Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Usafi wa wanawake wa Kiislamu

Katika somo hili, tunajifunza kuhusu hukumu zinazohusiana na usafi wa mwanamke wa Kiislamu.

  • Kubainisha hukumu ya mwanamke kujifunza hukumu za usafi wake mwenyewe.
  • Kufafanua janaba, hedhi na nifasi na baadhi ya hukumu zinazohusiana nayo.
  • Kubainisha hukumu za baadhi ya yale yanayotoka kwa mwanamke yasiyokuwa damu ya hedhi na nifasi.

Sheria imewawajibishia wanawake wa Kiislamu kujifunza kile wanachohitaji na kinachowahusu wao miongoni mwa hukumu za usafi, kama vile hedhi, istihadha na nifasi.

Miongoni mwa mambo ambayo wanawake wanapaswa kujua na kuyafanyia kazi ni:

١
Kuoga kutokana na janaba.
٢
Kuoga baada ya hedhi.
٣
Kuoga baada ya nifasi.

Kuoga kutokana na janaba

Janaba katika lugha ya Kiarabu ni kuwa mbali. Katika Sheria ya Kiislamu, ni hali anayokuwamo mtu baada ya kushusha manii au kujamiiana. Neno hili linaitwa hivi kwa maana mtu huyu haruhusiwi kukaribia maeneo ya swala mpaka atakapojisafisha. Kuoga kutokana na janaba ni wajibu kulingana na kauli yake Mwenyezi Mungu, "Na mkiwa na janaba, basi ogeni." [Al-Ma'idah: 6]

Kuoga baada ya hedhi

Inamlazimu mwanamke Muislamu kuoga wakati damu yake ya hedhi inapomalizika, kwa sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wasafike. Wakishasafika, basi waendeeni alivyowaamrisha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha." [Al-Baqarah: 222] Kwa hivyo kauli yake, "Wakishasafika;" yaani, kwa kuoga.

Hedhi na istihadha

Hedhi ni damu inayotoka katika tumbo la uzazi la mwanamke, na si ile anayotoka baada ya kujifungua wala inayotoka kwa sababu ya ugonjwa.

Muda wa hedhi hutofautiana kati ya wanawake, na hakuna kikomo cha muda wake wa chini zaidi kulingana na kauli sahihi zaidi ya wanazuoni, lakini wengi wao wanasema kwamba ni siku kumi na tano, na kinachozidi hapo, basi ni damu ya istihadha na si damu ya hedhi. Kutoka damu ya hedhi kwa siku sita au saba ndiyo hali ya wengi wa wanawake.

Kuoga baada ya kwisha kwa nifasi

Wanazuoni walikubaliana kwa kauli moja kwamba mwanamke anapaswa kuoga baada ya nifasi kuisha.

Maana ya nifasi

Ni damu ambayo tumbo la uzazi linatoa katika hali ya kuzaa, na kabla yake kwa siku mbili au tatu, pamoja na kuwepo kwa ishara za hilo - kama vile maumivu - na baada ya kuzaa hadi zikamilike siku arobaini. Ama muda wa nifasi, siku zake za juu zaidi ni siku arobaini, na hakuna kikomo kwa siku za chini zaidi. Kwa hivyo, pindi mwanamke anapoona amesafika, ataoga na kuswali.

Masuala yanayoambatana na hedhi na nifasi

١
Ni haramu kujamiiana naye.
٢
Ni haramu kumpa talaka.
٣
Ni haramu kwake kuswali na kufunga saumu.
٤
Ni haramu kwake kuzunguka kando ya Kaaba.
٥
Ni haramu kwake kuigusa Qur-ani.
٦
Ni haramu kwake kukaa msikitini.

Kuharamishwa kujamiiana

Ni haramu kwa mwanamume kumjamii mke wake aliye katika hedhi, kwa sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wasafike. Wakishasafika, basi waendeeni alivyowaamrisha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha." [Al-Baqarah: 222]. Pia ni haramu kumjaamii mwanamke anapokuwa katika damu ya nifasi kulingana na maafikiano ya wanazuoni.

Uharamu wa kumpa talaka

Hilo ni kwa sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu, "Ewe Nabii, mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao." [Surat Talaq 1] Maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao," ni kwamba, msimtaliki wakati yuko katika hedhi, nifasi, au katika hali ya usafi ambayo alimjamii ndani yake na bado haijakuwa wazi ikiwa ni mjamzito au la.

Uharamu wa kuswali na kufunga saumu

Hili ni kwa sababu ya kauli yake Mtume - rehema na amani ya Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, - "Kwani si kweli kwamba anapokuwa katika hedhi, haswali wala hafungi saumu? Basi huo ndio upungufu wa dini yake." (Al-Bukhari 1951)

Uharamu wa kuzunguka Ka'aba

Hili ni kwa kauli yake Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani ya Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, - akimwambia Aisha - Mwenyezi Mungu awe radhi naye - alipopata hedhi katika Hijja, "Hili kwa hakika ni jambo ambalo Mwenyezi Mungu aliandika juu ya mabinti wa Adam. Basi fanya yale anayofanya aliyeko katika Hija, isipokuwa usiizunguke Nyumba mpaka usafike." (Al-Bukhari 305, Muslim 1211)

Uharamu wa kuigusa Qur-ani

Hili ni kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Hapana akigusaye isipokuwa waliotakaswa." [Al-Waqi'a: 79] Na anaruhusiwa kuisoma Qur-ani kutoka katika yale aliyohifadhi kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi, tofauti na aliye na janaba, huyo haruhusiwi kusoma mpaka aoge. Ikiwa mwanamke aliye katika hedhi au nifasi atahitaji kudurusu aya au kuwafundisha wengine au mfano wa hayo, basi anaruhusiwa kuugusa Msahafu kwa kizuizi, kama vile glavu na vitu mfano wake.

Uharamu wa kukaa msikitini

Hili ni kwa kauli yake Mtume - rehema na amani ya Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, "Mimi hakika simhalalishii msikiti mwanamke aliye katika hedhi au aliye na janaba." (Abu Dawd 232) Na ama kupita tu ndani yake, au kuingia humo kwa ulazima, basi hilo linaruhusiwa. Imesimuliwa na Aisha - Mwenyezi Mungu amrishie - kuwa alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani ya Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - aliniambia, "Nipe mkeka wa kuswalia kutoka msikitini." Alisema: Nikasema, 'Nina hedhi.' Akasema, "Hakika hedhi yako haiko mikononi mwako." (Muslim 298)

Mambo ambayo yanapatikana kwa sababu ya hedhi:

١
Kubalehe
٢
Kuitumia katika kuhesabu muda wa eda kwa mwanamke aliyetalikiwa.

Kubalehe

Kujukumishwa na sheria kunaanza mtu anapobalehe. Hedhi ni katika ishara kubwa zaidi zinazoonyesha kwamba mtu amebalehe.

Kutumia hedhi katika kuhesabu muda wa eda kwa mwanamke aliyetalikiwa

Yaani, kipindi cha eda (kusubiri) cha mwanamke aliyetalikiwa ni kukamilika hedhi tatu kwa wale wanaopata hedhi, kwa kauli yake Yeye Mtukufu, "Na wanawake waliotalikiwa wangoje peke yao mpaka hedhi (au tahara) tatu zipite." [Al-Baqarah: 228]

Kinachoonyesha kwamba mwanamke ameshasafika kutokana na hedhi

١
Majimaji ya rangi nyeupe.
٢
Kukatika damu na kukauka kwake.

Maji ya rangi nyeupe

Ni kitu kinachofanana na uzi mweupe kinachotoka kwenye uke wa mwanamke siku ya mwisho ya hedhi yake, na kinakuwa ndiyo ishara ya kusafika kwake.

Kukatika damu na kukauka kwake

Ni mwanamke kuingiza kitambaa kwenye uke wake, na kitoke bila kuchafuliwa na damu, wekundu mzito au manjano.

Mambo ya wajibu katika kuoga

Kuoga kuna mambo mawili ya wajibu: niya na kufikisha maji kwenye nywele zote na ngozi. Ni lazima kufikisha maji katika mizizi ya kwenye hadi kwenye ngozi iliyo chini yake, sawa nywele iwe ni kidogo au nyingi.

Namna ya kuoga kwa mwanamke kutokana na hedhi na janaba

Imesimuliwa kutoka kwa Aisha - Mwenyezi Mungu amridhie - kwamba Asmaa alimuuliza Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - kuhusu kuoga kutokana na hedhi? Akasema, "Mmoja wenu achukue maji yake na mkunazi wake, kisha ajisafishe vizuri sana. Kisha amimine juu ya kichwa chake na akisugue vigumu mpaka afikishe kwenye kichwa chake chote. Kisha ajimiminie maji, kisha achukue kitambaa chenye miski na ajisafishe kwacho." Asmaa akasema, 'Atajisafishaje kwacho?' Akasema, "Subhanallah (Mwenyezi Mungu ametakasika)! Ajisafishe tu kwacho." Aisha akasema kama kwamba analificha hilo, 'kifutie athari ya damu.' Na akamuuliza kuhusu kuoga janaba? Akasema, "Achukue maji ajisafishe vizuri, kisha ajimiminie juu ya kichwa chake na asugue mpaka afike kwenye kichwa chake chote, kisha ajimiminie maji mwili mzima." Aisha akasema, 'Wanawake bora zaidi ni wanawake wa Maansari. Hawakuwa wakizuiliwa na aibu kutafuta kufahamu vyema dini yao." (Al-Bukhari 314, Muslim 332)

Kizuizi chochote kinachozuia maji kufikia sehemu yoyote ya mwili huharibu kuoga na kinafanya kuoga huko kusiwe sahihi, kama vile mwanamke kujipaka rangi ambayo inazuia maji kufikia kucha, au kuwepo kitu chochote chenye kuzuialia maji kufikia kilicho chini yake.

Rangi ya manjano na rangi ya wekundu weusi mzito

Baadhi ya vitu hutoka katika uke wa mwanamke - kabla au baada ya hedhi - na ikiwa vimeungana na hedhi, basi hivyo ni katika hedhi. Kwa hivyo lazima ajiepushe na kuswali na kila kitu kilichoharamishwa kwa sababu ya hedhi. Lakini ikiwa vitu hivyo havijashikana na hedhi, basi havina athari yoyote; kwa mujibu wa hadithi ya Umm 'Attiya - Mwenyezi Mungu amridhie, - "Hatukuwa tukihesabu rangi ya wekundu weusi mzito wala rangi ya manjano kwamba, ni kitu baada ya kusafika kutokana na hedhi." (Al-Bukhari 326, na Abu Daawuud 307 na haya ni matamshi yake).

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani