Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Kuamini Mipango ya Mwenyezi Mungu

Kuamini katika mipango ya Mwenyezi Mungu ni nguzo ya sita ya imani, na imani ya mja haiwi sahihi mpaka aiamini. Katika somo hili, utajifunza uhakika wake na baadhi ya mambo muhimu kuhusiana nayo.

  • Kujua uhakika wa mipango ya Mwenyezi Mungu na umuhimu wa kuiamini.
  • Kujua matunda ya kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu.

Maana ya kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu

Ni imani thabiti kwamba heri na shari zote zinatokana na mipango ya Mwenyezi Mungu na kadari yake, na kwamba Yeye ndiye anayefanya anachotaka, hakuna kinachotokea isipokuwa kwa mapenzi yake. Na hakuna kinachokengeuka kutoka kwa mapenzi yake, na hakuna chochote ndani ya dunia ambacho kinakengeuka amri yake na hakitokei ila kwa mpango wake. Pamoja na hayo, aliamrisha na kuwakataza waja wake, na akawafanya kuwa na chaguo katika vitendo vyao, wala hakuwalazimisha kuvifanya, bali vinatokea kwa uwezo wao na mapenzi yao. Na Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wao na Muumba wa uwezo wao. Humwongoa amtakaye kwa rehema yake, na humpoteza amtakaye kwa hekima yake, wala haulizwi anachofanya na wao wanaulizwa.

Maana ya mipango ya Mwenyezi Mungu

Kadari ni mipango ya Mwenyezi Mungu ya mambo tangu zamani, na kwamba alijua kuwa yatatokea katika nyakati zinazojulikana na kwa namna maalumu, na kuyaandika kwake, na mapenzi yake, na kuyaumba kwake, na kutokea kwake kulingana na kile alichokipanga.

Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu ni mojawapo ya nguzo za imani

Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni wajibu na ni miongoni mwa nguzo za imani. Kama ilivyokuja katika jawabu la Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, pale Jibril, amani iwe juu yake, alipomuuliza juu ya imani, naye akajibu akisema: “Ni kwamba umwamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na uamini mipango ya Mwenyezi Mungu ya heri na ya shari.” (Muslim 8)

Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu kunajumuisha nini?

Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu kunajumuisha mambo manne:

1. Elimu

Ni kuamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua kila kitu kwa ujumla na kwa undani, na kwamba Yeye Mwenyezi alivijua viumbe vyake vyote kabla ya kuviumba, na alijua riziki zao, maisha yao, maneno yao na vitendo vyao, harakati zao zote na mapumziko yao, siri zao na dhahiri zao, na ni nani miongoni mwao atakuwa katika watu wa Peponi, na ni nani miongoni mwao atakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyofichikana na yanayoonekana." (Al-Hashr: 22)

2. Kuandika

Ni kuamini kwamba Yeye, Mtakatifu, aliandika yale aliyoyajua hapo awali katika Ubao Uliohifadhiwa. Ushahidi wake ni kauli yake Mola Mtukufu: “Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika Kitabu kabla hatujauumba.” (Al-Hadid: 22) Naye Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: “Mwenyezi Mungu aliandika mipangilio ya viumbe miaka elfu hamsini kabla hajaumba mbingu na ardhi.” (Muslim 2653)

3. Kutaka kwake

Ni kuamini katika kutaka kwa Mwenyezi Mungu ambako kunatekelezeka, ambako hakuna kitu kinachoweza kukuzuia,na uwezo wake ambao hakuna kitu kinachoweza kuushinda. Hivyo basi, matukio yote yanatokea kwa utashi na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Chochote anachotaka, kinafanyika, na kile ambacho hataki, hakifanyiki. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote." (At-Takwir: 29)

4. Uumbaji wake

Ni kuamini kwamba Yeye, Utukufu ni wake, ndiye Muumba wa kila kitu, na kwamba Yeye ndiye Muumba peke yake, na kwamba kila kitu kingine kimeumbwa naye, na kwamba Yeye ni Muweza juu ya kila kitu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo.” (Al-Furqan: 2).

Mwanadamu ana chaguo, uwezo na utashi:

Imani katika hatima haikanushi kuwa na utashi wa mja na uwezo wa kufanya vitendo vyake vya hiari, kwa sababu sheria na ukweli unaonyesha kwamba hii imethibitishwa kwake.

Ama sheria, Mwenyezi Mungu Mtukufu kasema kuhusiana na utashi wake: "Hiyo ndiyo Siku ya haki. Basi anayetaka na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi." (Al-Naba’: 39). Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu uwezo: "Mwenyezi Mungu haijukumishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo. Faida ya yale iliyoyachuma ni yake, na hasara ya yale iliyoyachuma ni juu yake pia." (Al-Baqara: 286). Na kadiri hapa inamaanisha majaaliwa.

Ama hali halisi ni kwamba kila mwanadamu anajua kuwa ana hiari na uwezo ambao kwa huo, yeye hufanya mambo, na kwa huo yeye huacha mambo pia, na anaweza kutofautisha kati ya yale anayoyafanya kwa hiari yake, kama vile kutembea, na yale yanayotokea bila ya kutaka kwake, kama vile kutetemeka na kuanguka kwa ghafla. Lakini utashi wa mja na uwezo wake vinatokea kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mtukufu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Kwa yule miongoni mwenu anayetaka kwenda sawa. Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote." (At-Takwir: 28-29) Kwa hivyo, akayathibitisha mapenzi ya mwanadamu, kisha akathibitisha kuwa yamo ndani ya mapenzi yake (Mwenyezi Mungu). Na kwa sababu ulimwengu wote ni wa Mwenyezi Mungu, na hakuna chochote kinachoweza kuwa katika milki yake bila kujua kwake na utashi wake.

Kutumia mipango ya Mwenyezi Mungu kama ushahidi

Uwezo na hiari ya mwanadamu ndiyo mambo yanayohusishwa na kujukumishwa kisheria, kuamrishwa na kukatazwa. Ndiyo maana mtu mwema analipwa kwa sababu alichagua njia ya uongofu, na mbaya anaadhibiwa kwa sababu alichagua njia ya upotevu. Na Mwenyezi Mungu aliyetakasika hakutujukumisha isipokuwa yale tunayoweza kustahimili, na wala hamkubalii yeyote kuacha kumuabudu kwa kuitumia mipango ya Mwenyezi Mungu kama hoja yake.

Kisha, kabla ya kuasi, mwanadamu hajui yale ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anayajua na aliyoyapanga. Mwenyezi Mungu amempa uwezo na chaguo, na akambainishia njia za mema na njia za mabaya. Kwa hivyo akiasi, basi yeye mwenyewe ndiye aliyechagua kuasi. Na akiupendelea kuliko utiifu, basi atabeba adhabu ya uasi wake.

Matunda ya kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu:

Matunda ya kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu na majaaliwa yake ni makubwa katika maisha ya Muislamu, yakiwemo:

1- Imani sahihi katika mipango ya Mwenyezi Mungu humfanya mtu kufanya matendo na kutenda visababu, na kumzuia kukaa tu bila ya kutenda.

Waumini wameamrishwa kufanya visababu huku wakimtegemea Mwenyezi Mungu, na kuamini kuwa visababu havileti matokeo isipokuwa kwa idhini yake Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba visababu, na ndiye aliyeumba matokeo. Amesema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Jitahidini kwa ajili ya yale yatakayowafaa, na tafuteni msaada kwa Mwenyezi Mungu, wala msishindwe, hata likiwasibu jambo, basi msiseme: 'Lau ningelifanya hivyo na hivyo, ingekuwa hivi na hivi.' Lakini sema: 'Mungu alipanga na anachotaka kinatendeka.' Kwani "kama" hufungulia kazi ya Shetani.” (Muslim 2664). Na wakati watu wengine walidhani kwamba hakuna haja ya kufanya matendo madamu mambo yote yalikwishapangwa na Mwenyezi Mungu, Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake akaeleza upotovu wa hilo na akasema: "Fanyeni matendo, kwani kila mtu anafanyiwa wepesi kwa alichoumbiwa." Kisha akasoma: "Ama mwenye kutoa na akamcha Mungu, Na akaliwafiki lilio jema," [Al-Layl: 6] mpaka kauli yake, "Tutamsahilishia yawe mepesi." [Al-Layl: 10]) (Al-Bukhari 4949, Muslim 2647)

2- Ni mtu kujua thamani yake mwenyewe

Asiwe na kiburi au majigambo, kwa sababu hawezi kujua ni nini alichopangiwa au mustakabali wa yatakayotokea. Kwa hivyo, mwanadamu anapaswa kutambua kutojiweza kwake na haja yake kubwa kwa Mola wake Mlezi daima. Kwa hivyo, mtu anapofikwa na heri, hufurahi na kudanganyika nayo. Na uovu na msiba unapompata, hulalamika na kuhuzunika. Na hakuna kinachoweza kumhifadhi mtu kutokana na jeuri na dhuluma pindi anapopatwa na heri au huzuni na kulalamika anapopatwa na uovu isipokuwa kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu. Na kwamba yaliyotokea, yalikuwa ndani ya mipango ya Mwenyezi Mungu na tayari alijua kwamba yatatokea.

3- Huondoa tabia mbaya ya wivu.

Muumini hawaonei wivu watu kwa yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaruzuku na kuwajaalia hayo, na anajua kwamba anapowaonea wivu wengine, anapinga mipango ya Mwenyezi Mungu na amri yake.

4- Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu huleta moyoni ujasiri katika kukabiliana na shida

Inatia nguvu azimio na kumhakikikishia mtu kwamba muda na riziki za watu tayari vimeshapangwa, na kwamba mtu hatapatwa isipokuwa na kile ambacho aliandikiwa.

5- Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu hukuza ndani ya nafsi ya muumini mambo ya uhakia ya kiimani yanayotegemewa

Wao kwa daima hutafuta msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu, humtegemea Mwenyezi Mungu pamoja na kutenda visababu. Nao pia daima wanaonyesha haja ya kubwa kwa Mola wao Mlezi, na kutafuta msaada kutoka kwake ili aendelee kuwa imara.

6- Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu humfanya mtu kuwa na utulivu katika nafsi

Muumini anajua kwamba yaliyompata, hayangemkosa, na kilichomkosa hakingempata.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani