Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Ushirikiano

Katika somo hili, tutajifunza kuhusu maana ya ushirikiano na hukumu mbalimbali zinazohusiana nao katika Sheria ya Kiislamu.

  • Kujua maana ya ushirikiano katika sheria ya Kiislamu.
  • Kujua aina za ushirikiano.
  • Kujua kategoria za mikataba.
  • Kujua baadhi ya hukumu za ushirikiano.

Maana ya ushirikiano

Ni kushirikiana katika kustahiki kitu au kufanya jambo kati ya watu wawili au zaidi. Mfano wa hilo la kwanza ni watu wawili kushirikiana katika urithi au katika zawadi fulani. Na mfano wa hilo la pili ni wao kushirikiana katika kununua na kuuza.

Hukumu ya ushirikiano

Ushirikiano unaruhusiwa; kwa maana hukumu ya kimsingi katika miamala ni kwamba inaruhusika. Mwenyezi Mungu aliuruhusu ushirikiano ili iwe rahisi kwa waja wake katika kutafuta riziki. Inaruhusika kufanya ushirikiano pamoja na Muislamu na wengineo. Lakini kufanya ushirikiano na kafiri kunaruhusiwa kwa sharti kwamba asiachiwe yeye peke yake kutenda bila ya kusaidiwa na Mwislamu.

Hekima ya kuweka ushirikiano katika sheria

Mwanadamu anahitaji kukuza mali zake, na huenda asiweze kufanya hivyo peke yake, kwa sababu ya kutokuwa na uwezo na uzoefu, au kwa sababu ya ukosefu wa mtaji wa kutosha. Vile vile jamii inahitaji miradi mikubwa, na ni mara chache tu ambapo utapata mtu ambaye anaweza kufanya chochote katika miradi hiyo peke yake, kwa hivyo, kushirikiana kunarahisisha hayo yote.

Aina za ushirikiano

١
Ushirikiano katika kumiliki kitu.
٢
Ushirikiano kwa njia ya kufunga mkataba.

Ushirikiano katika kumiliki kitu ni kwa aina mbili:

١
Kushirikiana ambako mtu ana hiari
٢
Kushirikiana kwa lazima

Kushirikiana ambako mtu ana hiari

Ni kule ambako kunaundwa kwa kitendo cha washirika hao wawili. Kama vile kununua kitu kisichohama, au kinachohama, kwa hivyo wakawa wametengeneza ushirikiano baina yao katika kukimiliki.

Ushirikiano wa lazima

Ni kule kunakotokea watu wawili au zaidi bila ya wao wenyewe kuufanya, kama vile watu wawili wanaorithi kitu fulani. Wawili hao wanakuwa wametengeneza ushirikiano baina yao katika kumiliki kitu hicho.

Namna ya kuendesha mambo yanayohusiana na kitu wanachoshirikiana watu katika kukimiliki

Kila mmoja wa wenza hao wawili anakuwa kama mgeni katika fungu la mwezake. Kwa hivyo haruhusiwi kukifanyia chochote bila idhini yake. Lakini akikiendesha atakavyo, basi kuendesha kwake huko kutahusiana na fungu lake tu, isipokuwa ikiwa mwenzake huyo atamruhusu, kwa hivyo uendeshaji wake huo utathibiti katika kitu hicho chote.

Ushirikiano kwa njia ya kufunga mkataba

Huku ni kujumuika katika suala la kuendesha jambo, kama vile kujumuika katika kuuza, kununua, kukodisha, na mengineyo.

Aina za kushirikiana kwa njia ya kufunga mkataba

١
Ushirikiano wa Mudharaba
٢
Ushirikiano katika heshima
٣
Ushirikiano wa 'Inaan
٤
Ushirikiano wa kimiili
٥
Ushirikiano wa Al-Mufawadhwa

Ushirikiano wa Mudharaba

Ni wakati mmoja wa washirika anampa mwenzake mali ili aifanyie biashara kisha alipwe sehemu maalumu katika faida. Kama vile robo, au theluthi moja au mfano wa hivyo, na faida inayosalia inakuwa ni ya mmiliki wa mali hiyo. Na ikiwa mali hiyo itahasirika baada ya mwenzake huyo kuifanyia kazi, basi italipwa kutoka katika faida (ya baadaye), naye mfanyakazi huyo halazimiki kulipa kitu. Na ikiwa mali hiyo itaharibika bila ya mfanyakazi huyo kukiuka mkataba wala kuzembea, basi mmiliki huyo hapaswi kumlazimisha kuidhamini mali hiyo. Katika mkataba huu, mfanyakazi anaichukua mali hiyo kama amana, na ni wakili katika kuifanyia kazi, na anastahiki kulipwa ujira katika kazi yake hiyo, na ni mshirika katika faida.

Ushirikiano katika heshima

Ni watu wawili kushirikiana bila ya kuwepo mtaji, kwa namna kwamba wananunua kwa mkopo - kwa sababu ya heshima waliyo nayo kwa watu - kisha wauze kwa pesa taslimu. Na ile faida ambayo Mwenyezi Mungu atawapa watagawana kati yao, na hasara yoyote inayotokea, basi hiyo ni juu yao pia. Kila mmoja wao ni wakili wa mwenzake, na mdhamini wake katika kuuza, kununua na kila matendo yanayohusiana na ushirika wao huo. Uliitwa ushirikiano wa heshima kwa sababu haiuzwi kwa deni isipokuwa mwenye heshima kwa watu.

Ushirikiano wa 'Inaan

Ni watu wawili kushirikiana kwa miili yao na mali zao maalumu, hata kama wao si sawa katika hayo, ili wazifanyie kazi kwa miili yao. Ni sharti kwamba mtaji wa kila mmoja wao ujulikane, kisha inakuwa faida na hasara kulingana na masharti waliyowekeana na kuridhiana.

Ushirikiano wa kimiili

Ni watu wawili kushirikiana katika kile wanachokichuma kwa miili yao, iwe ni kushirikiana katika ufundi na taaluma, kama vile uhunzi, useremala na mfano wa hayo, au katika kazi zinazoruhusiwa. Kama vile kutema kuni na nyasi, kisha chochote anachowapa Mwenyezi Mungu, basi wanagawana kati yao kulingana na makubaliano yao na kuridhiana kwao.

Ushirikiano wa Mufawadhwa

Ni kila mmoja wa washirika kumuidhinisha mwenzake katika kuendesha mali au shughuli zinginezo zisizo za kimali katika ushirikiano wao huo. Kila mshirika anakuwa na uhuru wote wa kuendesha mambo kama vile kuuza na kununua, kuchukua na kutoa, kuweka dhamana na kuwakilisha, kufanya mkopo na kutoa sadaka, na mambo kama hayo miongoni mwa yale ambayo yanahitajika katika kuendesha biashara.

Kila mshirika anawajibika kwa kile ambacho mshirika wake anafanya, katika yale waliyofanya mkataba juu yake katika mali zao, kisha watagawana faida kati yao kulingana na masharti waliyowekeana, nayo hasara itakuwa kulingana na kiwango cha umiliki wa kila mmoja wao katika ushirikiano huo. Ushirikiano huu unaruhusika kisheria na unakusanya zile aina nne za ushirikiano zilizotangulia, ambazo zote zinaruhusika, kwa sababu ya ushirikiano ulio ndani yake, kuchuma riziki, kukidhi mahitaji ya watu, na kufikia uadilifu na masilahi.

Faida za ushirikiano

1- Ndiyo njia bora zaidi ya kukuza mali, kuwashughulisha wafanyakazi, kunufaisha taifa, kupanua riziki na kufikia uadilifu.

2- Kujitosheleza mbali na mapato ya haramu, kama vile riba, kamari, na yasiyokuwa hayo.

3- Kupanua duara la njia halali za kuchuma. Kwa maana Uislamu umemruhusu mwanadamu kuchuma peke yake au kwa kushirikiana na mtu mwingine.

Yanayobatilisha mkataba wa ushirikiano

١
Kuvunjwa ushirikiano huo na mmoja wa washirika hao wawili
٢
Kifo cha mmoja wa washirika hao
٣
Kupoteza akili kwa mmoja wa washirika hao
٤
Kupotea kwa mmoja wa washirika hao na kutokuwepo kwake kwa muda mrefu, kwa sababu hilo ni sawa na kifo

Nguzo za ushirikiano

١
Washirika hao wawili
٢
Kilichofungiwa mkataba juu yake, kama vile mali, kazi, au vyote viwili
٣
Mbinu. Nayo ni kupeana ofa na kuikubali kulingana na desturi

Masharti ya ushirikiano

١
Ujulikane mtaji na kazi ya kila mshirika.
٢
Kila mshirika apate sehemu inayojulikana inayoenea katika faida. Ima kwa asilimia, au mmoja wao apate robo au theluthi, na namna hivyo, naye huyo mwingine apate kilichosalia, na namna hivyo. Kwa hivyo si sahihi faida hiyo kutoenea, kama vile kwamba mmoja wao apate elfu moja, naye huyo mwingine apate kilichobakia.
٣
Iwe kazi ya ushirikiano huo ni katika mambo ambayo yanaruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Kwa hivyo, hairuhusiki kwa Muislamu kushiriki katika ushirikiano unaojishughulisha na shughuli zilizoharamishwa, kama vile kutengeneza sigara, madawa ya kulevya, pombe, au kufanya biashara ya vitu hivi, au nyumba za kucheza kamari, makampuni ya muziki na utengenezaji wa filamu chafu, benki za riba, na mambo mengineyo ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameharamisha.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani