Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Kutembelea Mji wa Nabii

Mji wa Mtume ndiyo sehemu bora zaidi duniani baada ya Makka. Katika somo hili, utajifunza kuhusu baadhi ya fadhila zake na adabu za kuitembelea.

  • Kujua fadhila za mji wa Mtume.
  • Kujifunza kuhusu adabu ya kutembelea mji wa Mtume.

Fadhila za Mji wa Mtume

Heshima ya mji wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, uliobarikiwa ilikuwa kubwa kwa kuhamia kwake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake,huko mpaka ukapendelewa kuliko ulimwengu wote baada ya Makka, na kuutembelea kunaruhusika wakati wote na wala hilo halihusiani na Hija. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: "Isifungwe safari (kwa ajili ya ibada) isipokuwa kwenda katika misikiti mitatu tu: Al-Masjid AI-Haram (Msikiti wa Makka), Msikiti wa Mtume,rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Msikiti wa Al-Aqsa (kule Palestina)." (Al-Bukhari 1189, na Muslim 1397). Na mji wa Madina una fadhila nyingi, ikiwemo:

1. Uwepo wa Msikiti wa Mtume ndani yake:

Jambo la kwanza alilofanya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipokuja Madina ni kujenga Msikiti wake Mtukufu, ambao ulikuja kuwa kitovu cha elimu, kulingania kwa Mwenyezi Mungu na kueneza heri baina ya watu. Msikiti huu uliobarikiwa una fadhila kubwa. Amesema Mtume, rehema za Mwenyezi Mungu na amani ziwe juu yake: “Swala ndani ya msikiti wangu huu ni bora zaidi ya swala 1000 (elfu moja) katika msikiti mwingineo, isipokuwa Al-Masjid Al-Haram (huko Makka)." (Al-Bukhari 1190, Muslim 1394)

2. Ni Haram Tukufu

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amekataza kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwamba isimwagwe damu ndani yake, wala silaha isibebwe ndani yake, wala mtu yeyote asitishwe humo, wala miti yake isikatwe, na mambo mengine yanayoingia katika katazo hili.” Amesema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Nyasi zake hazifai kung'olewa, wala mawindo yake hayafai kufukuzwa, wala kitu chake kilichodondoka, hakiokotwi, isipokuwa kwa yule atakayekitangaza, wala haukatwi mti wake isipokuwa ikiwa mtu anataka kuwalisha ngamia wake, wala haibebwi humo silaha kwa ajili ya vita." (Abu Dawud 2035, Ahmad 959)

3. Umebarikiwa katika riziki, matunda na maisha mema:

Alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Ewe Mwenyezi Mungu! Tubarikie katika matunda yetu; na tubarikie katika Madina (mji) yetu; na tubarikie katika Swaa' yetu, na tubarikie katika Mudd yetu. Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika, Ibrahim ni mja wako, na rafiki yako mwandani, na Nabii wako. Nami hakika ni mja wako na Nabii wako. Naye (Ibrahim) hakika alikuomba kwa ajili ya Makka. Nami hakika, ninakuomba kwa ajili ya Madina kwa mfano wa alivyoomba kwa ajili ya Makka, na mfano wake pamoja na hivyo." (Muslim 1373)

4.Mwenyezi Mungu ameuhifadhi mji huo kutokana na tauni na Dajjal

Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: "Katika njia zote za kuingilia Madina, kuna malaika. Tauni haiingii humo wala Ad-Dajjal." (Al-Bukhari 1880, Muslim 1379)

5. Fadhila za kukaa humo, kuishi na kufia ndani yake:

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alimuahidi mwenye kuvumilia ugumu wa Madina na ugumu wa maisha yake kwamba atamfanyia uombezi Siku ya Kiyama. Sa'ad ibn Abi Waqqas, Mwenyezi Mungu amridhie, alisema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: "Madina ni bora kwao lau wangekuwa wanajua. Hataiacha mtu kwa kuichukia isipokuwa Mwenyezi Mungu atamweka huko mtu aliye bora zaidi kumliko yeye badala yake. Na hatasubiri mtu yeyote juu ya dhiki yake (Madina) na shida zake isipokuwa ataandikiwa hivyo kama viombezi vyake, au mashahidi wake Siku ya Kiyama." (Muslim 1363)

Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: “Atakayeweza kufia Madina, basi na afie huko. Hakika mimi nitamfanyia uombezi mwenye kufia huko.” (Tirmidhi 3917, Ibn Majah 3112)

6. Ni pango la imani, na huepusha ubaya na uovu

Imani hurudi huko hata nchi ikakuwa ndogo kiasi gani, na wachafu na waovu hawana nafasi wala kuendelea kuwa ndani yake. Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie amesema: “Imani inarudi Madina kama vile nyoka anavyorudi kwenye shimo lake.” (Al-Bukhari 1876, Muslim 147) Na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, amesema: “...Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mkononi mwake, hapana hata mmoja wao anayetoka humo kwa kuikataa isipokuwa Mwenyezi Mungu hubadilisha mahali pake aliye bora kumliko yeye. Hakika Madina ni kama viriba vya kupulizia tanuri; inatoa uovu. Saa (ya Kiyama) haitasimama mpaka Madina iondoe waovu wake humo kama vile viriba vya kupulizia tanuri vinavyotoa uchafu wa chuma.” (Muslim 1381)

7. Inaondoa madhambi na uovu

Imesimuliwa kutoka kwa Zaid bin Thabit, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kuwa alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Hakika Madina ni nzuri. Na hakika Madina huondoa uchafu kama vile moto unavyoondoa uchafu katika fedha.” (Al-Bukhari 4589, Muslim 1384)

Adabu za kutembelea Mji wa Mtume

Mwenye kuizuru Madina yapaswa achunge adabu ambazo ni:

1. Kinachoruhusika kisheria ni kwamba mwenye kutaka kuja Madina, basi na akusudie kwa safari yake hiyo kuuzuru Msikiti wa Mtume, rehma na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, na si kusafiri kwa ajili ya kwenda kwenye kaburi la Mtume, rehema na amani ziwe juu yake. Hii ni kwa sababu ya kauli yake, Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Isifungwe safari (kwa ajili ya ibada) isipokuwa kwenda katika misikiti mitatu tu: Al-Masjid AI-Haram (Msikiti wa Makka), Msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Msikiti wa Al-Aqsa (kule Palestina)." (Al-Bukhari 1189, Muslim 1397)

2. Iwapo mwenye kufanya ziara atawasili msikitini, inapendekezwa kwake kutanguliza mguu wake wa kulia na kusema: “Ewe Mola nifungulie milango ya rehema yako.” (Muslim 713)

3. Ataswali rakaa mbili za kusalimia msikiti, na akiziswalia katika Rawdha tukufu, basi hilo ni bora zaidi.

4. Ni Sunna kuzuru kaburi la Mtume na maswahaba zake wawili. Kwa hivyo, atasimama kuelekea kaburi la Mtume kwa adabu, huku akishusha sauti yake chini na taadhima na aseme: “Amani iwe juu yako, ewe Mtume, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu. Ninashuhudia ya kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kwamba ulifikisha ujumbe, ulitimiza amana, uliusia umma na ulijitahidi katika haki ya Mwenyezi Mungu sawasawa. Mwenyezi Mungu akulipe kwa niaba ya umma wako malipo bora kabisa ambayo nabii anafaa kupata kutoka kwa umma wake."

Kisha atachukua hatua moja au mbili kuliani kwake na asimame mbele ya kaburi la Abu Bakr, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, na atamsalimia na atamtakia radhi. Kisha atachukua hatua moja au mbili kuliani kwake na asimame mbele ya kaburi la Umar, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, na atamsalimia na atamtakia radhi.

5. Inapendekezwa kwa mwenye kuzuru Msikiti wa Mtume kuswali sana katika Msikiti wa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ili apate malipo makubwa yaliyoahidiwa katika kauli yake Mtume,rehema na amani ziwe juu yake: “Swala moja katika Msikiti wangu huu ni bora kuliko swala elfu moja katika msikiti mwingine wowote, isipokuwa Al-Masjid-AI-Haram (Msikiti wa Makka).” (Al-Bukhari 1190, na Muslim 1394)

Ni Sunna kuzuru Msikiti wa Quba na kuswalia humo, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alieleza juu ya ubora wa jambo hilo: “Mwenye kutoka mpaka akaujia msikiti huu - Msikiti wa Quba, - na akaswalia humo, atakuwa na mfano wa Umra.” (Nasai 699)

7. Ni Sunna kuzuru makaburi ya Al-Baqi’ na makaburi ya Mashahidi wa Uhud kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa akiwatembelea na kuwaombea dua. Na mojawapo ya dua zake kwa watu wa makaburini ni: "Amani iwe juu yenu enyi watu wa nyumba hii miongoni mwa waumini na waislamu. Nasi hakika, Mwenyezi Mungu akipenda tutakuwa ni wenye kufuata. Ninamuomba Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu na kwa ajili yenu salama." (Muslim 975)

8. Ni Muislamu kufanya bidii anapokuwa katika mji huu katika kufuata amri ya Mwenyezi Mungu, kudumu kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na anafaa kujihadharisha sana kuingia katika uzushi na maasia.

9. Hafai kuikata miti yake au kuwawinda mawindo yake, kwa sababu ya yale yaliyokuja katika Hadithi zilizotoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake kama vile kauli yake: “Hakika, Ibrahim aliiharamisha Makka. Nami hakika, ninaharamisha Madina vile vilivyoko katikati ya Laabba zake mbili. Haipaswi kukatwa miti yake mikubwa yenye miiba, wala hayawindwi mawindo yake.” (Muslim 1362)

10. Ni Muislamu kuhisi anapokuwa katika mji huu kwamba yumo katika nchi ambayo nuru imetokea humo na ambayo elimu yenye manufaa imeenea sehemu zote za dunia kutoka huko, kwa hivyo na awe na hamu kubwa ya kupata elimu ya Kiislamu itakayompeleka katika Mwenyezi Mungu kwa ufahamu mzuri, hasa ikiwa anatafutia elimu hiyo katika msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Hii ni kwa mujibu wa Hadithi ya Abu Huraira, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kwamba alimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mweneyzi Mungu zimshukie akisema: “Mwenye kuingia katika msikiti wetu huu kujifunza heri au kuifundisha, atakuwa sawa na mpambanaji katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuingia humo kwa ajili ya mengine, atakuwa kama mtu anayeangalia yasiyokuwa yake.” (Ahmad 10814, na Ibn Hibban 87)

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani