Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Kukodisha au kuajiri

Katika somo hili tunajifunza kuhusu maana ya kukodisha na baadhi ya hukumu zake katika sheria za Kiislamu.

  • Kujua maana ya kukodisha (kuajiri), hukumu yake na hekima ya kuliweka jambo hili katika sheria.
  • Kujua nguzo za mkataba wa kukodisha (kuajiri) na masharti yake.
  • Kujua aina za ujira na mwajiriwa.
  • Kujua hali mbalimbali ambazo mkataba wa kukodisha (kuajiri) unavyomalizika.

Maana ya kukodisha (kuajiri)

Ni mkataba wa kufanya kazi fulani, au kwa ajili ya manufaa fulani yanayoruhusiwa yanayojulikana kutoka kwa kitu kinachojulikana au kisichojulikana lakini kinachoweza kuelezewa, kwa muda unaojulikana, kwa malipo yanayojulikana.

Hukumu ya kukodisha (kuajiri) katika sheria ya Kiislamu

Kukodisha (kuajiri) kunaruhusiwa, na hili linavyoashiriwa na Kitabu Kitukufu, Sunna, na makubaliano ya wanazuoni. Ni mkataba unaolazimu pande zote mbili unapokwisha hitimishwa. Nao unahitimishwa kwa kila neno lenye kuuonyesha, kama vile nimekuajiri (nimekukodisha), na maneno mengineyo ambayo yanatumika kulingana na desturi.

Miongoni mwa ushahidi wa kuruhusika kukodisha (kuajiri) ni:

Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, ''Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.'' [Al-Qasas: 26]

Na imesimuliwa kutoka kwa Aisha – Mwenyezi Mungu amuwiye radhi – kuwa alisema, "Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - na Abu Bakr walimwajiri mwanamume mmoja kutoka kwa Banu Ad-Dail: aliyekuwa mwongozaji hodari, naye alikuwa katika dini ya makafiri wa Kiquraishi. Walimpa vipando vyao viwili, na wakampa miadi ya kukutania katika pango la Thawr baada ya usiku tatu. Kwa hivyo akawajia na vipando vyao hivyo katika asubuhi ya siku ya tatu." (Al-Bukhari 2264)

Hekima ya kuruhusu kukodisha (kuajiri) kisheria

Kukodisha (kuajiri) hufanikisha manufaa mengi kwa watu katika maisha yao. Kwa maana, wanahitaji watu hodari wa kufanya ufundi na kazi, nyumba za kuishi, maduka ya kununua na kuuza, wanyama, magari, mashine, na mfano wa hivyo kwa ajili ya kubebea mizigo kuvipanda na kunufaika. Na watu wengi hawawezi kununua vitu hivi. Kwa hivyo ikawa katika kuruhusu kukodisha (kuajiri) kuna kupanua na kuwarahisishia watu, na kuwasaidia katika kukidhi mahitaji yao kwa kiasi kidogo cha mali, pamoja na kuzifaidisha pande zote mbili. Basi sifa njema zote na neema ni zake Mwenyezi Mungu.

Aina za kukodisha (kuajiri)

١
Kukodisha kitu kinachojulikana, kama vile makazi, duka, na mengineyo.
٢
Kuajiri juu ya kazi inayojulikana, kama vile kuajiri mtu kwa ajili ya kujenga nyumba, au kulima shamba, na mfano wa hayo.

Aina za watu walioajiriwa

١
Mwajiriwa wa kibinafsi
٢
Mwajiriwa wa zaidi ya mtu mmoja

Mwajiriwa wa kibinafsi

Ni yule ambaye mtu amemuajiri kwa muda maalumu ili amfanyie kazi. Huyu hafai kufanya kazi kwa asiyekuwa mwajiri wake. Na akifanya kazi kwa mtu mwingine katika muda huo, basi ujira wake utapungua kulingana na kiasi cha kazi yake. Anayo haki ya kupata malipo ikiwa atajisalimisha na akafanya kazi hiyo. Na atapata ujira kamili ikiwa mwajiri wake ataghairi kumuajiri kwake kabla ya kukamilika kwa kipindi walichoelewana, isipokuwa kama kuna udhuru kama vile ugonjwa au ulemavu, hapo atapata ujira kwa kipindi ambacho alifanya kazi tu.

Mwajiriwa wa zaidi ya mtu mmoja

Ni yule ambaye wanafaidika naye zaidi ya mtu mmoja, kama vile mhunzi, fundi bomba, mtia nguo rangi, au fundi cherehani. Ikiwa anajishughulisha kwa kujisimamia mwenyewe, na anakubali kazi kutoka kwa wanaomuomba aifanye, basi huyu hafai kuzuiwa na yule aliyemuajiri kumfanyia kazi mtu mwingine, na hastahiki ujira isipokuwa kwa kufanya kazi hiyo.

Nguzo za mkataba wa ajira

١
Wanamkataba wawili hao
٢
Njia ya kufunga mkataba
٣
Manufaa
٤
Mshahara (malipo)

Wanamkataba wawili hao

Ni wale wanamkataba wawili (muajiri na muajiriwa) miongoni mwa wale ambao wana haki ya kutoa ofa na kukubali.

Njia ya kufunga mkataba

Ni kufanya ofa na kukubali kirasmi, au njia yoyote ile inayothibitisha kuhitimisha mkataba, kisheria au kidesturi.

Manufaa

Ni kile kinachokusudiwa katika kufunga mkataba wa kukodisha (kuajiri), sawa iwe ni kwa ajili ya manufaa kutoka kwa binadamu, mnyama au kitu fulani, basi hayo ndiyo yaliyofungiwa mkataba.

Mshahara (malipo)

Ni malipo yanayotolewa kwa ajili ya kunufaika na kitu au binadamu, nayo ni sawa na bei katika mkataba wa mauzo.

Masharti yanayoufanya mkataba wa kukodisha (kuajiri) kuwa sahihi

١
Kila mmoja wa wana mkataba hao awe anaruhusiwa kisheria kufunga mkataba, kwa maana ni sharti awe ana akili timamu, si mpumbavu, na awe ana utambuzi. Kwa hivyo, mkataba wa kukodisha (kuajiri) hauwi sahihi ikiwa utafanywa na mtoto mdogo asiyekuwa na utambuzi, au mwendawazimu. Hivyo basi, mwana mkataba analazimika kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake, na pia kuwafanya wengine kumtekelezea haki yake.
٢
Kujua manufaa, kama vile kuishi ndani ya nyumba, au kumtumikia mwanadamu.
٣
Kujua ujira
٤
Manufaa yanapasa kuwa yanaruhusika, na siyo yaliyoharamishwa. Kwa hivyo, si halali kukodisha (kuajiri) kwa ajili ya kuimba, au kuifanya nyumba kuwa kanisa, au pahali kuwa pa kuuza pombe.
٥
Kujua kitu kilichokodishwa kwa kukiona kwa macho au kwa kuelezewa, na kwamba afanye mkataba juu ya manufaa yake na siyo sehemu za hicho kitu chenyewe. Pia inafaa kuwa inawezekana kukiwasilisha kitu hicho kwa wengine, na kwamba kiwe kina manufaa yanayoruhusiwa, na kwamba kiwe ni miliki ya aliyekikodisha, au kwamba awe ameidhinishwa kukikodisha.
٦
Kwamba kuwe kukodisha (kuajiri) kwa kuridhia kwa pande zote mbili.
٧
Ipatikane ofa na kukubali kati ya pande zote mbili.
٨
Kujua muda wa kukodisha (kuajiri) kama vile mwezi, au mwaka au mfano wa hivyo.
٩
Usalama wa kitu kilichokodishwa kutokana na kasoro ambayo inazuia kunufaika nacho.

Muda ambao kulipa kodi (ujira) kunakuwa ni lazima

Kodi (ujira) inakuwa lazima kuilipa kwa kusaini mkataba, na inakuwa ni lazima kuisalimisha kodi hiyo baada ya kukamilika kwa kipindi cha kukodisha.

Ikiwa watakubaliana kuilipa mapema au baadaye au kuilipa kwa awamu, basi hayo yanaruhusika. Naye mfanyakazi anastahili kupewa mshahara wake pindi anapokamilisha kazi yake vizuri.

Ikiwa kukodisha ni juu ya kitu fulani, basi kodi (ujira) utastahili baada ya kutumia kikamilifu manufaa yake. Imesimuliwa kutoka kwa Abu Huraira - Mwenyezi Mungu amuwiye radhi - kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - amesema, “Mwenyezi Mungu alisema: “Watu watatu mimi nitakuwa hasimu wao siku ya Kiyama: Mtu ambaye alitoa ahadi kwa jina langu, kisha akaivunja. Na mtu ambaye alimuuza mtu huru na akala thamani yake. Na mtu aliyeajiri mfanyakazi, na mfanyakazi huyo akamfanyia kazi yake, lakini yeye hakumlipa ujira wake." (Al-Bukhari 2227)

Hali zinazosababisha mkataba wa kukodisha (kuajiri) kuisha

١
Kuharibika kwa kitu kilichopangwa (kilichokodishwa), kama vile nyumba, gari, au mfano wake.
٢
Kukamilika kwa kipindi cha kukodisha.
٣
Iqala. Hili ni wakati mmoja wa wana mkataba amuomba mwenzake kukubali kumfutia biashara iliyokuwa imetimia, naye akakubali hilo.
٤
Kutokea kasoro katika kitu kilichokodishwa kwa sababu ya mtu mwingine asiyekuwa huyo aliyekodisha, kama vile kubomoka kwa nyumba, kuharibika kwa mashine, na mfano wa hayo.

Mkataba wa kukodisha (kuajiri) haufutilikii mbali kwa kifo cha mmoja wa wahusika, wala kwa kuuzwa kitu kilichokodishwa. Mwenye kuajiriwa kwa ajili ya kazi maalumu, kisha akafa, basi mkataba wa kuajiri huko unafutika. Na pindi kipindi cha kukodisha kinapomalizika, mpangaji anapaswa kuinua mkono wake na kumkabidhi mwenyewe kitu hicho ikiwa kinaweza kuhamishwa.

Miongoni mwa tofauti zilizoko kati ya kukodisha na kuuza

١
Kilichokodishwa katika mkataba wa kukodisha - ambacho ni manufaa - hayatumiki yakaisha mara moja. Ama katika mauzo, kilichouzwa kinatimizwa mara moja.
٢
Siyo kila kitu kinachoruhusiwa kukodisha vile vile kinaruhusiwa kuuzwa. Kwani inaruhusiwa kumuajiri mtu aliye huru, kwa sababu kilichokodishwa hapa ni kazi yake, naye mwenyewe hawezi kuuzwa kwa sababu si mali.
٣
Ingawa mkataba wa kukodisha ni kama uuzaji, unatofautishwa na uuzaji kwa kuwa huu unahusiana tu na kuuza manufaa, siyo kitu chenyewe, kama ilivyo katika uuzaji.
٤
Mkataba wa kukodisha unakubali kukamilika hapo hapo, na hata kuufungamanisha na siku zijazo. Ama uuzaji, huo hauwezekani kuwa isipokuwa unapokamilishwa papo hapo.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani