Sehemu ya sasa:
Somo Uhakika wa Zaka na malengo yake
Zaka ndiyo nguzo ya tatu ya Uislamu. Nayo ni wajibu wa kimali ambao Mwenyezi Mungu aliufaradhisha juu ya matajiri kuwapa masikini, wahitaji na watu wengineo wanaostahili sehemu maalumu katika mali zao ili kuondoa shida zao.
1. Kupenda mali ni silika ya kibinadamu ambayo humfanya mwanadamu awe na hamu kubwa ya kuihifadhi na kuishika. Kwa hivyo, Sheria iliwajibisha kutoa Zaka ili kuisafisha nafsi kutokana na uovu wa ubahili na uchoyo, na kutibu kuipenda dunia na kushikamana na vitu vyake visivyo na thamani. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema, "Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo." (Tawba: 103)
2. Kutoa Zaka kunafanikisha suala la kushikamana na kuungana. Kwa sababu, nafsi ya mwanadamu imefanywa kuwapenda wanaoifanyia uzuri. Kwa hilo, wanajamii wa Kiislamu wataishi pamoja kwa kupendana na kushikamana, kama jengo lililokamatana, linaloimarishana lenyewe kwa lenyewe, na yatapungua matukio ya wizi, uporaji, na utapeli.
3. Inatimia maana ya uja na unyenyekevu mkamilifu, na kujisalimisha kamili kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Tajiri anapotoa Zaka ya mali yake, anakuwa anatekeleza sheria ya Mwenyezi Mungu na kutimiza amri yake. Na pia katika kuitoa kuna kumshukuru yule aliyeneemesha kwa neema hiyo, na Mwenyezi Mungu atamlipa kwa shukrani hii. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, "Mkishukuru, nitawazidishia." (Ibrahim: 7)
4. Kwa kuitoa, linafikiwa lengo la dhamana ya kijamii na uwiano wa kijamii kwa kiwango fulani kati ya vikundi vya jamii. Kwa maana, kuitoa na kuwapa wastahiki wake hakuachi rasilimali kurundikana mikononi mwa vikundi fulani tu wakawa wanaihodhi wao tu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema, "Ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu." (Al-Hashr: 7)
Uislamu umeshafafanua wale wanaostahiki Zaka. Mwislamu anaruhusiwa kukipa kikundi kimoja kati ya wapokezi wa Zaka au azipe taasisi na mashirika ya kihisani ambayo yanazigawanya kwa wapokezi wake miongoni mwa Waislamu, ingawa ni bora zaidi kuigawanya katika nchi anayoishi aliyeitoa Zaka hiyo.