Sehemu ya sasa:
Somo Uhakika wa kifo na uhai
Kifo siyo mwisho wa jambo la maisha, bali ni awamu mpya kwa mtu na mwanzo wa maisha kamili ya akhera. Kama vile Uislamu ulivyokuwa na nia ya kulinda haki mbalimbali tangu kuzaliwa, pia ulisisitiza juu ya hukumu zinazohifadhi haki za maiti na kuzingatia hali ya familia yake na jamaa zake.
Mwenyezi Mungu Mtukufu alituumba na akatufanya kuwepo katika maisha haya ya kidunia ili kutujaribu na kutupa mtihani. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu, "Ambaye ameumba mauti na uhai ili kuwajaribu ni nani miongoni mwenu ndiye mwenye vitendo vizuri zaidi." (Al-Mulk: 2) Basi atakayeamini na kumcha Mwenyezi Mungu, ataingia Peponi. Na atakayechagua upotovu na uasi, ataingia Motoni.
Uhai wa binadamu katika maisha haya hata ukawa mrefu kiasi gani, una mwisho na utaondoka. Kubakia, kudumu na uhai wa milele ni katika Akhera. Kama alivyosema Mtukufu: "Na hakika nyumba ya Akhera ndiyo maisha hasa; laiti wangelikuwa wanajua!" (Al-Anakabut: 64)
Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema akimwambia mbora wa viumbe wake, Nabii wetu Muhammad, rehema na amani Mwenyezi Mungu zimshukie, kwamba atakufa kama watu wanavyokufa, kisha kila mtu atakusanyika mbele ya Mwenyezi Mungu ili wahukumiwe. "Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa. Kisha bila ya shaka mtagombana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu Mlezi." (Az-Zumar: 30, 31)
Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, alitufananishia hali yake - na hali ya kila mwanadamu, - na dunia na ufupi wake kwa kulinganishwa na Akhera na hali ya msafiri aliyepumzika, na kulala kidogo chini ya kivuli cha mti kisha akaondoka na akauacha. Yeye, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani ziwe juu yake, alisema: “Sina uhusiano wowote na ulimwengu huu. Mimi ni kama msafiri aliyekaa katika kivuli chini ya mti, kisha akaondoka na kuuacha.” (Tirmidhi 2377, Ibn Majah 4109)
Vile vile Mwenyezi Mungu alitusimulia nasaha ya Yaaqub, amani iwe juu yake, kwa wanawe aliposema: "Hakika Mwenyezi Mungu amewateulia Dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu." (Al-Baqarah: 132)
Ikiwa mtu hajui ni lini wakati wake ambao Mwenyezi Mungu amemkusudia utafika, na mahali ambapo itakuwa, na hakuna mtu aliye na uwezo wa kuibadilisha, basi mtu mwenye akili timamu lazima atumie siku na saa zake katika mambo ya heri, kujiboresha na kufata dini. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na kila umma una muda wake. Utakapofika muda wao, basi hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia.” (Al-A’raf: 34)
Na yeyote anayekufa kwa kutolewa roho yake katika kiwiliwili chake, Kiyama yake inakuwa imesimama na ameanza safari yake katika maisha ya Akhera, ambayo (maisha hayo) ni katika elimu ya ghaibu, kwa hivyo akili ya mwanadamu haiwezi kujua jinsi yalivyo kwa undani.
Kama vile Sheria imezingatia hukumu na adabu ya mwanadamu tangu kuzaliwa kwake na kisha malezi yake, utoto wake, ujana wake na uzee wake; pia imetuwekea hukumu na adabu mbalimbali ambazo zinahifadhi haki za maiti, na kuzingatia hali ya familia na jamaa zake. Kwa hivyo, asifiwe Mwenyezi Mungu aliyekamilisha dini yake, akatimiza neema yake na akatuongoa kwenye dini hii kuu.
Mwenye kumtembelea mgonjwa anapaswa amwombee afueni na afya njema, na ya kwamba ugonjwa huu uwe ni utakaso wa madhambi na kafara kwa makosa yake. Kama alivyokuwa Mtume akimwambia mtu mgonjwa: “Laa ba'sa twahurun in shaa Allah (Hakuna ubaya. (Ugonjwa huu) ni kusafishwa (kutokana na madhambi) Mwenyezi Mungu akitaka)." (Al-Bukhari 3616)
Anapaswa kuchagua maneno na usemi ambao utamtia moyo mgonjwa ya kwamba yatamwondokea maradhi hayo na kumpigia mifano ya waliopona. Na achukue fursa hiyo kulingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kumkumbusha mgonjwa huyo kuhusu Mwenyezi Mungu na kuhusu siku ya mwisho kwa hekima na mawaidha mazuri. Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alitupigia mfano mkubwa zaidi wa jambo hilo. Imesimuliwa kutoka kwa Anas Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema: Alikuwepo kijana mmoja wa kiyahudi aliyekuwa akimtumikia Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie. Siku moja akawa mgonjwa, basi Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, akamjia ili kumtembelea. Aliketi upande wa kichwa chake, na akamwambia "Kuwa Mwisilamu." Kijana huyu akamtizama babake ambaye pia alikuwa hapo pamoja naye, na akamwambia: "Mtii baba ya Qassim, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie." Basi akasilimu. Kwa hivyo, Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, akatoka nje huku anasema: "Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu aliyemwokoa kutokana na moto." (Al-Bukhari 1356)
2.Kumwambia mtu anayekufa cha kusema
Ikiwa dalili za kifo zitaonekana kwa mgonjwa, ni vyema kumfundisha na kumtia moyo kusema neno la tauhidi na ufunguo wa Pepo ambalo ni "hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu" kwa hekima na kwa namna ifaayo. Mtume, rehema za Mwenyezi Mungu na amani ziwe juu yake, alisema: “Waambieni cha kusema watu wenu wanapokufa, kwamba: hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu.” (Muslim 916)
Nalo ndilo neno bora kabisa analofaa aseme mtu katika uhai wake na wakati wa kufa kwake. Atakayewezeshwa liwe ndilo tamko lake la mwisho, basi atakuwa amepata utukufu mkubwa zaidi. Kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Yeyote ambaye maneno yake ya mwisho yatakuwa: Hakuna mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, ataingia Peponi." (Abu Dawud 3116)
Inapendekezwa kumuelekeza mtu anayekufa kwenye Kibla. Hii ni kwa mujibu wa kauli yake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimfikie: "Nyumba Takatifu ni Kibla yenu mkiwa hai na mkiwa mmekufa." (Abu Dawud 2875) Kwa hivyo mtu anayekufa anafaa kulalishwa kwa upande wake wa kulia na aelekezwe Kibla kama anavyolalishwa kaburini.