Sehemu ya sasa:
Somo Hukumu na adabu za kusoma Qur-ani Tukufu
Hukumu ya kuhifadhi Qur-ani
Imesimuliwa kutoka kwa Aisha, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa: Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema, "Mfano wa yule anayeisoma Qur-ani na akaihifadhi kwa moyo, atakuwa pamoja na malaika waandishi, watukufu." (Bukhari 4937)
Hukumu ya kusoma Qur-ani Tukufu
Inapendekezwa kwa Muislamu kuisoma Qur-ani Tukufu, na azidishe kufanya hivyo namna awezavyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika Swala, na wakatoa kwa siri na kwa dhahiri katika tulivyowaruzuku, hao hutaraji biashara isiyobwaga." [Fatir 29]
Hukumu ya kunyamaza na kusikiliza Qur-ani inaposomwa
Inamlazimu Muislamu asikilize na anyamaze Qur-ani inaposomwa ikiwa ni katika swala ya lazima na katika hotuba ya Ijumaa kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na isomwapo Qur-ani, isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemewa." (Al-A'raf: 204)
Na inapendekezwa kusikiliza na kunyamaza Qur-ani inaposomwa katika hali zisizokuwa hizi. Kwa sababu ya hilo, kuna kuyafanyia adabu nzuri na kuyaheshimu maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Inamlazimu kila mmoja kuiamini Qur-ani Tukufu, na kuzifanyia kazi hukumu zake kwa kuhalalisha halali zake, kuharamisha haramu zake, kusimamia kwenye makatazo yake na kutekeleza maamrisho yake.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Wale tuliowapa Kitabu, wanakisoma kama ipasavyo kusomwa." (Al-Baqara: 121) Ibn Mas'ud na Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, walisema: Wanaihalalisha halali yake na wanaiharamisha haramu yake, na wala hawaipotoshi nje ya maana zake. (Tafsir Ibn Kathir 403/1)
Imesimuliwa kutoka kwa Abdullah bin Masud, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema: "Tulikuwa tunaposoma aya kumi za Qur-ani kutoka kwa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hatukuwa tukijifunza aya kumi zilizoshuka baada yake mpaka tujue kilichomo ndani ya zile za kwanza." (Al-Hakim 2047)
Muislamu anapaswa kuisoma Qur-ani mara kwa mara, na hafai kumaliza siku nzima bila ya kusoma kitu katika Qur-ani ili asiisahau wala asiihame. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na Mtume alikuwa akisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-ani ni kihame." [Al-Furqan: 30]
Imesimuliwa kutoka kwa Abu Musa kutoka kwa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kuwa alisema, "Endeleeni kuisoma Qur-ani; kwa kuwa, ninaapa kwa Yeye ambaye nafsi yangu iko katika mkono wake! Hiyo (Qur-ani) hutoka (husahaulika) haraka zaidi kuliko ngamia ambao wamefunguliwa kutoka kwenye kamba zao." (Bukhari 5033)
Adabu za kusoma Qur-ani Tukufu
Kusoma Qur'ani kuna adabu zinazopaswa kuzingatiwa ili usomaji huo ukubalike na mtu aweze kupata thawabu kwa hilo. Baadhi ya adabu hizo huwa kabla ya kusoma, na baadhi yake huwa wakati wa kusoma.