataitwa kutoka kwenye mlango wa Ar-Rayyaan. Na yeyote aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa wakitoa sadaka, basi ataitwa kutoka kwenye mlango wa sadaka." Abu Bakr akasema, "Na wazazi wangu wakatolewe kama dhabihu kwa ajili yako, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!" Hakuna dhiki wala haja yeyote itakayompata yeye atakayeitwa kutoka kwenye milango hiyo yote. Je, kutakuwa na mtu yeyote atakayeitwa kutoka kwenye milango hii yote?" Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake akajibu, "Ndiyo. Na ninatumai kwamba wewe utakuwa mmoja wao." (Al-Bukhari 1897, Muslim 1027)

Ibada inajumuisha nyanja zote za maisha.

Ibada inajumuisha matendo yote ya Muumini ikiwa ataweka nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Ibada katika Uislamu haikomei kwenye ibada mfano wa swala, saumu na zinginezo. Bali matendo yote yenye manufaa yaliyofungamanishwa na nia njema, makusudio sahihi yanakuwa ibada ambazo mja analipwa juu yake. Mfano, ikiwa Muislamu atakula chakula, au akanywa au akalala kwa nia ya kupata nguvu ya kufanya utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi atalipwa kwa hilo.

Muislamu anaishi maisha yake yote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Yeye anakula ili apate nguvu ya kumtii Mwenyezi Mungu, kwa hivyo kula kwake kwa nia hii kunakuwa ibada. Na anaoa ili kujiepushe na mambo ya haramu, basi kuoa kwake huku kunakuwa ibada. Na kwa mfano wa nia hii, inakuwa biashara yake, kazi yake, na kuchuma kwake mali ni ibada. Na kutafuta kwake elimu, utafiti wake, ugunduzi wake, na uvumbuzi wake ni ibada. Na utunzaji wa mwanamke mume wake, watoto wake, na nyumba yake ni ibada. Na vivyo hivyo katika nyanja zote za maisha, matendo yake, na mambo yake yenye manufaa, maadamu yote hayo yanaambatana na nia njema na makusudio mazuri.

Ibada ndiyo hekima nyuma ya kuumba viumbe:

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti." (Dhariyat: 56-58)

Mwenyezi Mungu Mtukufu alituambia kuwa hekima ya kuumbwa kwa majini na wanadamu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi hahitaji ibada zao. Lakini wao ndio wanaohitaji kumuabudu, kwa sababu ya haja yao kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Iwapo mtu atapuuza lengo hilo na kujiingiza katika anasa za kidunia bila kukumbuka hekima ya Mwenyezi Mungu ya kuwepo kwake; basi atabadilika na kuwa kiumbe kisichokuwa na faida yoyote tofauti na viumbe wengine katika sayari hii. Kwa sababu wanyama wanakula na wanafanya pumbao pia, ingawa wao hawatafanyiwa hesabu akhera tofauti na mwanadamu. Amesema Mwenyezi Mungu: "Na wale waliokufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makazi yao." (Muhamad: 12) Hapo wao huwa wamefanana na wanyama katika matendo yao na malengo yao, isipokuwa wao watakutana na malipo ya juu ya hayo. Kwa sababu wana akili ambazo wanatambua na kuelewa kwazo, tofauti na wanyama ambao hawana akili.

Nguzo za ibada

Ibada ambayo Mwenyezi Mungu aliamuru inategemea juu ya nguzo tatu muhimu, ambazo kila moja yake inakamilisha nyinginezo.

Nguzo za ibada

١
Kumpenda Mwenyezi Mungu aliyetakasika
٢
Kujidhalilisha na kumhofu Mwenyezi Mungu
٣
Kumtumaini na kuwa na dhana nzuri kwa Mwenyezi Mungu

Ibada ambazo Mwenyezi Mungu aliwafaradhishia waja wake ni lazima ijumuishe unyenyekevu udhalilifu kamili kwa Mwenyezi Mungu, na kumuogopa pamoja na kumpenda kikamilifu, kumtaka na kumtumaini.

Kwa hivyo, mapenzi ambayo hayaambatani na hofu wala kujidhalilihfu - kama vile kupenda chakula na mali - siyo ibada. Na vile vile kuhofu bila ya upendo - kama vile kuhofu mnyama anayewala watu na mtawala dhalimu - haya yote hayazingatiwi kuwa ni ibada. Kwa hivyo hofu, upendo, na matumaini vinapojumuika pamoja katika tendo, basi tendo hilo linakuwa ibada. Na ibada haiwi ila kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee.

Kwa hivyo, Muislamu akiswali au kufunga saumu, na yakawa makusudio yake katika kufanya hivyo ni kumpenda Mwenyezi Mungu, kutaraji malipo yake, na kuogopa adhabu yake, basi anakuwa katika ibada. Lakini ikiwa ataswali ili isisemwe: haswali, au alifunga kwa lengo la kudumisha afya yake, basi huyo hawi katika ibada.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu akiwasifu Mitume Wake: "Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na hofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea." (Al-Anbiya: 90)

Aina za ibada:

١
Ibada tupu
٢
Mambo yanayokuwa ibada yanapoambatana na nia

1- Ibada tupu

Ni yale ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameamrisha yafanywe kwa namna maalumu, na hayawezi kuwa isipokuwa ibada tu, kama vile: Swala, Saumu, Hija, Dua, Tawaf na mengineyo kama hayo. Hairuhusiki kumfanyia yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu ibada hizi, wala kuwatafuta malipo kwazo kutoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

2- Mambo yanayokuwa Ibada yanapofungamana na nia:

Miongoni mwake ni maadili mema ambayo Mwenyezi Mungu ameyaamrisha au ameyapendekezea watu, kama vile kuwaheshimu wazazi, kuwafanyia watu wema, kuwaunga mkono wanaodhulumiwa, na ada na tabia nzuri ambazo Mwenyezi Mungu ameziamrisha kwa ujumla, na Muislamu anapata dhambi kwa kuziacha. Katika aina hii ya ibada, si lazima kumfuata Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa undani, lakini inatosha tu kutozivunja na kutumbukia katika haramu.

Ikiwa mwenye kuyafanya matendo haya ana nia njema na alikusudia kwayo kupata kumtii Mwenyezi Mungu, basi atapata thawabu. Na ikiwa yatafanywa bila ya kuukusudia uso wa Mwenyezi Mungu, basi mwenyewe hatalipwa lakini hapati dhambi. Miongoni mwa ibada hizo ni mambo ya kidunia kama vile kulala usingizi, kufanya kazi, kufanya biashara, kufanya mazoezi na mengineyo. Kwa hivyo, kila tendo lenye manufaa lililokusudiwa uso wa Mwenyezi Mungu, mtendaji wake anapata ujira. "Hakika Sisi hatupotezi ujira wa anayetenda mema." (Al-Kahf: 30)

Kuna masharti mawili yanayohitajika ili ibada iwe sahihi na ikubalike:

١
Kumkusudia Mwenyezi Mungu peke yake kwa ibada hiyo, bila ya mshirika yeyote.
٢
Kukubaliana na kufuata Sunna za Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Kwa hivyo, mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi, basi na atende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi." (Al-Kahf: 110)

Basi kauli yake: "Wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi," inaashiria kumkusudia Mwenyezi Mungu pekee katika ibada na si mwengine. Nayo kauli yake: "Vitendo vyema," inaashiria kufuata Sunna. Kwa sababu matendo mema ni yale yaliyo sahihi, na wala matendo hayawi sahihi mpaka yaafikiane na Sunna za Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimfikie. Kwa hivyo, anayemtaka Mwenyezi Mungu na nyumba ya Akhera, basi na amwabudu Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa masharti haya mawili yaliyotajwa katika Aya hii.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani