Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Unyenyekevu katika Swala

Unyenyekevu ndiyo roho ya swala, na ni katika sifa zake muhimu zaidi.

  • Kujua maana ya kunyenyekea katika swala.
  • Kujua njia zinazosaidia juu ya kunyenyekea katika swala.

Unyenyekevu katika Swala

Unyenyekevu ndio uhakika wa swala na kiini chake. Maana yake ni uwepo wa moyo wa yule anayeswali mbele ya Mwenyezi Mungu katika swala kwa unyenyekevu na kujishusha chini, huku akihisi kile anachosema miongoni mwa aya, dua na utajo.

Unyenyekevu katika swala ni katika ibada bora zaidi na mambo ya utii ya utukufu zaidi. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasisitiza katika Kitabu chake kwamba ni miongoni mwa sifa za waumini. Kama alivyosema Yeye Mukufu, "Hakika wamefanikiwa Waumini. Wale ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao." (Al-Muminun: 1-2)

Mwenye kunyenyekea katika swala ataonja raha ya ibada na imani. Ndiyo maana Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, akasema, "Na furaha ya jicho langu iliwekwa katika swala." (An-Nasai 3940). Hili linamaanisha furaha kubwa muno, utulivu na raha.

Njia zinazosaidia juu ya kunyenyekea katika swala.

1. Kujiandaa kwa ajili ya swala

Hili linakuwa kwa kwenda mapema msikitini kwa wanaume, kufanya sunna zinazotangulia swala, kuvaa vazi zuri linalofaa na kutembea hadi huko kwa heshima na utulivu.

2. Kuondoa kila chenye kushawishi na kusumbua

Kwa hivyo hafai kuswali huku mbele yake kuna vitu vya kughafilisha kama vile picha, au huku anasikia sauti zinazomsumbua. Wala asisimame kuswali huku anahitaji kwenda msalani, wala kama ana njaa au kiu mbele ya chakula na kinywaji. Na haya yote ni ili akili ya mwenye kuswali iwe safi na ajishughulishe na jambo kubwa zaidi ambalo amelielekea, ambalo ni swala yake na kunong'ona na Mola wake Mlezi.

3. Kutulizana katika swala

Na Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alikuwa akitulizana katika kurukuu kwake na kusujudu kwake mpaka kila mfupa urudi mahali pake. Alimuamuru yule ambaye hakuwa ameswali vizuri kwamba atulizane katika vitendo vyake vyote. Pia akakataza kwenda mbio wakati wa kuswali na akalifananisha hilo na kudona kwa kunguru.

Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alisema, “Mbaya wa watu wote kwa wizi ni yule anayeiba kutoka katika swala yake.” Wakasema, 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni vipi ataiba kutoka katika swala yake?' Akasema, "Hatimizi rukuu yake wala sijda yake." (Ahmad 22642) Na yule asiyetulizana katika swala yake hawezi kuwa na unyenyekevu, kwa maana kuharakisha kunaondoa unyenyekevu, na kudona kwa kunguru huondoa thawabu.

4. Kukumbuka ukuu wa yule ambaye atasimama mbele yake

Na akumbuke ukuu wa Muumba, utukufu wake, udhaifu na unyonge wake mwenyewe, na kwamba amesimama mbele ya Mola wake Mlezi, akimnong'oneza na kumuomba kwa unyenyekevu, kujishusha chini, na kuvunjika mbele yake. Na akumbuke yale ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia Waumini katika Akhera ya malipo na yale aliyowaandalia washirikina ya adhabu, na akumbuke kusimama kwake mbele ya Mwenyezi Mungu katika Akhera.

Basi anayeswali anapokumbuka kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anamsikia, atampa, na kumuitikia, ananyenyekea kwa kiasi cha anavyokumbuka, na anakuwa karibu kuingia katika wale ambao Mwenyezi Mungu amewasifu kwa kauli yake, "Na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. Wale wanaodhani kuwa watakutana na Mola wao Mlezi na kwamba watamrudia." (Al-Baqara: 45-46)

5. Kuzingatia aya zinazosomwa na ujato mwingineo katika swala, pamoja na kuyaelewa vyema

Kwa maana, Qur-ani imeteremshwa ili izingatiwe. Amesema Mtukufu, “Kitabu tulichokiteremsha kwako kilichobarikiwa, ili wapate kuzingatia Aya zake, na wenye akili wakumbuke.” (Swad 29)

Kuzingatia kunakuwaje?

Kuzingatia kwa anayeswali hakuwezekani isipokuwa kwa kuwa na elimu juu ya maana ya kile anachosoma miongoni mwa aya, utajo na dua. Hapo ndipo anaweza kutafakari juu ya hali yake na uhalisi wake kwa upande mmoja, na maana za aya hizo na utajo mbalimbali kwa upande mwingine. Ndiyo atafikia kunyenyekea na kujishusha, na kuathirika, na labda macho yake yanaweza kutokwa machozi, na hakuna aya itakayompita bila kuathiriwa nayo, kana kwamba hakusikia au kuona. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Na wale ambao, wanapokumbushwa ishara za Mola wao Mlezi, hawajifanyi viziwi nazo na vipofu." (Al-Furqan: 73)

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani