Sehemu ya sasa:
Somo Kuamini Siku ya Mwisho
Maana ya kuamini Siku ya Mwisho
Kusadiki kidhabiti kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafufua watu kutoka makaburini, kisha atawafanyia hesabu na kuwalipa kwa matendo yao, ili watu wa Peponi watue katika makazi yao, na watu wa Motoni watue katika makazi yao. Kuamini Siku ya Mwisho ni miongoni mwa nguzo za Imani, na imani haiwezi kuwa sahihi bila ya hilo.” Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Bali wema ni wa anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho." (Al-Baqarah: 177)
Siku ya Mwisho ni ipi?
Siku ya Mwisho ni siku ambayo watu watafufuliwa kwa ajili ya kufanyiwa hesabu na malipo, ili watu watuwe peponi au motoni. Na inaitwa hivyo kwa sababu hakutakuwa na siku nyingine baada ya hapo. Na siku hii ina majina mengi yaliyotajwa katika Qur-ani na Sunna, kama vile Siku ya Kiyama. Kwa sababu ya mambo makubwa yatakayojitokeza humo, kama vile watu kusimama mbele ya Mola Mlezi wa walimwengu wote. Pia inaitwa Saa, Siku ya Uamuzi, Siku ya Hukumu. Na pia ina majina mengine.
Kwa nini Qur-ani ilisisitiza kuamini Siku ya Mwisho?
Qur-ani Tukufu ilisisitiza suala la kuamini Siku ya Mwisho, na ikaitilia maanani katika kila tukio, na ikathibitisha kutokea kwake kwa njia mbalimbali za Kiarabu, na kuhusisha imani ndani yake na kumwamini Mwenyezi Mungu katika sehemu zaidi ya moja. Ili kudhihirisha umuhimu wake, ili watu wasiipuuze, na wajitayarishe kwa yaliyomo ndani yake kwa imani na matendo mema.
Kuamini Siku ya Mwisho ni matokeo ya lazima ya kumwamini Mwenyezi Mungu na uadilifu wake, Utukufu ni wake na ufafanuzi wa hilo:
Mwenyezi Mungu hakubaliani na dhuluma na hamuachi dhalimu bila ya kumuadhibu, wala mwenye kudhulumiwa bila ya kumfanyia haki, wala hamuachi mtendaji wema bila ya kumlipa thawabu, na humpa kila mwenye haki haki yake. Tunaona katika maisha ya dunia yule ambaye anaishi akiwa dhalimu na anakufa akiwa dhalimu na wala haadhibiwi. Pia tunamuona mtu ambaye anaishi akidhulumiwa na anakufa akidhulumiwa bila ya kupata haki yake. Je, hii ina maana gani wakati Mwenyezi Mungu hakubali dhuluma? Maana yake ni kwamba lazima kuwe na maisha mengine tofauti na haya tunayoishi. Lazima kuwe na wakati mwingine ambao atalipwa mtendaji wema ataadhibiwa mtendaji makosa, na kila mwenye haki atapata haki yake.
Alama za Saa
Katika kuamini Siku ya Mwisho ni kuamini ishara na alama za Saa ya mwisho, ambazo ni matukio yatakayotokea kabla ya Siku ya Kiyama, ambazo zitakuwa ishara zake. Alama hizi za Saa zimegawanywa katika sehemu mbili:
1- Alama ndogo
Hizi ni alama zitakazoitangulia Saa kwa nyakati tofautitofauti. Zikiwemo wachungaji wasio na viatu, walio uchi wanaoshindana kujenga majengo marefu. Kama ilivyoelezwa katika Hadithi ya Jibril, amani iwe juu yake: “Akasema, ‘Niambie kuhusu Saa (yaani, Kiyama)." (Mtume) Akasema, "Mwulizwaji juu yake si mjuzi zaidi ya mwulizaji (yaani, Jibril)." Kisha akamwambia, "Basi nijulishe juu ya alama zake." (Mtume) Akasema, "Ni kijakazi kumzaa bibi yake, na utakapowaona wachunga kondoo walio pekupeku, walio uchi, mafukara hali ya kuwa wanashindana katika kujenga majumba (ya kifahari)." (Muslim 8)
2- Alama kubwa
Nayo ni mambo makubwa yatakayojitokeza karibu na Saa ya Kiyama, nayo ni alama kumi. Kama ilivyoelezwa katika Hadithi kutoka kwa Hudhayfa bin Usaid, ambaye alisema: “Nabii rehema na amani za Mweneyzi Mungu ziwe juu yake, alituangalia hali ya kuwa tunakumbushana. Akasema, "Mnakumbushana nini?" Wakasema, "Tunakumbushana Saa." Akasema, "Hakika, (Saa) haitasimama mpaka muone kabla yake ishara 10 (kumi)." Kisha, akataja (1) Moshi, (2) Ad-Dajjal, (3) mnyama, (4) jua kuchomoza kutokea magharibi yake, (5) kushuka kwa Isa bin Mariam (radhi ziwe juu yake), (6) Juju-wa-maajuju, (7,8,9) mitetemeko mitatu ya ardhi: mtetemeko mmoja huko mashariki, na mtetemeko mmoja huko magharibi, na mtetemeko mmoja katika Bara Arabu, (10) na ya mwisho ya hizo (ishara) ni moto utakaotokea Yemen ambao utawafukuza watu kwenda katika mahali pao pa kukusanyika (huko Sham)." (Muslim 2901)
Je, imani katika Siku ya Mwisho inajumuisha nini?
Imani ya Muislamu katika Siku ya Mwisho inajumuisha mambo kadhaa, yakiwemo:
1. Kuamini kufufuliwa na kukusanywa:
Ni kufufuliwa wafu kutoka makaburini mwao, na roho kurejea kwenye miili yao, ili watu wasimame mbele ya Mola Mlezi wa walimwengu wote, kisha watakusanywa mahali pamoja, bila viatu na wakiwa uchi kama walivyoumbwa mara ya kwanza. Imani ya kufufuliwa inashuhudiwa na Qur-ani, Sunna, akili na umbile la asili lililo salama. Tunaamini kwa yakini kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua waliomo makaburini, na roho zao zinarudishwa kwenye miili yao, na watu watamsimamia Mola Mlezi wa walimwengu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa. Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa." (Al-Mu’minun: 15-16) Vitabu vyote vya mbinguni vimeafikiana juu ya hili, na hayo ndiyo matakwa ya hekima. Ambapo inatakiwa kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu awafanyie viumbe hawa Siku ambayo atawalipa kwa kila alichowajukumisha kupitia ndimi za Mitume wake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Je, mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?" (Al-Muuminun: 115)
2. Kuamini kwamba watu watafanyiwa hesabu na kupimiwa matendo:
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu atawafanyia hesabu viumbe kwa matendo yao waliyoyafanya katika maisha ya dunia. Kwa hivyo, atakayekuwa miongoni mwa watu wa tauhidi na mtiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hesabu yake itakuwa nyepesi. Na atakayekuwa miongoni mwa watu wa ushirikina na uasi, hesabu yake itakuwa ngumu.
Na matendo yatapimwa kwa mizani kubwa. Mazuri yatawekwa upande mmoja na mabaya upande wa pili. Kwa hivyo yule ambaye wema wake utazidi ubaya wake, basi atakuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Na yule ambaye mabaya yake yatazidi mema yake, basi atakuwa miongoni mwa watu wa Motoni, na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hesabu." (Al-Anbiya': 47).
3. Pepo na Moto:
Pepo ni makazi ya neema ya milele, iliyoandaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waumini wachamungu, wanaomtii Mwenyezi Mungu na Mitume wake, ina kila aina ya neema ya milele ambayo roho inatamani na ambayo macho yanatulia kwa sababu yake miongoni mwa kila aina ya vitu vinavyopendwa. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu, akiwataka waja wake wafanye hima katika kumtii na kuingia Peponi ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi: “Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyoandaliwa tayari kwa ajili ya wachamungu.” (Al-Imran: 133)
Ama Moto huo ni nyumba ya adhabu ya milele, Mwenyezi Mungu aliutayarisha kwa ajili ya makafiri waliomkufuru Mwenyezi Mungu na kuwaasi Mitume wake. Ndani yake kuna aina mbalimbali za adhabu, maumivu na mateso, ambazo haziingii akilini. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu, akiwaonya waja wake dhidi ya Moto aliowaandalia makafiri: "Basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, ulioandaliwa makafiri." (Al-Baqara: 24)
Ewe Mwenyezi Mungu hakika sisi tunakuomba Pepo na maneno na vitendo vinavyotukurubisha kwayo, na tunajikinga kwako kutokana na Jahannam na maneno na vitendo vinavyotukurubisha kwayo.
4. Adhabu na furaha ya kaburini
Tunaamini kuwa kifo ni hakika, Mwenyezi Mungu amesema: "Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi." (As-Sajdah: 11). Hili ni jambo ambalo linashuhudiwa na wala halina shaka yoyote, na tunaamini kwamba yeyote anayekufa au kuuawa kwa sababu yoyote ile, basi kifo chake kilitokea katika muda wake na wala muda huo haukupungaka kwa chochote.” Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Utakapofika muda wao, basi hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia." (Al-A'raf: 34) Na mwenye kufa, basi Kiyama yake huwa imefika, na anahamia nyumba ya Akhera.
Aya nyingi tukufu na hadithi tukufu zilikuja kuthibitisha adhabu ya kaburini juu ya makafiri na waasi, na neema yake kwa waumini na watu wema. Kwa hivyo, tunaiamini na wala hatujiingizi katika kueleza uhalisia wake; kwani akili haina uwezo wowote wa kujua uhalisia wake, kwa sababu hilo liko katika ulimwengu wa ghaibu kama vile Pepo na Moto, na haliko katika ulimwengu unaoshuhudiwa. Na uwezo wa akili wa kulinganisha, kutohoa mambo na kuhukumu huwa katika yale ambayo yana mfano unaojulikana katika ulimwengu wa dunia unaoonekana.
Kama vile hali za kaburini ni mambo ya ghaibu ambayo hayawezi kutambulika kwa hisia. Na lau kuwa yangetambuliwa kwa hisia, basi faida ya kuamini ghaibu ingepotea, na hekima ya kuwa wajibu ingeondolewa na watu wasingezikana. Kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Lau tu si kwamba hamtazikana, basi ningemwomba Mwenyezi Mungu kwamba awasikizishe kutoka katika adhabu kaburi." (Muslim 2868, An-Nasai 2058) Na kwa kuwa hekima hii haikutumika kwa wanyama, basi hao wanaisikia na kuielewa. Amesema Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hakika wao (wafu) huadhibiwa adhabu ambayo wanyama wote wanaisikia." (Al-Bukhari 6366 na Muslim 586)
Miongoni mwa ushahidi wa Qur-ani unaothibitisha ufufuo:
Kuna ushahidi mwingi ndani ya Qur-ani Tukufu unaothibitisha ufufuo baada ya kifo, na baadhi ya ushahidi huo ni pamoja na:
Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaumba wanadamu hapo mwanzo, na Mwenye uwezo wa kuanzisha uumbaji ana uwezo wa kuurejesha. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na Yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine." (Ar-Rum: 27) Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwajibu wale wanaokadhibisha kufufulia kwa mifupa na hali imeshaoza: "Sema: Ataihuisha huyo huyo aliyeiumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.” (Yasin: 79)
Kwamba ardhi huwa imekufa na imetulia kimya bila ya mti mbichi wowote ndani yake, kisha mvua inapoinyeshea, husisimka na kuwa kijani kibichi na kuotesha kila namna ya mimea mizuri. Kwa hivyo, mwenye uwezo wa kuihuisha baada ya kufa kwake ana uwezo wa kuwafufua wafu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa. Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi. Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyokuwa ufufuaji.” (Qaf: 9-11)
Kila mwenye akili anajua kwamba mwenye uwezo juu ya makuu na makubwa kama haya, ana nguvu zaidi na zaidi juu ya madogo yake. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi na sayari pamoja na ukubwa wake na upana wake na uumbaji wake wa ajabu. Kwa hivyo, Yeye ni Muweza zaidi wa kufufua mifupa iliyokwisha mung'unyika. Amesema Mwenyezi Mungu: "Kwani aliyeziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi." (Yasin: 81)
Matunda ya kuamini Siku ya Mwisho:
1- Kuamini Siku ya Mwisho kuna athari kubwa zaidi katika kumuongoza Muislamu, na katika nidhamu yake na kushikamana kwake na matendo mema na kumcha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kujiweka mbali na sifa na tabia mbaya. Ndiyo mara nyingi linafungamanishwa suala la kuamini Siku ya Mwisho na matendo mema. Kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika wanaoimarisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho." (At-Tawba: 18). Na kauli yake: "Na wenye kuamini Akhera wanakiamini hiki, nao wanazihifadhi Swala zao.” (Al-An’am: 92).
2- Inawaonya wale walioghafilika na wanaojishughulisha na mambo ya maisha na anasa zake, na wakaacha kushindana katika utiifu na kuchukua fursa katika wakati wao ili kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa utiifu juu ya ukweli wa maisha na ufupi wake, na kwamba Akhera ndiyo nyumba ya kuendelea na ya milele. Na Mwenyezi Mungu alipowasifu Mitume wake katika Qur-ani, na akataja vitendo vyao, aliwasifu kwa sababu iliyowasukuma kufanya vitendo hivyo. Alisema: "Hakika Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa Akhera." (Swad: 46). Yaani, sababu ya matendo hayo mema yenye ubora ni kwamba wana sifa maalumu ya kukumbuka kwao nyumba ya Akhera, kwa hivyo kukumbuka huku kukawachochea kufanya vitendo hivyo na kuwa na masimamo huo.
Na baadhi ya Waislamu walipositasita kufuata amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema akiwatanabahisha: "Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na ya Akhera ni chache.” (At-Tawba: 38) Kwa hivyo, mtu anapoiamini Siku ya Mwisho, atakuwa na yakini kwamba kila neema hapa duniani hailinganishwi na neema ya Akhera, wala haitoshani kuzamishwa kumoja katika adhabu. Na kwamba kila adhabu katika dunia - katika njia ya Mwenyezi Mungu - hailinganishwi na adhabu ya akhera, na wala haitoshani na kuzamishwa kumoja katika neema ya Akhera.
3- Kuwa na utulivu kwamba haki haitapotea. Kwa hivyo, atakayechukuliwa uzito wa chembe kwa dhuluma, ataupokea Siku ya Kiyama na hali yeye ni mhitaji zaidi juu yake. Basi vipi atahuzunika mtu anayejua kwamba haki yake itamjia bila ya kukosa katika wakati muhimu zaidi na ambao ni hatari zaidi? Na vipi atahuzunika mtu anayejua kwamba atakayehukumu baina yake na wapinzani wake ndiye hakimu bora zaidi ya mahakimu wote, aliyetakasika, Mtukufu?