Sehemu ya sasa:
Somo Mkopo
Mwenyezi Mungu Mwenye Nguvu Mtukufu aligawanya riziki kati ya watu kwa uadilifu na hekima yake. Basi kati yao kuna matajiri na maskini, wenye uwezo na wahitaji. Na desturi ya watu ikawa kwamba baadhi yao wanakopa kutoka kwa wengine cha kuwasaidia kutimiza mahitaji yao. Na kwa sababu sheria ya Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu, Mtukufu ni kamilifu na pana, ilikuja na hukumu kadhaa zinazohusiana na mikopo. Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha mkopo katika aya ndefu zaidi katika Qur-ani Tukufu, ambayo ni aya ya 282 ya Suratul-Baqara, nayo inaitwa Aya ya deni.
Maana ya mkopo
Ni kupeana mali kwa njia ya kusaidia anayetaka kunufaika nayo, kisha arudishe badili yake.
Hukumu ya mkopo
Mkopo ni jambo linalopendekezwa, na linaloruhusiwa kwa mkopaji. Na kukopa siyo katika kuomba kunakochukiwa, kwa sababu mkopaji huchukua mali ili afaidike nayo katika kukidhi mahitaji yake, kisha arudishe badili yake.
Lakini ikiwa mkopo unaleta faida kwa mkopeshaji, basi hiyo ni riba iliyoharamishwa, kama vile kumkopesha pesa ili azirudishe na kitu zaidi juu yake. Na vile vile, ikiwa mkataba mwingine, kama vile uuzaji na mwingineo, utajumuishwa katika mkopo, basi hilo ni haramu, kwani mkopo hauruhusiwi kuunganishwa na kuuza au kununua.
Uislamu uliruhusu mkopo kwa sababu ya uzuri ulio ndani yake kwa watu, na kuwaepesishia mambo yao, na kuondoa shida zao, na kuwafariji wahitaji. Na huu ni mojawapo ya milango ambayo humleta mkopeshaji karibu na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwa kiasi hitaji lilivyokuwa kubwa, ndivyo thawabu zinazidi kuwa kubwa.
Inapendekezwa kuuandika mkopo, uwe mdogo au mkubwa, kwa kuuwekea mashahidi. Uandikwe kiasi chake, aina yake, na muda wake ili kuuhifadhi mkopo huo, na ili kumhakikishia mkopeshaji kwamba haki yake haitapotea ima kwa kifo cha mkopaji, kusahau kwake, au kukataa kwake, na mfano wa hayo. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema katika Aya ya deni, "Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi liandikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi huyo asikatae kuandika kama alivyomfunza Mwenyezi Mungu. Basi na aandike, na mwenye deni juu yake aandikishe, naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani yake." [Al-Baqarah: 282] Na akasema katika aya hiyo hiyo, "Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka." [Al-Baqarah: 282]
Masharti ya kuufanya mkopo kuwa sahihi
Ni lazima kwa mwenye kukopa mali kutoka kwa wengine aazimie kuitekeleza. Kwa hivyo ni haramu kwa mtu kuchukua mali za watu ilhali hakusudii kuwarudisha mali hizo. Na wakati wa kulipa deni unapofika, inamlazimu kulilipa. Imesimuliwa kutoka kwa Abu Huraira - Mwenyezi Mungu - kwamba Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - alisema, "Mwenye kuchukua mali za watu akitaka kuzilipa, basi Mwenyezi Mungu atamlipia hizo. Na mwenye kuzichukua huku anataka kuziharibu, basi Mwenyezi Mungu atamharibu." (Al-Bukhari 2387)
Hali mbalimbali za wadaiwa wakati wa kulipa deni
Hukumu ya kuweka mali katika benki
Hairuhusiki kumuwekea sharti mdaiwa kulipa faini ikiwa atachelewa kulipa deni kwa wakati uliowekwa, kwa sababu hiyo ni riba. Na hairuhusiki kukopa ikiwa kuna sharti hili, hata kama mkopaji anafikiria kuwa ataweza kulipa kwa wakati bila kuwepo kwa faini hii, kwa sababu huko ni kuingia katika mkataba ambao atalazimika kulipa riba.
Kufanya wema wakati wa kulipa mkopo
Kufanya wema wakati wa kulipa mkopo - kama vile akimkopesha kitu kisha yeye arudishe kilicho bora kuliko hicho, au kikubwa kuliko hicho, au kingi kuliko hicho. Hili linapendekezwa ikiwa siyo sharti. Kwa sababu hili ni katika kulipa kwa uzuri, na maadili ya ukarimu. Lakini ikiwa ni sharti, basi ni riba iliyoharamishwa.