Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Maana na fadhila za Hija

Hija ni kumwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kwenda Makka katika wakati maalumu kwa ajili ya kufanya ibada maalumu. Hija ni nguzo ya tano ya Uislamu. Katika somo hili, utajifunza kuhusu maana na fadhila za Hija.

  • Kujua maana ya Hija.
  • Kujua masharti yanayofanya Hija kuwa wajibu.
  • Kujua fadhila za Hija.

Maana ya Hija

Hija ni niya ya kuzuru nyumba Takatifu ya Mwenyezi Mungu katika wakati maalumu kwa ajili ya kufanya ibada maalumu. Ibada hizo ni matendo na maneno yaliyoamrishwa na Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kama vile kuvaa nguo ya Ihram, kuzunguka Nyumba Takatifu mara saba, kufanya saa'yi mara saba kati ya mlima wa Swafa na Marwa, kusimama huko Arafa, na kutupa mawe huko Minna na mengineyo. Katika Hija kuna faida kubwa kwa waja kama vile kuutangaza upweke wa Mwenyezi Mungu, msamaha mkubwa wanaoupata mahujaji, kufahamiana kati ya Waislamu, kujifunza hukumu za dini, na mengineyo.

Hukumu ya Hija

Hija ni nguzo ya tano ya Uislamu, na ni wajibu kwa kila Muislamu mara moja katika maisha yake kama ni mwenye uwezo. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezaye njia ya kwendea. Na atakayekanusha, basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu." (Al-Imran: 97)

Imesimuliwa kutoka kwa Abu Huraira, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa Mtume wa Allah, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alituhutubia na akasema: "Enyi watu! Hakika, mmefaradhishiwa kuhiji, basi hijini." Kwa hivyo, mwanamume mmoja akasema, "Kila mwaka, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akanyamaza mpaka (huyo mwanamume) akayasema mara tatu. Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akasema: "Lau ningesema 'Ndiyo' basi (hija) ingekuwa lazima (kila mwaka), na wala hamngeweza (kufanya hivyo)." (Muslim 1337)

Ni wajibu kwa Muisilamu kuharakisha kufanya Hija ikiwa amehakikishika kwamba ana uwezo.

Wakati wa Hija

Hija ina vipimo vya kinyakati na kimahali:

Vipimo ya kinyakati

Hija ina miezi yake maalumu, ambayo hairuhusiwi kuhirimia Hija isipokuwa: Shawwal, Dhul-Qa 'dah, na Dhul-Hijja. Matendo ya Hija hutekelezwa kati ya siku ya nane na ya kumi na tatu ya Dhul-Hija, ambao ni mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya Kiislamu.

Vipimo vya kimahali

Haya ni maeneo ambayo haruhusiwi hujaji au mwenye kufanya umra aliyekuja kutoka sehemu nyingine kuyaendea hadi Makka bila ya ihram. Miqat ya watu wa Madina ni Dhul-Hulayfa. Na Miqat ya watu wa Sham ni al-Juhfa. Na Miqat ya watu wa Najd ni Qarn Al-Manaazil. Na Miqat ya watu wa Yemen ni Yalamlam. Na Miqat ya watu wa Iraq ni Dhatu Irq. Miqat hizi ni kwa ajili yao, na kwa wale waliokuja ambao siyo miongoni mwa watu wao, ambao walitaka Hijja au Umrah, na maeneo haya yanajulikana kupitia watu wenye uzoefu, na ramani za kisasa.

Masharti ya wajibu ya Hija:

١
Uislamu
٢
Akili timamu
٣
Kubaleghe
٤
Kuwa huru
٥
Uwezo
٦
Uwepo wa Mahram atakayefuatana na mwanamke katika safari yake ya Hija.

Sharti la kwanza: Uislamu

Hijja ni wajibu kwa Mwisilamu, wala haipaswi kwa asiyekuwa Mwisilamu wala haiswihi kwao, kwa sababu Uisilamu ni sharti la ibada kuwa sahihi.

Sharti ya pili: Kuwa na akili timamu

Hija si wajibu kwa mwendawazimu na wala si sahihi kwake, kwani kuwa akili timamu ni sharti la kuifanya Hija kuwa faradhi na pia ni sharti la kuifanya Hija kuwa sahihi. Kama ilivyoelezwa katika Hadithi kutoka kwa Ali, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kwa amri ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ambaye alisema: "Kalamu imeinuliwa kutoka kwa watu watatu; kutoka kwa mtu aliyelala mpaka aamke, kutoka kwa mtoto mdogo mpaka abaleghe, na kutoka kwa mwendawazimu mpaka awe na akili timamu." (Abu Dawud 4403)

Sharti ya tatu: Kubaleghe

Hija si wajibu kwa mtoto mdogo, kama ilivyoelezwa katika Hadithi kutoka kwa Ali, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: “Kalamu imeinuliwa kutoka kwa watu watatu; kutoka kwa mtu aliyelala mpaka aamke, kutoka kwa mtoto mdogo mpaka abaleghe, na kutoka kwa mwendawazimu mpaka awe na akili timamu." (Abu Dawud 4403)

Ikiwa mtoto mdogo atahiji, hija yake itakuwa sahihi, ila yeye hatopata ujira wa Hija ya Uisilamu. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Anapohiji mtoto mdogo, basi hiyo kwake itakuwa Hija mpaka anapopata akili, na anapopata akili, basi atalazimika kufanya Hija nyingine."(Mustadrak Al-Hakim 1769)

Sharti la nne: Kuwa huru

Mtumwa anayemilikiwa hatakiwi kuhiji, na anapewa udhuru kwa sababu anashughulika na kumtumikia bwana wake. Kama mtumwa atahiji kwa idhini ya bwana wake, Hija yake ni sahihi, lakini haihesabiki kwamba ni Hija ya Uislamu. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu awawie radhi wote wawili, kuwa alisema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Mtumwa yeyote anayehiji kisha akaachiliwa huru, basi anahitajika kuhiji mara nyingine tena.” (As-Sunan Al-Kubra cha Al-Bayhaqi 8613)

Sharti la tano: Uwezo

Hija ni faradhi kwa mwenye uwezo, ambaye ni yule aliye sawa kimwili, mwenye uwezo wa kusafiri, na ana riziki na kipando, mambo ambayo atatumia kwa kutekeleza Hija yake. Uwezo wa mwanamke kuhiji ni kuwepo kwa mahram ambaye atafuatana naye wakati wa safari ya Hija. Hili ni kwa sababu hairuhusiki kwake kusafiri kwa ajili ya Hija au kwa ajili ya mambo mengineyo bila ya mahram.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye nyumba hiyo, kwa yule awezaye njia ya kuendea.” (Al-Imran: 97)

Na yeyote anayeweza kuhiji kwa mali zake lakini hana uwezo wa kimwili kwa sababu ya maradhi ambayo hayatibiki, au kwa sababu ya uzee, lazima ateue mtu wa kuhiji kwa niaba yake. Imesimuliwa kutoka kwa Al-Fadhl bin Abbas, kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, baba yangu alisilimu akiwa mzee na hawezi kusimama imara juu ya kipando chake cha kusafaria. Je, nihiji kwa niaba yake? Akasema: “Unaonaje kama angekuwa na deni na ukalilipa kwa niaba yake, je, hilo lingemtosheleza? Akasema: "Ndiyo." Akasema: “Basi hiji kwa niaba ya baba yako.” (Musnad Ahmad 1812)

Hali mbalimbali za uwezo wa Mwislamu katika kufanya Hija:

١
Ikiwa anaweza kufanya Hija peke yake kwa kuifikia nyumba takatifu peke yake bila ugumu wa ziada kuliko kawaida, na ana mali ya kutosha kwa ajili ya hilo, basi huyu ni wajibu kwake kufanya Hijja mwenyewe.
٢
Ikiwa ana uwezo wa kuhiji kupitia kwa mtu mwingine, na siyo yeye mwenyewe kwa sababu ya maradhi au uzee, lakini akapata mtu wa kuhiji kwa niaba yake, na pia anaweza kumtolea mali yake ili aende kuhiji kwa niaba yake, basi huyu analazimika kutoa mali hizo ampe mtu wa kuhiji kwa niaba yake.
٣
Ikiwa hawezi kuhiji peke yake wala kwa kupitia kwa mtu mwengine, basi huyu si wajibu kwake kuhiji maadamu hawezi. Kama vile mtu ambaye hana mali inayozidi mahitaji yake na matumizi ya familia yake ambayo inatosha kuhiji kwayo. Huyu haimlazimu kukusanya mali ili aweze kuhiji, lakini pindi atakapokuwa na uwezo, Hija inakuwa ni wajibu kwake.

Sharti la sita: Uwepo wa mahram atakayeandamana na mwanamke katika safari

Ili Hija iwe wajibu kwa mwanamke, ni sharti kuwepo kwa mahram wake. Hija si wajibu kwa mwanamke isipokuwa ikiwa atakuwa pamoja na yeyote miongoni mwa maharimu wake katika Hija. Nao ni: mume wake au mtu ambaye kamwe hawezi kuoana naye, kama vile baba, babu, mwanawe, mwana wa mwanawe, kaka yake na watoto wao, ami yake na mjomba wake.

Iwapo mwanamke atahiji bila ya mahram kwa njia ambayo ni salama kwake, basi Hija yake ni sahihi na anapata malipo yake, lakini atapata dhambi kwa sababu ya kusafiri bila mahram.

Fadhila za Hija

Kuna fadhila na mambo mengi mazuri yaliyotajwa katika Hija, ikiwa ni pamoja na:

1- Ni mojawapo ya matendo bora zaidi

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipoulizwa: "Ni tendo gani bora zaidi?" Akasema: "Kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Ikasemwa: Kisha lipi? Akasema: "Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu." Ikasemwa: Halafu ipi? Akasema: " Hija yenye kukubaliwa." (Al-Bukhari 1519 Muslim 83)

2- Msimu mkubwa wa kupata msamaha

Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake: “Mwenye kuhiji kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wala asiseme maneno machafu, wala asifanye vitendo vichafu, atarejea kama siku aliyozaliwa na mama yake.” (Al-Bukhari 1521, Muslim 1350) Ikimaanisha kwamba atarudi bila dhambi kana kwamba alikuwa ametoka tu kuzaliwa.

3-Fursa nzuri ya kujikomboa kutokana na moto

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimfikie alisema: “Hakuna siku ambayo Mwenyezi Mungu humkomboa mja kutokana na moto kuliko siku ya Arafa.” (Muslim 1348)

4- Malipo yake ni Pepo

Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Hija iliyokubaliwa haina malipo mengine isipokuwa Pepo.” (Al-Bukhari 1773, Muslim 1349) Fadhila hizi na nyinginezo ni kwa wale waliosadikisha na kusahihisha makusudio yao, na wakafuata sawasawa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani