Sehemu ya sasa:
Somo Maana ya Qur-ani Tukufu
Qur-ani Tukufu
Mwenyezi Mungu Mtukufu aliiteremsha Qur-ani kwa mbora wa viumbe vyake na wa mwisho katika Mitume wake, Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ili kuwaongoza wanadamu na kuwatoa katika viza na kuwapeleka kwenye nuru. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, "Amekwisha wajia Mtume wetu anayewafichulia mengi katika yale mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayasamehe mengi. Bila shaka imewajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinachobainisha. Mwenyezi Mungu huwaongoa kwacho njia za salama wale wenye kufuata radhi yake, na huwatoa katika viza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye njia iliyonyooka." (Al-Maida: 15-16)
Maana ya Qur-ani Tukufu
Qur-ani Tukufu ni maneno ya Mwenyezi Mungu yenye ushindi, yaliyoteremshwa juu ya Muhammad, amani iwe juu yake, ambayo kuyasoma ni ibada, yaliyoanza na Surat Al-Fatiha na kumalizia kwa Surat An-Nas.
Qur-ani Tukufu ina majina mengi yanayoashiria heshima na fadhila zake, na miongoni mwake ni:
Kuteremka kwa Qur-ani Tukufu
Qur -ani iliteremka mara ya kwanza ilipoteremka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika usiku wa cheo katika Ramadhani. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Sisi tumeiteremsha Qur-ani katika Laylatul Qadri (Usiku wa Cheo Kitukufu)." (Al-Qadr: 1) Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur-ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi." (Al-Baqarah: 185)
Aliyeteremsha Qur-ani kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni Jibril, amani iwe juu yake, ambaye ni miongoni mwa Malaika watukufu na walio karibu na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema kuhusu Qur-ani. “Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Ameuteremsha Roho muaminifu. Juu ya moyo wako, ili uwe katika waonyaji. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi." (Ash-Shu'raa 192 - 195)
Wahyi wa kwanza wa Qur-ani ulioteremka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni Aya tano za mwanzo za Suratul-Alaq, ambazo ni maneno ya Mwenyezi Mungu: "Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliyeumba. Amemuumba binadamu kwa tone la damu. Soma! Na Mola wako Mlezi ni Mkarimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu yale aliyokuwa hayajui." (Al-Alaq: 1 - 5)
Baada ya hapo, Qur-ani ilifunuliwa kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika nyakati tofauti huko Makka na Madina kwa kipindi cha miaka ishirini na tatu kulingana na matukio mbalimbali.
Imesimuliwa kutoka kwa Ibn Abbas, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao, kwamba alisema: “Qur-ani iliteremshwa yote pamoja hadi kwenye mbingu ya chini katika Usiku wa Cheo, kisha baada ya hapo ikawa inateremshwa kidogo kidogo kwa miaka ishirini.” (Al-Asmaa wa Aswifat, cha al-Bayhaqi 497)
Sura za Qur-ani Tukufu
Idadi ya sura za Qur-ani Tukufu ni 114. Ya kwanza ni Al-Fatiha na ya mwisho ni An-Nas.
Sura za Makka na za Madina
Sehemu za Qur-ani Tukufu (juzuu) ni thelathini, na vipande vyake (hizb) ni sitini.
Uandishi wa Qur-ani na kukusanywa kwake
Uandishi wa Qur-ani na ukusanyaji wake ulikuwa katika awamu tatu:
Awamu ya kwanza: Katika zama za Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake
Katika awamu hii, watu walitegemea zaidi juu ya kuhifadhi kuliko kuandika; kwa sababu ya nguvu ya kumbukumbu zao, kasi kubwa ya kuhifadhi na uchache wa wanaojua kuandika na vifaa vya kuandikia. Kwa hivyo, haikukusanywa katika Musahafu (kitabu). Lakini ilikuwa kwamba anayesikia aya, anaihifadhi au anaiandika katika kile ambacho angeweza kupata, kama vile matawi ya mitende, viraka vya ngozi, mawe, mifupa ya mabegani, na pia wasomaji walikuwa idadi kubwa.
Awamu ya pili: Katika zama za uongozi wa Abu Bakr, Mwenyezi Mungu amridhie
Katika mwaka wa kumi na mbili wa Hijra, wakati idadi kubwa ya wasomaji walipouawa huko Al-Yamama, Abu Bakr, Mwenyezi Mungu amridhie, aliamrisha kwamba Qur-ani ikusanywe pamoja ili isipotee.
Imesimuliwa kutoka kwa Zayd bin Thabit, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema: "Abu Bakr alituma niitwe baada ya mauaji makubwa ya (vita vya) Yamama (ambako idadi kubwa ya Al-Qurra waliuawa). Na tazama! 'Umar bin Khattwab alikuwepo pamoja naye. Abu Bakr akasema, "Hakika Umar amenijia na akasema, 'Hakika watu wengi waliuawa siku ya (vita vya) Yamama, nami kwa hakika ninahofia kwamba ikiwa kutakuwa na mauaji zaidi miongoni mwa Al-Qurra (wale wanaoijua Qur-ani kwa moyo) katika maeneo mengine ya vita, basi sehemu kubwa ya Qur-ani inaweza ikapotea. Nami kwa hakika ninaona kwamba uamrishe ikusanywe Qur-ani." (Mimi Abu Bakr) nilimwambia 'Umar, 'Unawezaje kufanya kitu ambacho Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hakufanya?' Umar akasema, "Wallahi! Hilo ni jambo jema." Kwa hivyo, 'Umar aliendelea kulisisitiza hilo sana akijaribu kunishawishi kulikubali pendekezo lake, mpaka Mwenyezi Mungu alipokifungua kifua changu kulikubali hilo pia, na nikawa na maoni sawa na ya Umar." Zaid alisema: Kisha Abu Bakr akaniambia, "Hakika wewe ni kijana mwenye hekima na hatukutuhumu (kwa jambo la kusema uongo au kusahau); na ulikuwa ukimwandikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, wahyi (ufunuo wa Mwenyezi Mungu). Kwa hivyo, ifuatilie Qur-ani na uikusanye (iwe katika kitabu kimoja)." Wallahi! Lau kama (Abu Bakr na 'Umar) waliniagiza kuuhamisha mlima miongoni mwa milima (kutoka mahali pake), basi hilo halingekuwa zito kwangu kuliko kile ambacho waliniagiza kufanya ambacho ni kuikusanya Qur-ani. Niliwaambia (wote wawili), "Mnawezaje kufanya jambo ambalo Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, hakufanya?" Abu Bakr akasema, "Wallahi! Ni jambo la heri." Kwa hivyo, Abu Bakr akaendelea kunijadili mpaka Mwenyezi Mungu akakifungua kifua changu kwa yale aliyokifungua kifungo cha Abu Bakr na Umar. Kwa hivyo, nikaanza kuifuatilia Qur-ani na kuikusanya kutoka kwa matawi ya mitende iliyotolewa majani, mawe, na kutoka kwenye vifua vya watu. Basi Musahafu huo ukabakia pamoja na Abu Bakr hadi Mwenyezi Mungu alipomfisha, na kisha (kikabakia) pamoja na Umar mpaka mwisho wa maisha yake, kisha kikabakia kwa Hafsa binti ya Umar, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. (Al-Bukhari 4986)
Awamu ya tatu: Zama za uongozi wa Uthman bin Affan, Mwenyezi Mungu amridhie
Eneo la nchi ya Kiislamu lilipanuka wakati wa uongozi wa Uthman bin Affan, Mwenyezi Mungu amridhie. Watu wa kila eneo wakachukua njia fulani ya kuisoma Qur-ani kutoka kwa wale waliowafundisha miongoni mwa Maswahaba. Kutokana na wingi wa njia hizi za kuisoma Qur-ani Tukufu, ilihofiwa kwamba fitina inaweza kutokea hasa kwa wale ambao hawakuisikia Qur-ani Tukufu kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Kwa hivyo Uthman akaamrisha kwamba wakusanywe watu kwenye Qur-ani moja, ili watu wasitofautiane na kuvutana juu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kutengana.
Imesimuliwa kutoka kwa Anas bin Malik, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa: Hudhaifa bin Al-Yaman alikuja kwa `Uthman wakati watu wa Sham na watu wa Iraq walikuwa wanapigana vita kuikomboa Arminia na Adhrabijan. Hudhaifa alikuwa anahofia tofauti yao (yaani watu wa Sham na Iraq) katika kusoma Qur-ani. Kwa hivyo, akamwambia 'Uthman, 'Ewe kiongozi wa Waumini! Uokoe umma huu kabla hawajatofautiana katika Kitabu (yaani Qur-ani) kama vile Mayahudi na Wakristo walivyotofautiana." Kwa hivyo, 'Uthman akatuma ujumbe kwa Hafsa akisema, "Tutumie Msahafu ili tuuandike katika nakala zingine kisha tukurudishie." Kwa hivyo, Hafsa akautuma (Msahafu huo) kwa `Uthman. Kwa hivyo, 'Uthman akawaamrisha Zaid bin Thabit, Abdullah bin Az-Zubair, Sa`id bin Al-As na Abdur-Rahman bin Harith bin Hisham, wakauandika katika nakala zingine. (Al-Bukhari 4987)
Basi Qur-ani imeendelea kusalia namna ilivyokusanywa hadi sasa, huku Waislamu wamekubaliana juu yake na kujulikana vyema baina yao.