Sehemu ya sasa:
Somo Haki za watoto
:idadi wanafunzi wengine walimaliza somo hili
Mwenyezi Mungu aliumba mioyo ya baba na mama kutamani kuwa na watoto, na kwamba wawe salama na wenye afya njema. Haya ndiyo yaliyokuwa matamanio ya baba yetu Adam na mkewe, amani iwe juu yao. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Yeye ndiye aliyewaumba katika nafsi moja; na katika hiyo hiyo akamfanya mwenzi wake, ili akae naye kwa utulivu. Na anapomuingilia, hubeba mzigo mwepesi, akitembea nao. Anapokuwa mja mzito, wote wawili humwomba Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wao: Kama ukitupa mwana mwema, hakika tutakuwa katika wanaoshukuru." [Al-A'araf: 189] Kutokea kwa matamanio haya ni neema ya Mwenyezi Mungu tu inayohitaji shukrani za daima kwa sababu yake.
Uislamu umelijali suala la watoto na kila kitu kinachohusiana nao. Katika yale yanayoashiria hilo, ni mazungumzo yaliyoko katika Qur-ani Tukufu juu ya watoto na neema ya watoto, baada ya kuzungumza juu ya umiliki wa Mwenyezi Mungu juu ya mbingu na ardhi. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi, Mwenye uweza." [Shuraa: 49, 50] Mwenyezi Mungu Mtukufu amehesabu uzao kwamba ni katika pambo la maisha ya dunia. Amesema Mtukufu, "Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayobakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini." [Al-Kahf: 46]
Sheria iliwapa watoto na malezi yao umuhimu mkubwa, kwa maana wao ndio nguzo ya siku zijazo, na kwa kutengenea kwao, ndio suala la kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu linaendelea duniani, na kunafikiwa kuiimarisha dunia kwa njia inayompendeza Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe." [Tahrim: 6] Ali, Mwenyezi Mungu awe radhi naye alisema, 'Inamaanisha wafundisheni elimu na watieni tabia nzuri.' Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alisema, “Mwenye kuwatunza wasichana wawili mpaka wabalehe, atakuja siku ya Kiyama, mimi na yeye (tukiwa hivi);” na akaweka pamoja vidole vyake. (Muslim 2631)
Haki za watoto juu ya wazazi
Haki hizi ni pamoja na kuwapa makazi, chakula, vinywaji, mavazi, kuwatunza kiafya, kuwapa matumizi watoto kama ilivyoagizwa na sheria. Haki hizi ni za lazima kwa baba maadamu anaweza.
Miongoni mwa haki kubwa zaidi zisizo za kimali ambazo watoto wanazo juu ya wazazi wao, ni kuwalea malezi mema yanayosimama juu ya misingi sahihi ya dini. Kwa hivyo wanafaa kufundishwa Qur-ani Tukufu, Sunna sahihi za Mtume, maisha yake na walelewe juu ya mafundisho ya Uislamu, kwa kufanya maamrisho na kuacha makatazo, na kushikamana na maadili yake mazuri. Yote hayo ni kwa sababu ya kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu, kumpenda, kumpenda Mtume wake, amani iwe juu yake, na dini yake na sheria yake.
Kuwafanyia wana huruma kuna athari kubwa katika malezi na kunafungua ufahamu wao, mradi hilo lisifikie kuwalegeza sana kwa njia ambayo inaathiri vibaya tabia zao nzuri katika maisha. Kutokuwa na rehema kwa watoto na kuwafanyia upole, na kuamiliana nao kwa ukatili mkubwa au wazazi wao kuwawia wagumu, huenda hayo yakachangia kutia giza katika nafsi zao, kuzima moto wa werevu katika akili zao, kuwafanya kutotii na kuasi, na labda wanaweza kupotea na kuharibika.
Katika haki zisizo za kimali ni kuweka mazingira ya heshima, utulivu, na upendo katika familia, ili ugomvi wa wazazi au ndugu wakubwa usitawale, ukaja kuathiri tabia za watoto na kuwafanya kuwa katika mazingira ya hofu na chuki.
Katika haki za kihisia za watoto ni wazazi kufanya bidii kuwatafutia wana wao marafiki wazuri, na kutowaruhusu kutangamana na wale walio na tabia mbaya au tabia za kulaumiwa, kwa sababu hilo linaathiri vibaya tabia zao, na wanaambukizwa tabia mbaya.
Wazazi wanapaswa kukagua hali za wana wao wa kiume na mabinti zao, kuangalia tabia na matendo yao, na kuingilia kati kwa ushauri, mwongozo na kuelekeza kila inavyohitajika kufanya hivyo. Lakini ni lazima kuwepo wastani katika hilo, na haifai kuendelea kuelekeza na kuongoza hata kwa kila dogo na kubwa. Kwa maana hilo linaweza kumfanya mtoto kuchoka kusikiliza au kufuata nasiha hizo. Kwa hivyo, baba na mama wanapaswa kuchagua nyakati na njia zinazofaa za ushauri na mwongozo.