Endelea kujifunza

Umeshaingia
Jisajili sasa kwenye jukwaa la Taa ili uanze kujifunza, na fuatialia maendeleo yako, na kukusanya pointi, na uingie kwenye mashindano.Baada ya kujisajili, utapata cheti cha kielektroniki katika mada ambazo utajifunza.

Sehemu ya sasa:

Somo Namna ya kufanya Hija

Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie aliwafundisha watu wake jinsi ya kutekeleza ibada ya Hija. Katika somo hili, utajifunza jinsi ya kutekeleza Hija kulingana na Sunna.

  • Kujifunza kuhusu aina tatu za ibada za Hija.
  • Kujifunza kuhusu namna ya kufanya Hija.

Aina za Hija

Kuna aina tatu za Hija: Tamattu, Qiran na Ifrad. Mwenye kuhiji anaweza kuchagua moja ya aina hizi tatu kwa ajili ya Hija yake.

Imepokelewa kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema: Tulitoka pamoja na mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na akasema: "Yeyote miongoni mwenu anayetaka kutia ihram ya Hija na Umrah, basi na afanye hivyo, na yeyote anayetaka kutia ihram ya Hija pekee, basi na afanye hivyo, na yeyote anayetaka kutia ihram ya Umrah pekee, basi na afanye hivyo." (Muslim 1211)

Tamattu

Jinsi ya kufanya Tamattu ni kuhirimia Umrah katika miezi ya Hija, na atasema anapohirimia Umrah: "Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu na ninanuia kufanya Umrah, ya kujistarehesha mpaka Hija." Kisha baada ya kufanya Umrah na kuimaliza, atatoka katika ihram, na kisha atajistarehesha kwa kufanya yale yaliyokuwa amekatazwa alipokuwa katika ihram. Kisha atahirimia kufanya Hija katika siku ya nane ya Dhul-Hijja huko Makka. Ataendelea kuwa katika ihram mpaka atakapoitupia mawe Jamrah al-Aqaba katika siku ya Iddi. Itamlazimu kuchinja mnyama kwa sababu ya kujistarehesha alikojistarehesha. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndiyo akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. (Al-Baqarah: 196)

Qiran

Namna ya kufanya Qiran ni kwamba ataingia katika ihramu kwa ajili ya Umra na Hija, na aseme anapoingia katika ihram: "Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu ninanuia kufanya Umra na Hija." Kisha anapofika Makka atafanya Tawaf ya kufika. Itamlazimu kufanya saa'yi moja, ambayo ima aitangulize na aifanye baada ya Tawaf ya kufika au aicheleweshe na aifanye baada ya Tawaf ya Hija. Asinyoe kichwa chake au kutoka nje ya ihramu, bali atabakia katika ihramu mpaka atakapoirushia vijiwe Jamarat al-Aqaba siku ya kuchinja, kisha anyoe nywele. Mtu aliyefanya Hija ya Qiran analazimika kuchinja mnyama atakayepatikana kwa wepesi.

Ifrad

Namna ya kufanya Hija ya Ifrad ni kwamba ataingia katika hali ya ihram kwa ajili ya Hija peke yake, atasema anapoingia kwenye ihram: "Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu kwa kunuia kufanya Hija," kisha anapofika Makka atafanya Tawaf ya kufika. Atalazimika kufanya saa'yi mara moja; ima aitangulize aifanye baada ya Tawaf ya kufika au ataichelewesha aifanye baada ya Tawaf ya Hija. Hatanyoa kichwa chake wala kutoka katika Ihram. Bali atabakia katika ihramu yake mpaka atakapoirushia vijiwe Jamaratul Aqaba siku ya kuchinja, na hapo ataruhusiwa kunyoa. Mtu anayefanya Hija ya Ifrad halazimiki kuchinja mnyama wa dhabihu.

Namna ya kufanya Hija

Muislamu lazima awe na bidii ya kuhiji kwa namna ambayo Mtume wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alivyofanya Hija na namna alivyowaamrisha maswahaba zake watukufu, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Imesimuliwa kutoka kwa Jabir, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kuwa alisema: Nilimuona Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, akirusha vijiwe akiwa juu ya kipando chake siku ya kuchinja na akisema: “Chukueni (kwangu) ibada zenu za Hija. Kwani mimi hakika sijui kama nitahiji baada ya Hija yangu hii.” (Muslim 1297)

1- Ihram

Hujaji anapofika kwenye stesheni za Hija na akataka kuingia katika ihram kwa ajili ya Hija, anapaswa kuvua nguo zake za kawaida, aoge, ajipake manukato kichwani na ndevuni, avae nguo za ihramu, kisha aswali swala ya faradhi ikiwa ni wakati wa swala hiyo ya faradhi, la sivyo ataswali rakaa mbili akitaka, akikusudia kwayo kuswali sunna ya baada ya wudhu.

Anapomaliza kuswali, ataingia katika ihram na kunuia Hija anayotaka, kimoyomoyo, kisha:

١
Ikiwa anafanya Hija ya Tamattu, atasema: "Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu kwa kunuia Umra ya kujistarehesha mpaka Hija."
٢
Ikiwa anataka kufanya Hija pekee, atasema: Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu kwa kunuia Hija."
٣
Ikiwa anafanya Qiran, atasema: Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu kwa kunuia Hija na Umra."

Kisha atasema kwa wingi Talbiya, akisema: “Labbayka Aluhumma llabayk, labbayka laa sharika laka labbayk, innal hamda wa nna'amata laka wal mulk, laa sharika laka (Nimekuitika ewe Mwenyezi Mungu nimekuitika, nimekuitika huna mshirika nimekuitika. Hakika sifa njema, na neema na Ufalme, ni vyako, huna mshirika wako).” Mwanaume atanyanyua sauti yake kwa hili, naye mwanamke atayasema kwa kiasi wanavyoweza kusikia wanawake walio karibu naye, siyo wanaume. Hujaji anapaswa kujiepusha na makatazo ya ihram anapokuwa bado katika hali ya Ihram.

2. Kuingia Makka

Inapendekezwa kwa mwenye kuhiji kuoga ili aingie Makka, kisha ataenda kwenye Msikiti Mtukufu kufanya Umra ikiwa yuko katika Tamattu. Inapendekezwa kwa hujaji anayefanya Hija ya Qiran na Ifrad kufanya Tawaf ya kuingia Makka.

3- Tawaf (kuzunguka kaaba)

Anapoingia ndani ya Msikiti Mtukufu atatanguliza mguu wake wa kulia na aseme dhikri ya kuingia msikitini. Anapoifikia Al-Kaaba, ataacha kusema Talbiyah kabla hajaanza kuizunguka. Inapendekezwa kwa wanaume kulifunika bega lake la kushoto na kuliwacha wazi bega lake la kulia.

Kisha ataliendea Jiwe Jeusi ili aanze kuzunguka Al-Kaba. Ataligusa jiwe hilo kwa mkono wake wa kulia na alibusu, lakini asipoweza, basi atalielekea na kuliashiria kwa mkono wake. Ataiweka nyumba kushotoni kwake, kisha ataizunguka mara saba. Mwanamume atazunguka kwa haraka katika mara tatu za kwanza.

Akifika kwenye kona ya upande wa Yemen, ataigusa bila ya kuibusu. Lakini asipoweza, basi asiiashirie. Na aseme baina ya kona hiyo ya upande wa Yemen na lile jiwe jeusi: “Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto!"

Kila wakati atakapopita jiwe jeusi, atasema: Mwenyezi Mungu ni mkubwa, kisha atasema katika tawafu zake zinginezo kile anachopenda miongoni mwa dhikri, na kusoma Qur-ani.

Atakapomaliza kuzunguka raundi saba, atavaa ihram yake vizuri, kisha ataelekea nyuma ya Maqam Ibrahim, ikiwezekana, au popote pale msikitini humo, na aswali rakaa mbili, akisema “Sema: Enyi makafiri,” katika rakaa ya kwanza baada ya Suratul-Fatiha. Na aseme: “Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee,” baada ya Suratul-Fatiha katika rakaa ya pili.

4 - Sa'ayi

Kisha atatoka kwenda Al-Mas'a, na atapokaribia Safaa, atasoma kauli ya Mola Mtukufu: “Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu," kisha atasema: "Ninaanza kwa aliyoanza nayo Mwenyezi Mungu."

Ataanza kufanya Sa'ayi kutokea Safaa kwa kupanda juu ya mlima huo na aelekee Kaaba. Kisha atanyanyua mikono yake amhimidi Mwenyezi Mungu na aombe. Na ilikuwa katika dua za Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake ni: Laa Ilaha Ila llahu wahdahu laa shariika lahu, lahul mulk wa lahul hamdu wahuwa alaa kulli shay-in qadir. Laa ilaaha ila llahu wahdahu, anjaza wa'adahu, wa naswara abdahu, wahazamal ahzaaba wahda (Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke yake, wala hana mshirika, ni wake Ufalme, na ni zake sifa njema, naye juu ya kila kitu ni Muweza. Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu hali ya kuwa peke yake, alitekeleza ahadi yake, na akamnusuru mja wake, na akavishinda vikosi peke yake)." Kisha ataomba anayotaka, na atarudia hivyo mara tatu.

Kisha atashuka kutoka Safaa na aanze kwenda Marwa. Kwa hivyo atatembea mpaka atakapofika kwenye alama mbili zile ambazo ni taa za kijani kwenye sehemu ya kufanyia Sa'ayi, hapo inapendekezwa kwa mwanamume kukimbia kwa bidii kiasi awezavyo. Lakini mwanamke halazimishwi kukimbia hivyo, bali atatembea katika Sa'ayi yote.

Kisha ataendelea kutembea mpaka afike Marwa na kupanda juu yake. Ataelekea Kibla, ainue juu mikono yake, na aseme kile alichokisema akiwa Safaa, isipokuwa asisome aya, wala asiseme: Ninaanza kwa yale aliyoanza nayo Mwenyezi Mungu.

Kisha anateremka kutoka Al-Marwa na kuelekea Al-Safaa, mpaka atakapokuwa karibu na taa hizo za kijani, atakimbia, na kisha akishafika Safaa atafanya yale aliyoyafanya akiwa Al-Marwa. Atarudia hayo yote mpaka amalize mizunguko saba, raundi moja ya kwenda ikiwa ni mara moja ya kurudi ikiwa ni mara ya pili. Inapendeza afanye dhikri na dua nyingi kiasi awezavyo, na awe msafi kutokana na hadathi kubwa na ndogo.

Mwenye kufanya Hija ya Tamattu analazimika afanye sa'ayi mbili, sa'ayi ya Umra na sa'ayi ya Hija. Ama kuhusu mwenye kufanya Al-qiran na Al-ifrad, kila mmoja wao analazimika afanye sa'ayi moja tu, ambayo ima ataifanya baada ya tawaf ya kufika Makka, au ataifanya baada ya tawaf ya Hija.

5- Kunyoa au kupunguza nywele

Mwenye kuhiji akimaliza sa'ayi, atanyoa kichwa chake au apunguze nywele zake, ikiwa anafanya Tamattu. Kunyoa kwa mwanamume ndiyo bora, lakini akipunguza na kuacha kunyoa, basi hakuna ubaya. Mwanamke atakusanya nywele zake kisha azipunguze kwa inchi moja. Mwenye kufanya Hija ya Tamattu akifanya hivyo, basi Umra yake inakuwa imekamilika, na kila alichoharamishiwa wakati wa Ihram kinajuzu kwake. Ama ikiwa ni mwenye kufanya Hija ya Ifrad au ya Qiran, yeye hafai kunyoa au kupunguza baada ya sa'ayi, lakini atabakia katika ihram yake.

6- Siku ya Tarwiya

Siku ya Tarwiyah ni siku ya nane ya Dhul-Hijja, nayo ndiyo siku ambayo Hija huanza. Mwenye kufanya Tamattu', ataingia katika ihramu ya Hija asubuhi ya siku hiyo katika sehemu aliyopo. Ataoga, ajipake manukato, avae nguo za ihram na aswali. Kisha atakusudia kuingia katika ihram ya Hija na aseme Talbiyah: “Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu, kwa kunuia kufanya Hija.” Ama wa Ifrad na Qarin bado watakuwa kwenye ihramu yao iliyotangulia. Kisha hujaji ataondoka aende Mina kabla ya adhuhuri, na atakaa na kulala huko. Ataswalia huko adhuhuri, alasiri, magharibi na ishaa, kwa kufupisha swala za rakaa nne bila kuziunganisha, na ataswalia hapo swala ya alfajiri ya siku ya tisa. Hujaji anafaa kuushughulisha muda wake kwa kufanya talbiyah, dhikri, na kusoma Qur-ani.

7- Siku ya Arafa

Pindi linapochomoza jua siku ya Arafa, ambayo ni siku ya tisa ya Dhul-Hijja, hujaji atatembea kutoka Mina hadi Arafa kwa utulivu na unyenyekevu, akimtaja Mwenyezi Mungu na kusema Talbiyah. Inapendekezwa ashukie na kukaa Namrat mpaka adhuhuri ikiwa ataweza kufanya hivyo, la sivyo ataingia Arafa na hakuna tatizo lolote katika hilo. Jua litakapopita katikati ya mbingu, ataswali swala ya adhuhuri na ya alasiri kwa kuzifupisha na kuziunganisha pamoja kwa kuswali swala ya alasiri katika wakati wa swala ya adhuhuri. Kisha baada ya hapo atakaa faragha kwa ajili ya kufanya dhikri na kumuomba dua Mwenyezi Mungu Mtukufu huku amenyanyua mikono yake juu na kuielekea Kibla.

Imesimuliwa kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Hakuna siku ambayo Mwenyezi Mungu humweka huru mja kutokana na Moto kuliko Siku ya 'Arafa. Yeye kwa hakika anakaribia, kisha anajifahirisha nao mbele ya Malaika wake akisema, 'Je, hawa wanataka nini?'" (Muslim 1348)

Wakati wa kusimama huko Arafa huanza kwa kupindukia jua katikati ya mbingu, na jua linapozama, mahujaji watatembea kwenda Muzdalifa. Na yeyote aliyekosa wakati huu, lakini akapata kusimama huko Arafa kabla ya alfajiri ya siku ya kumi - hata kwa muda mchache tu, - basi atakuwa amepata Hija na kusimama kwake huku kutakuwa sahihi. Ama atakayekosa kusimama kabla ya alfajiri hiyo, basi atakuwa amekosa Hija.

8- Huko Muzdalifa

Mwenye kuhiji akifika Muzdalifa, ataswali swala ya Maghrib na Isha kwa kuziunganisha na kuzifupisha kwa adhana moja na iqama mbili, na atalala huko Muzdalifa. Na alfajiri itakapopambazuka, ataswali swala ya alfajiri, kisha ataendelea kufanya dhikri na kuomba dua huku ameelekea Kibla huku amenyanyua mikono yake juu, mpaka alfajiri idhihirike vizuri.

9- Siku ya kuchinja

Unapochomoza mwanga wa mchana na kudhihirika vizuri siku ya kumi ya Dhul-Hijja, hujaji ataelekea Mina kabla ya jua kuchomoza, na atachukua changarawe saba katika kutembea kwake, ambazo atazitupa kwenye Jamarat. Atakapofika Mina, atairushia changarawe Jamrat al-Aqaba, ambayo ndiyo ya mwisho na iliyo karibu na Makka - kwa changarawe saba, huku akisema; “Allahu Akbar,” kwa kila changarawe. Atakapomaliza, atachinja mnyama wake wa dhabihu, kisha atanyoa nywele au kuzipunguza. Ama mwanamke, yeye atachukua katika nywele zake kiasi cha ncha ya kidole na azikate hizo. Inapendekezwa kwa hujaji kupaka manukato, kisha aende Makka na kufanya Tawaf al-Ifadha, ambayo ni moja ya nguzo za Hija. Kisha atafanya Sa'ayi ya Hija, kisha baada ya hayo atarudi Mina, na alale huko usiku wa kumi na moja.

10- Siku za Tashriq

Yapaswa kwa mwenye kuhiji katika siku za Tashriq alale Mina usiku wa kumi na moja na usiku wa kumi na mbili, na pia anaweza kulala huko usiku wa kumi na tatu ikiwa atataka kuchelewesha. Atakuwa akizitupia changarawe Jamarat hizo tatu katika siku hizi baada ya jua kupita katikati ya mbingu.

Jinsi ya kutupa vijiwe

Ataitupia vijiwe Jamrat ya kwanza, ambayo iko karibu na Msikiti wa Al-Khaif kwa vijiwe saba mfululizo, moja baada ya nyingine. Na atasema; "Allahu Akbar," kwa kila kijiwe. Kisha atasonga mbele kidogo na kuomba dua ndefu kwa yale anayopenda. Kisha ataitupia vijiwe Jamrat ya kati kwa vijiwe saba mfululizo, akisema “Allahu Akbar,” kwa kila kijiwe. Kisha ataenda upande wa kushoto na kusimama akielekea Kibla huku ameinua mikono yake juu, na aombe dua. Kisha ataitupia vijiwe Jamrat al-Aqaba kwa vijiwe saba mfululizo, akisema “Allahu Akbar,” kwa kila kijiwe, kisha ataondoka na wala hataomba dua baada ya hilo.

Akikamalisha kurusha vijiwe siku ya kumi na mbili, akipenda basi aharakishe na aondoke Mina, na akitaka acheleweshe na alale hapo siku ya kumi na tatu na atupe vijiwe vitatu baada ya adhuhuri kama ilivyotajwa hapo awali, na kuchelewa ndiyo bora zaidi.

Tawaf ya kuaga

Atakapotaka kutoka Makka kwenda nchini kwake, hatatoka hadi afanye tawaf ya kuaga Makka; na aifanye Tawaf hiyo kuwa kitu cha mwisho katika nyumba hiyo ya Makka ikiwa anataka kusafiri. Imesimuliwa kutoka kwa Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu amridhie, kuwa alisema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe za Mwenyezi Mungu juu yake: “Asiondoke, tena asiondoke mtu yeyote mpaka la mwisho lake liwe kuizunguka Nyumba." (Muslim 1327) Lakini Tawaf hii huondolewa kwa mwanamke akiwa ana hedhi.

Umemaliza somo kwa ufanisi


Anza mtihani