Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Maisha ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake

Maisha ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake yalibadilika pindi ufunuo ulipomshukia, na uso wa ardhi ukabadilika hadi Siku ya Kiyama. Katika somo hili, utajifunza kuhusu maisha ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, baada ya kupewa utume.

  • Kujua matukio muhimu zaidi katika maisha ya Nabii, kutoka alipopewa utume hadi kifo chake.

Kutumwa kwake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na ujumbe wa Uislamu

Jambo la kwanza ambalo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alianzishwa nalo la unabii ni ndoto za ukweli. Kwa hivyo akawa haoni ndoto katika usingizi wake isipokuwa inatokea kweli kama mwanga wa alfajiri, na hilo likaendelea hivyo kwa miezi sita, kisha ufunuo wa Mwenyezi Mungu ukaanza kumshukia.

Umri wa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake ulipokaribia miaka arobaini, alipenda upweke, basi akawa anakaa ndani ya pango la Hira mwezi wa Ramadhani, akiabudia humo. Aliendelea kufanya hivyo muda wa miaka mitatu mpaka ufunuo wa Mwenyezi Mungu ulipomjia alipokuwa peke yake.

Alipofikia umri wa miaka arobaini, nuru ya unabii ilimwangazia. Mwenyezi Mungu akamtukuza kwa ujumbe wake, akamtuma kwa viumbe wake, akamteua kwa mambo ya utukufu na akamfanya kuwa mwanaminifu wake kati yake na waja wake. Kwa hivyo Jibril, amani iwe juu yake, alimjia na amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akamtuma kama rehema kwa walimwengu na kwa watu wote, mbashiri na mwonyaji.

Wito wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, huko Makka

Pindi Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipopokea amri ya Mola wake Mlezi, ya kufikisha ujumbe kwa kauli yake: “Ewe uliyejigubika! Simama uonye!" [Surat Al-Muddaththir: 1-2] Akatoka mara moja akiwaita watu wamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na kuikubali dini ambayo Mwenyezi Mungu alimtuma nayo.

Wito wa kisiri

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alianza kuulingania Uislamu kwa siri ili asiwaambie kwa ghafla watu wa Makka yale yatakayowakasirisha. Kwa hivyo akaanza kuwafunza Uislamu watu ambao walikuwa karibu zaidi naye miongoni mwa wana familia na marafiki zake, na pia kila aliyeona heri ndani yake miongoni mwa wale aliowajua kwamba wanapenda haki na heri.

Waislamu wa kwanza

Wa kwanza kusilimu alikuwa mkewe, Khadija bint Khuwaylid, Mwenyezi Mungu amridhie, na sahibu yake, Abu Bakr as-Siddiq, Mwenyezi Mungu amridhie, na binamu yake, Ali bin Abi Twalib, Mwenyezi Mungu amridhie, na mtumwa aliyemkomboa, Zaid bin Haritha, Mwenyezi Mungu amridhie.

Kuilingania dini waziwazi

Kisha ikaja amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba aulinganie Uislamu waziwazi: "Basi wewe yatangaze uliyoamrishwa." [Al-Hijr: 94] Kwa hivyo, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akaudhihirisha wito wake kwa Uislamu na akaitangaza haki kama alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu alipoulingania Uislamu waziwazi, viongozi wa Maquraishi wakaukabili wito wake huo kwa kuupa mgongo na kuuzuilia kwa njia mbalimbali. Kwa kukejeli, kudharau, kudhihaki, kukadhibisha, kutowasaidia Waislamu, kuwadhoofisha katika nguvu zao za kiroho, kuyapotosha mafundisho ya dini ya Uislamu, kuzua tuhuma juu yake, kueneza propaganda za uongo na kujadiliana na Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ili aache wito huo na badala yake wampe mambo fulani ya kidunia.

Kuhamia Uhabeshi

Washirikina walipoona kuwa njia hizi hazifanyi kazi na kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, anaendelea na wito wake, wakaamua kupigana na Uislamu. Na wakaanza kumuudhi Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kuwatesa na kuwakandamiza maswahaba zake walioamini pamoja naye. Wakati maudhi haya ya washirikina yalipozidi, Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akawaamuru maswahaba wake kuhamia Uhabeshi. Basi idadi kadhaa ya Waislamu, wanaume na wanawake wakahamia huko katika mwaka wa tano wa utume.

Al-Israa na Mi'raj

Wakati Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alipokuwa katika hali hii, ambapo wito wake ulikuwa unapasua njia kati ya mafanikio na kufeli, tukio la Israa na Mi'raj likatokea. Tukio hili lilikuja ili kumuimarisha Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kumkirimu baada ya miaka mingi ya wito, na uvumilivu juu ya madhara ya washirikina na mateso yao, kukanusha kwao na ugumu wao.

Kulingania nje ya Makka

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alianza kuulingania Uislamu nje ya Makka. Kwa hivyo akaenda Taif, lakini alipowakuta wakilizuilia hilo na kulipa mgongo, akarudi Makka na kuanza kuulingania Uislamu kwa makabila na watu binafsi wakati wa msimu wa Hija.

Ahadi ya utii ya Al-'Aqaba

Katika mwaka wa kumi na moja wa utume, Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikutana katika msimu wa Hija na watu sita miongoni mwa watu wa mji wa Yathrib - ambao baadaye aliuita Madina - na akawalingania Uislamu na kuwabainishia ukweli wake, akawaita kwa Mwenyezi Mungu na akawasomea Qur-ani. Kwa hivyo wakasilimu kisha wakarudi Madina na kuwalingania watu wao mpaka Uislamu ulipoenea kati yao. Kisha ahadi ya kwanza ya Al-'Aqaba ikatimia katika msimu wa Hija wa mwaka wa kumi na mbili. Kisha ikafuatiwa na ahadi ya utii ya pili ya Al-Aqaba katika msimu wa Hija wa mwaka wa kumi na tatu, nayo ilikuwa kisiri. Ilipotimia, Mtume wa Mwenyezi Mungu akawaamrisha Waislamu waliokuwa pamoja naye kuhamia Madina, kwa hivyo wakatoka makundi makundi.

Nabii huko Madina

Baada ya Waislamu wengi kuhama kutoka Makka, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Abu Bakr, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, walitoka wakihamia Madina. Lakini walikwenda upande wa kinyume ili kuwaficha Maquraishi jambo hilo, kwa hivyo wakashuka katika pango la Thawr na kukaa humo siku tatu. Kisha wakatoka kwenda Madina kupitia njia ambayo watu walikuwa hawaifahamu, karibu na pwani ya Bahari Nyekundu. Wakati yeye na mwenzake walipofika nje kidogo ya mji wa Madina, Waislamu walimpokea katika msafara mtukufu uliojaa furaha kubwa.

Kitendo cha kwanza ambacho Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alifanya alipofika Madina ni kujenga Msikiti wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kufanya udugu kati ya Wahamiaji na Answari. Kwa hivyo akawa ameweka misingi ya jamii mpya ya Kiislamu.

Baada ya kuhamia Madina, sheria za Uislamu ziliendelea kushuka, kama vile sheria ya Zaka, kufunga saumu, Hija, Jihadi, Adhana, kuamrisha mema na kukataza maovu na sheria nyingine za Uislamu.

Vita vyake

Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwateremshia Waislamu ruhusa ya kupigana vita kwa ajili ya kuilinda dini yao na nchi yao, na ili wajitahidi kuueneza ujumbe wa milele wa Uislamu. Akasema: "Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa." [Al-Hajj: 39] Hii ndiyo aya ya kwanza iliyoteremshwa ikiruhusu kupigana vita. Mtume wa Mwenyezi Mungu alipigana vita ishirini na saba na akatuma vikosi vya kijeshi hamsini na sita.

Matukio muhimu zaidi yaliyotokea baada ya kuhamia Madina.

Yafuatayo ni maelezo mafupi ya matukio muhimu zaidi yaliyotokea baada ya Mtume kuhamia Madina.

Mwaka wa kwanza wa uhamiaji:

١
Uhamiaji.
٢
Kuujenga Msikiti wa Nabii huko Madina.
٣
Kuweka misingi ya nchi ya kwanza ya Kiislamu.

Mwaka wa pili wa uhamiaji

Wajibu wa kutoa Zaka, kufunga saumu, na vita vikuu vya Badr, ambapo kwavyo Mwenyezi Mungu aliwatukuza na kuwapa nguvu Waumini, na akawanusuru dhidi ya makafiri wa Kiqureishi.

Mwaka wa tatu wa uhamiaji

Vita vya Uhud, ambapo Waislamu walishindwa kwa sababu ya kukiuka maagizo ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, waliposhuka kutoka kwenye Mlima wa wapiga mishale ili wakusanye ngawira.

Mwaka wa nne wa uhamiaji

Vita vya Bani Nadhir, ambamo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie, aliwafurusha Mayahudi wa Bani Nadhir kutoka mji wa Madina kwa sababu walivunja agano kati yao na Waislamu.

Mwaka wa tano wa uhamiaji

Vita vya Bani Nadhir, ambamo Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani zimshukie, aliwafurusha Mayahudi wa Bani Nadhir kutoka mji wa Madina kwa sababu walivunja agano kati yao na Waislamu.

Mwaka wa sita wa uhamiaji

Upatanisho wa Hudaibiya kati ya Waislamu na Maqureishi

Mwaka wa saba wa uhamiaji

Vita vya Khaybar. Mwaka huu Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Waislamu waliingia Makka na wakafanya 'Umra ya kulipiza ile waliyokosa kuifanya.

Mwaka wa nane wa uhamiaji

Vita vikali kati ya Waislamu na Warumi, kuuteka mji wa Makka na vita vya Hunayn dhidi ya makabila ya Hawazin na Thaqif.

Mwaka wa tisa wa uhamiaji

Vita vya Tabuk, ambavyo ni vya mwisho katika vita vyake. Na mwaka huu wajumbe mbalimbali walimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na watu wakaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi. Mwaka huu uliitwa Mwaka wa wageni.

Mwaka wa kumi wa uhamiaji

Hija ya kuaga, ambapo Waislamu zaidi ya laki moja walihiji pamoja na Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Kifo chake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake

Wakati ulinganiaji wake ulipokamilika, Uislamu ukaenea katika bara Arabia, na watu wakaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi, ishara za kuenea kwake zikaonekana ulimwenguni na dini hii ikashinda dini zingine zote, Mtume wa wenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akahisi kwamba wakati wake ulikuwa umekaribia kwisha. Kwa hivyo akaanza kujiandaa kukutana na Mola wake Mlezi, na akasema maneno na kufanya vitendo vilivyoonyesha kwamba amekaribia kuondoka katika ulimwengu huu.

Katika mwaka wa kumi na moja wa Hijra, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikufa siku ya Jumatatu, tarehe kumi na mbili ya mwezi wa Rabi' al-Awwal.

Alifariki akiwa na umri wa miaka sitini na tatu, ikiwa inajumuisha miaka arobaini kabla ya utume, na miaka ishirini na mitatu kama nabii. Na katika hiyo kulikuwa na miaka kumi na tatu aliyokaa Makka na miaka kumi aliyokaa Madina.

Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikufa lakini dini yake ikabaki; na wala hakuacha heri yoyote isipokuwa aliwaonyesha umma wake, na hakuna shari yoyote isipokuwa aliwaonya dhidi yake. Na heri ambayo aliwaelekeza kwayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu na mambo yote ambayo Mwenyezi Mungu anapenda na kuyaridhia. Na shari ambayo alitahadharisha dhidi yake ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na mambo yote ambayo Mwenyezi Mungu anachukia na kuyakataa.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani