Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Kumuamini Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake

Kwa kutumwa kwa Mtume wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, milango yote ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ilifungwa isipokuwa mlango wake, na haitakubaliwa imani ya yeyote mpaka amwamini yeye na kile alichokileta kutoka kwa Mola wake Mlezi.

  • Kujua baadhi ya yale tunayopaswa kuhusiana na Mtume wetu Muhammad, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani.
  • Kujua sifa za ujumbe wa Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake).
  • Kujua tunachopaswa kufanya kuhusiana na Maswahaba wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na ahali zake.

Inatulazimu tufanye mambo kadhaa kuhusiana na Nabii wetu Muhammad, rehema na amani zimshukie, miongoni mwake ni:

1- Tunaamini kwamba Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kwamba yeye ndiye bwana wa mwanzo na wa mwisho, na ndiye mwisho wa manabii, na hakuna Nabii yeyote baada yake, na kwamba alifikisha ujumbe wa mwenyezi Mungu, na akatekeleza amana, na akawausia umma, na akapigania katika haki ya Mwenyezi Mungu.

2- Na tumsadiki katika yale anayotuambia, na tumtii katika yale aliyotuamrisha, na tujiepushe na yale aliyokataza na kuyakemea, na tumuabudu Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa Sunnah zake, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani. Na sisi tunamuiga yeye na si mwengine. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.” (Al-Ahzab: 21)

3- Na ni lazima tuyatangulize mapenzi ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, juu ya mapenzi ya baba, mtoto, na watu wote. Kama alivyosema Nabii, rehema na amani zimshukie, “Hataamini mmoja wenu mpaka niwe kipenzi zaidi kwake kuliko baba yake, mtoto wake na watu wote.” (Al-Bukhari 15, Muslim 44) Na mapenzi yake ya dhati yanakuwa kwa kufuata Sunnah zake na kuiga mwongozo wake. Na furaha ya uhakika na uwongofu kamili haupatikani isipokuwa kwa kumtii. Kama Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyosema: "Na mkimtii yeye, mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe wazi wazi." (An-Nur: 54)

4- Inatulazimu kuyakubali yale aliyokuja nayo Nabii rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kufuata Sunna zake, na tuuheshimu na kuutukuza uwongofu wake. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "La! Ninaapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayohitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wanyenyekee kabisa." (An-Nisa: 65)

5- Na inatulazimu kujihadhari na kuasi amri yake, rehema na amani ziwe juu yake. Kwa sababu kuasi amri yake ni sababu ya kuingia katika majaribio, upotofu na adhabu chungu. Mwenyezi Mungu mtukufu amesema: "Basi na watahadhari wale wanaohalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu." (An-Nuur: 63)

Sifa maalumu za ujumbe wa Muhammad

Ujumbe wa Muhammad unatofautiana na jumbe zilizopita kwa sifa maalumu mbalimbali. Na faida miongoni mwake ni:

1- Ujumbe wa Muhammad ndiyo wa mwisho wa jumbe zilizotangulia. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii." (Al-Ahzab: 40)

2- Ujumbe wa Muhammad ulizifutulia mbali sheria zilizotangulia, kwa hivyo, Mwenyezi Mungu hatakubali Dini yoyote kutoka kwa mtu yeyote - baada ya utume wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - isipokuwa kwa kumfuata Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, na wala hakuna yeyote anayeweza kufikia neema ya Peponi isipokuwa kwa njia yake, kwani yeye, rehema na amani ziwe juu yake, ndiye mtukufu zaidi ya Mitume, na umma wake ndio bora zaidi kuliko umma zote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, kamwe haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kuhasiri." (Al-Imran: 85). Na amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, “Ninaapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mkononi mwake, hakuna mtu katika umma huu, awe Myahudi au Mkristo, anayesikia kunihusu, kisha akafa na asiamini yale niliyotumwa nayo, isipokuwa atakuwa miongoni mwa watu wa Motoni.” (Muslim 153, Ahmad 8609).

3- Ujumbe wa Muhammad ni wa jumla kwa viumbe viwili vikubwa: majini na wanadamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu atujulisha kuhusu kauli ya majini: "Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu." (Al-Ahqaf: 31) Na akasema Mwenyezi Mungu: "Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui." (Saba: 28) Na akasema Nabii, rehema na amani ziwe juu yake: “Nimefadhilishwa juu ya Manabii kwa njia sita: Nilipewa usemi mfupi wenye maana pana, nikaungwa mkono kwa hofu, nikahalalishiwa ngawira, nikafanyiwa ardhi kuwa ni safi na mahali pa kuswalia, nilitumwa kwa viumbe vyote, nami ndiye niliyekuwa mwisho wa Manabii.” (Al-Bukhari 2977, Muslim 523)

Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na Ahali zake watukufu

Mwenyezi Mungu hakuwahi kumtuma Nabii yeyote isipokuwa kwamba maswahaba wake na wanafunzi wake walikuwa ni watu bora zaidi wa wafuasi wake, na kizazi chao kilikuwa kizazi kikubwa zaidi cha umma wake. Mwenyezi Mungu amewateuwa kundi la Mtume wake mbora wa viumbe vyake baada ya Mitume na Mitume, kubeba dini hii na kuifikisha kwa watu, iliyo safi na isiyo na uchafu. Kama alivyosema yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. “Walio bora katika Umma wangu ni wale niliotumwa kwao, kisha waliowafuata baada yao.” (Muslim: 2534)

Maana ya swahaba

Swahaba ni mtu aliyekutana na Nabii rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akiwa Mwislamu na akafa akiwa Mwislamu, bila ya kuritadi baada ya kufariki kwa Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, walisifiwa kwa wingi katika sehemu nyingi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake. Zikiwemo:

١
Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwasifu Maswahaba, akawa radhi nao, na akawaahidi kheri. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na waliowafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa." [At-Tawba: 100]
٢
Mtume rehema na amani za Mweneyzi Mungu zimshukie amewasifu kuwa ni watu bora kuliko mataifa yote. Hao ndio wabora wa Ummah huu. Kutoka kwa Abdullah bin Masoud, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kwamba Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: “Watu bora wa Umma wangu ni wale niliotumwa ndani yao kisha wale waliowafuata baada yao.” (Al-Bukhari 2652 na Muslim 2533)
٣
Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alibainisha wazi kuwa ujira wao na vitendo vyao vinazidishwa maradufu. Kutoka kwa Abu Said al-Khudri, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, amesema: Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: “Msiwatukane maswahaba wangu, kwani lau kuwa mmoja wenu atatoa kiasi cha Uhud cha dhahabu, basi hilo halitafikia Mudd (theluthi mbili ya kilo) ya mmoja wao wala nusu yake.” (Al-Bukhari 3673)

Mambo ya lazima kuhusiana na Maswahabah, Mwenyezi Mungu awe radhi nao

Kuna mambo kadhaa yanayomlazimu Muislamu kuhusiana na Maswahaba:

1- Kuwapenda, kuwaheshimu na kuwaombea

Mwenyezi Mungu aliwasifu Wahamiaji walioacha majumba na mali zao huko Makka na kuhamia Madina kwa sababu ya kujali dini yao na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, kisha akafuatisha hilo kwa kuwasifu Ansari, watu wa Madina, ambao waliwaunga mkono ndugu zao na wakagawana nao mali zao na vitu vyao, bali waliwatanguliza ndugu zao mbele ya nafsi zao wenyewe. Kisha akawasifu wale waliokuja baada yao mpaka Siku ya Kiyama, miongoni mwa wale wanaojua fadhila na hadhi ya Maswahaba, akawapenda, akawaombea dua, na wala hakuchukia yeyote kati yao moyoni mwake.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wapewe mafakiri Wahajiri waliotolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli. (8) Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda waliohamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyopewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa. Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walioamini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu." (Al-Hashr: 8-10).

2- Kuwaombea radhi Maswahaba wote, Mwenyezi Mungu awe radhi nao

Inamlazimu Mwislamu akimtaja yeyote miongoni mwao aseme: "Mwenyezi Mungu amuwie radhi," kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu amejulisha kwamba aliwaridhia, akawakubalia utiifu wao na vitendo vyao, na kwamba wao pia walimridhia kwa neema alizowatunuku za Dini na Dunia. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: "Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na waliowafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” (At-Tawbah: 100)

Nafasi ya Maswahaba:

1- Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu wote ni watu wa fadhila na hisani, lakini walio bora zaidi yao ni Makhalifa wanne waongofu, nao kulingana na kufuatana kwao ni: Abu Bakr Al-Siddiq, Umar bin Al-Khattab, Uthman bin Affan, na Ali bin Abi Talib, Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote.

2- Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake ni wanadamu ambao hawajahifadhika kutokana na kufanya makosa, na makosa yanatokea baina yao, lakini makosa yao ni madogo kuliko makosa ya watu wengine, na usahihi wao ni mkubwa zaidi kuliko usahihi wa watu wengine. Mwenyezi Mungu alichagua kwa kundi la Mtume wake liwe la watu bora zaidi ili wabebe dini hii: “Watu bora zaidi katika umma wangu ni kizazi nilichotumwa miongoni mwao, kisha wale waliokuja baada yao.” (Muslim: 2534)

3- Tunawashuhudia maswahaba wote watukufu kuwa ni waadilifu na wema, na tunataja fadhila zao, na hatuzami katika makosa yao au jitihada zao zilizo kinyume na haki. Kwani walikuwa na imani ya kweli na matendo mema na kumfuata Mtume kwa uzuri zaidi ya hayo (makosa yao). Kwani amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Msiwatukane maswahaba wangu, kwa sababu, lau kama mtu yeyote kati yenu atatoa dhahabu sawa na (mlima) Uhud (kwa njia ya Mwenyezi Mungu), basi haiwezi kuwa sawa na Mudd (theluthi mbili ya kilo) ya mmoja wao (yaani, maswahaba) wala nusu yake, (yaani, nusu ya Mudd).” (Al-Bukhari 3673)

Watu wa Nyumba ya Utume

Familia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ni wake zake, watoto wake, na jamaa zake, wakiwemo binamu zake: familia ya Ali, familia ya Aqiil, familia ya Jaafar, familia ya Abbas na vizazi vyao.

Na mbora wao zaidi ni wale waliokutana na Mtume wa Mwenyezi Mungu,rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama vile Ali bin Abi Talib na Fatima binti wa Mtume,rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake,pamoja na wana wao: Al-Hassan na Al-Husein, mabwana wa vijana wa watu wa Peponi, na wake za Mtume wa Mwenyezi Mungu, mama za Waumini. Kama Khadija binti Khuwaylid, na Aisha Al-Siddiqa, Mungu awe radhi nao wote.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema kuhusu wake wa Nabii rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, baada ya kuwaelekeza kwenye adabu ya hali ya juu na maadili bora: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara." (Al-Ahzab: 33)

Kuwapenda watu wa familia ya Mtume:

Muislamu anapaswa kuipenda familia ya Nabii,rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wale ambao ni waumini wanaofuata Sunnah zake, na akalifanya hili kuwa ni sehemu ya mapenzi yake kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kwa kufuata Hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu kuhusu wasia wake, kutunza familia yake, na kuwafanyia tabia njema: “Ninakukumbusheni Mwenyezi Mungu kuhusu watu wa nyumba yangu, ninakukumbusheni Mwenyezi Mungu kuhusu watu wa nyumba yangu, ninakukumbusheni Mwenyezi Mungu kuhusu watu wa nyumba yangu.” (Muslim: 2408) Kama vile baba mwenye huruma asemavyo: Mwenyezi Mungu, katika haki za watoto wangu.

Na Muislamu anapaswa kujitenga na aina mbili hizi:

١
Aina ambayo inawainua watu wa familia ya Mtume kupita kiasi na kuwapandisha kwenye kiwango cha watakatifu.
٢
Aina inayowapuuza, na kuwafanyia uadui, na kuwachukia.

Watu wa familia ya Mtume sio maasumu:

Ahlul-Bayt (Watu wa familia ya Mtume) ni kama watu wengine tu, ndani yao kuna Muislamu, kafiri, watu wema na wahalifu, tunawapenda watiifu miongoni mwao na tunataraji kwamba watalipwa mazuri, na tunawahofia waasi miongoni mwao na tunawaombea uongofu. Ubora wa watu wa familia ya Mtume haumaanishi kuwaboresha katika hali zote, na juu ya watu wote kila mmoja wao kivyake. Kwani watu hutofautiana kulingana na mazingatio mengi, na kunaweza kuwa na aliye bora na mwenye heshima zaidi katika watu wengine wasiokuwa wao.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani