Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Jinsi ya kufanya Umrah

Umra ni ibada tukufu ambayo kwayo Muumini huenda kwenye Nyumba tukufu, na kwa kuitekeleza anapata malipo makubwa. Katika somo hili, utajifunza kuhusu maana, fadhila na jinsi ya kufanya Umra.

  • Kujua kuhusu maana ya Umra, hukumu na fadhila zake.
  • Kujifunza kuhusu jinsi ya kufanya Umra.

Maana ya Umra

Umra ni kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa kuizunguka Al-Kaaba, kwenda mbio baina ya Safa na Marwah, kisha kunyoa au kupunguza nywele.

Hukumu ya Umra

Umra ni wajibu kwa mwenye uwezo mara moja katika maisha, na baada ya hapo inapendekezwa kuifanya na kuirudia kulingana na urahisi na uwezo wa mtu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu." (Al-Baqarah: 196)

Imesimuliwa kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kuwa alisema: Nilisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je kuna jihadi kwa wanawake?" Akasema: “Ndiyo, jihadi isiyohusisha kupigana vita; Hija na Umra.” (Ahmad 25322 na Ibn Majah 2901)

Fadhila ya Umra

١
Imesimuliwa kutoka Abu Huraira radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Umra mpaka Umra ni kafara kwa yale yaliyo baina yake. Na Hija iliyokubalika haina malipo isipokuwa Pepo.” (Bukhari 1773, Muslim 1349)
٢
Imesimuliwa kutoka kwa Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili, kuwa alisema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Fuatanisheni kati ya Hija na Umra, kwani zinaondoa umaskini na madhambi kama vile viriba vipulizavyo tanuru vinavyoondoa uchafu katika chuma.” (An-Nasa’i 2630)

Wakati wa Umra

Inajuzu kufanya Umra wakati wowote wa mwaka, na ni bora katika miezi ya Hija. Umra katika Ramadhani ina malipo maradufu na ni sawa na Hija. Imesimuliwa kutoka kwa Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: “Umra katika Ramadhani inatimiza Hija, au Hija pamoja nami." (Bukhari 1863, Muslim 1256)

Namna ya kufanya Umra

١
Kuwekea Ihram kwenye vituo vya Umrah (Miqat)
٢
Tawaf
٣
Sa'ayi
٤
Kunyoa au kupunguza nywele

Ya Kwanza: Ihram

Inajuzu kwa mwenye kutaka kuingia katika Ihram kwa ajili ya Umra avue nguo zake, aoge, ajipake manukato kichwani na ndevuni, na avae nguo za ihram.

Kisha ataswalia huko kwenye kituo (Miqat) swala ya faradhi ikiwa ni wakati wa swala ya faradhi, la sivyo ataswali rakaa mbili akitaka. Atakapomaliza kuswali, ataingia katika Ihramu na atakusudia kuingia moyoni mwake kuingia kwenye Umra akisema: "Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu huku nimenuia Umra."

-

Ya pili: Tawaf

Anapoingia ndani ya Msikiti Mtukufu, atatanguliza mguu wake wa kulia na kusema dhikri ya kuingia msikitini. Atakapoifikia Al-Kaaba, ataacha kusema Talbiyah kabla hajaanza kuzunguka. Inapendekezwa kwamba aliwache wazi bega lake la kulia, na alifunike bega lake la kushoto.

Tawaf huanzia kwenye Jiwe jeusi

Kisha ataliendea Jiwe Jeusi ili aanzie hapo kuizunguka Al-Kaba. Ataligusa jiwe hilo kwa mkono wake wa kulia na kulibusu. Na asipoweza, basi atalielekea tu lile jiwe na kuliashiria kwa mkono wake. Ataiweka Nyumba kushotoni kwake, na aizunguke raundi saba. Ataizunguka kwa haraka katika raundi tatu za kwanza.

Atakapoifika Kona ya upande wa Yemen, ataigusa bila ya kuibusu, lakini ikiwa hawezi, basi asiiashirie. Atasema tu baina ya kona hiyo na lile jiwe jeusi: “Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema na Akhera mema, na utulinde kutokana na adhabu ya Moto!"

-

Kila atakapopita hapo kwenye Jiwe Jeusi, atamtukuza Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Allahu Akbar," na atasema katika Tawafu zake zinginezo chochote anachopenda miongoni mwa dhikri na kusoma Qur-ani.

Rakaa mbili za Tawaf

Atakapomaliza kuzunguka raundi saba, atavaa shuka lake vizuri kwa kuliweka juu ya mabega yake na aweke ncha zake mbili kifuani mwake, kisha atasonga mbele hadi kwenye Maqam Ibrahim, na aswali rakaa mbili nyuma yake ikiwezekana, au katika mahali popote pale msikitini. Katika rakaa ya kwanza, baada ya Suratul Fatiha, atasoma: “Sema: Enyi makafiri” na katika rakaa ya pili atasoma: “Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee," baada ya Suratul Fatiha.

Ya tatu: Sa'ayi

Kisha atatoka kwenda Al-Mas'a, ambayo ni sehemu ya kufanyia Sa'ayi. Atakapokaribia Safaa, atasoma kauli ya Mola Mtukufu: “Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu.” Na atasema: Ninaanza kwa aliyoyaanza nayo Mwenyezi Mungu.

Kisha atapanda juu ya Safaa na kuielekea Al-Kaaba, na atanyanyua mikono yake na kumhimidi Mwenyezi Mungu na kuomba dua. Ilikuwa mojawapo ya dua za Mtume, rehema na amani ziwe juu yake ni: “Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu peke yake. Ufalme ni wake na sifa njema ni zake, na Yeye ni Muweza wa kila kitu. Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu peke yake. Aliitimiza ahadi yake, na akampa ushindi mja wake na akavishinda vikosi peke yake.” Kisha ataomba chochote anachotaka, na atarudia hivyo mara tatu.

-

Kisha atashuka kutoka Safaa na aanze kwenda Marwa. Atatembea mpaka atakapofika kwenye alama mbili za kijani ambazo sasa ni taa za kijani kwenye eneo la kufanya Sa'ayi, inapendekezwa kwa mwanamume kukimbia kwa bidii kiasi awezavyo. Mwanamke halazimiki kwenda haraka katika eneo hili.

-

Kisha ataendelea kutembea mpaka afike Marwa na kupanda juu yake. Ataelekea Kibla na anyanyue mikono yake, na aseme kile alichokisema alipokuwa juu ya Safaa, isipokuwa asisome ile aya, wala asiseme: Ninaanza kwa yale aliyoanza nayo Mwenyezi Mungu.

-

Kisha atateremka kutoka Al-Marwah na aelekee As-Safaa, mpaka atakapokuwa karibu na zile taa mbili za kijani, atakimbia. Kisha atafanya kwenye As-Safaa yale aliyoyafanya kwenye Al-Marwa. Ataendelea mpaka anamaliza mizunguko saba, raundi moja ya kwenda na raundi moja ya kurudi. Inapendeza afanye dhikri na dua nyingi kadiri awezavyo, na awe safi kutokana na hadathi kubwa na ndogo.

-

Ya nne: Kunyoa ama kupunguza nywele

Hujaji wa Umra akimaliza sa’ayi, atatoka kwenye eneo la kufanyia sa’ayi na kwenda kunyoa au kupunguza nywele, na kunyoa ni bora zaidi.

Imesimuliwa kutoka kwa Abdullah bin Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili kuwa: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: “Ewe Mwenyezi Mungu! Wasamehe wale ambao wamenyoa vichwa vyao." Watu walisema, "Pia wale ambao wamepunguza nywele zao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume akasema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Wasamehe wale ambao wamenyoa vichwa vyao." Watu wakasema, "Pia wale ambao wamepunguza nywele zao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume akasema, "Pia (wasamehe) wale ambao wamepunguza nywele zao." (Bukhari 1727, na Muslim 1301)

Na ama mwanamke yeye atakusanya nywele zake kisha azipunguze kwa inchi moja, Iwapo mtu aliye katika Ihram amekwisha yafanya ayo yaliyotajwa, basi Umra yake itakuwa imekamilika na kila alichoharamishiwa wakati wa ihram kitakuwa sasa kinaruhusika kwake.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani