Sehemu ya sasa:
Somo Kuandikwa kwa Sunna na vitabu vyake muhimu zaidi
Wanachuoni wa Uislamu walikuwa na hamu ya kuandika Sunnah, kwa hivyo walimaliza miaka yao katika kuzihifadhi, kutofautisha zilizo sahihi mbali na zisizo sahihi, na kubainisha hali za wasimulizi wake kwa njia ambayo haina mfano wake katika historia ya wanadamu wote.
Maana ya uandishi wa Sunna za Mtume
Ni kuandika na kurekodi yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama vile maneno, matendo, mambo aliyoidhinisha bila ya kuyafanya mwenyewe, na kuyakusanya hayo yote katika vitabu.
Mchakato wa kurekodi Sunnah na kuandika Hadithi za Mtume ulipitia awamu kadhaa, kama ifuatavyo:
Awamu ya kwanza:
Uandishi wa Sunna katika zama za Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na maswahaba zake, katika karne ya kwanza ya Hijra, licha ya kwamba Nabii rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa amekataza kuandika hadithi zake mwanzoni mwa Uislamu, kwa kuogopa zichanganyike na Qur-ani.
Imesimuliwa kutoka kwa Abu Sa'id Al-Khudri, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa: Mtume wa Allah, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Msiandike chochote kutoka kwangu, na yeyote atakayeandika kutoka kwangu yasiyokuwa Qur-ani, basi na akifute. Na zungumzeni kunihusu, na hakuna ubaya wowote katika hilo." (Muslim 3004)
Kwa hivyo, hadithi za Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, zilikuwa zikihifadhiwa katika vifua na zilikuwa zikienezwa kwa mdomo kwa kuzisimulia tu. Kisha Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, aliidhinisha baadhi ya masahaba kuziandika Sunna zake.
Imesimuliwa kutoka kwa Abdullah bin Amr, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwa alisema: Nilikuwa nikiandika kila kitu nilichokisikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ili nikihifadhi. Lakini Maquraishi walinikataza, na wakasema: "Je, unaandika kila kitu unachokisikia, ilhali Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni binadamu anayesema katika hali ya ghadhabu na katika hali ya kuridhia?" Kwa hivyo nikaacha kuandika, na nikamtajia hilo Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Lakini akaashiria kwa kidole chake kuelekea kwenye mdomo wake, na akasema: "Andika, ninaapa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, hakitoki ndani yake isipokuwa haki." (Sunan Abu Dawud 3646).
Katika Hadithi ya Al-Walid bin Muslim kutoka kwa Awzai, kuna kwamba Abu Huraira, Mwenyezi Mungu amridhie alisema: "Mwenyezi Mungu alipomfungulia Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, Makka, alinyanyuka miongoni mwa watu, na akamhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu. [Abu Huraira alitaja hotuba yake hiyo kisha akasema]: Abu Shah, mwanamume mmoja kutoka Yemen, akasimama na akasema: "Niandikieni, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akasema: "Mwandikieni Abu Shah." Al-Walid alisema: Nikamwambia Awzai: Ni nini maana ya maneno yake: Niandikieni, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Akasema: "Hii ni hotuba aliyoisikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake." (Al-Bukhari 2434, na Muslim 1355)
Awamu ya pili
Uainishaji wa Hadithi katika zama za mwisho za wale waliokuja baada ya maswahaba katika karne ya pili ya Hijra. Uandishi huu ulikuwa na sifa maalumu ya uainishaji wa jumla wa Sunnah ya Mtume, lakini haukuwa na utaratibu maalumu. Na wa kwanza kufanya hivi alikuwa amiri wa Muumini Umar bin Abdul Aziz Mwenyezi Mungu amrehemu. Aliwaamrisha maimamu wawili, Ibn Shihab Az-Zuhri na Abu Bakr bin Hazm kukusanya Sunnah za Nabii, na akaandika barua kwenda kwenye sehemu za mbali kwamba: "Angalieni Hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu, mzikusanye na mzihifadhi. Kwani, ninahofia kupotea kwa elimu na kufa kwa wanazuoni."
Na alikuwa wa kwanza kuandika hadithi kwa amri yake Imam Az-Zuhari – Mwenyezi Mungu amrehemu. - Na huu ndio ulikuwa mwanzo wa kuandikwa kwa Sunnah na hadithi za Nabii kwa ujumla.
Uandishi wa Sunnah kwa njia ya vitabu maalimu vilivyopangwa sawasawa, ima kwa mpangilio wa milango ya kielimu kama vile imani, elimu, twahara, swala, na kadhalika. Au kwa namna ya kupanga hadithi za kila swahaba kivyake, kama vile mlango wa Abu Bakr, kisha Umar, hivyo hivyo.
Katika awamu hii, kiliandikwa kitabu cha Imam Malik bin Anas - Mwenyezi Mungu amrehemu. Awamu hii ilikuwa na sifa maalumu ya mpangilio wake mzuri wa hadithi na pia yakachanganywa meneno ya Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, pamoja na maneno ya maswahaba na wale waliowafuata maswahaba na fatwa zao.
Hii ilikuwa awamu ya kupambanua hadithi za Nabii,rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika uandishi na kuzikusanya na kuzipanga sawasawa bila ya kuzichanganya na maneno mengineyo kama vile maneno ya maswahaba na wale waliokuja baada yao - isipokuwa kwa kiasi kidogo kinachoweza kuhitajika. Awamu hii ilianza mwanzoni mwa karne ya tatu ya Hijra. Na mojawapo ya vitabu maarufu vilivyoandikwa wakati huu ni: Musnad Imam Ahmad, Musnad Al-Humaidi, na vinginevyo.
isha uandishi wa hadithi ulifikia kikomo chake katikati ya karne ya tatu ya Hijra. Ambapo Imam Al-Bukhari alitunga Sahih Al-Bukhari, na Imam Muslim akatunga Sahih Muslim, na vile vile vitabu viitwavyo Sunan vikaandikwa kama vile Sunan Abu Dawud, Sunan Tirmidhi, Sunan Nasai, Sunan Ibn Majah, Sunan Darmi na vitabu vinginevyo maarufu vya hadithi.
Miongoni mwa vitabu vingi vya Sunnah ya Mtume, kuna vitabu sita ambavyo ni maarufu, navyo ni: Sahih al-Bukhari, Sahih Muslim, Sunan Abu Dawud, Sunan Ibn Majah, Sunan Nasai, na Jamii' Tirmidhi.
Pia miongoni mwa vitabu vya Sunna vilivyokuwa maarufu ni Sunan Darmi, Musnad Imam Ahmad, na Muwatta Imam Malik.
Kuhusu Vitabu Sita vya hadithi
Miongoni mwa vitabu maarufu zaidi vya Sunna, ambavyo umma ulivipokea kwa kuvikubali ni vitabu sita, ambavyo ni:
1. Sahih Al-Bukhari (aliyekufa mwaka wa 256 Hijria)
Ni miongoni mwa vitabu vilivyokusanya vyote vilivyomfikia mwandishi miongoni mwa Hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika itikadi, ibada, miamala, vita, tafsiri na fadhila mbalimbali. Na hakuna kilichoandikwa humo isipokuwa hadithi sahihi, nacho ndicho kitabu sahihi zaidi baada ya Qur-ani Tukufu.
2. Sahih Muslim (aliyekufa mwaka wa 261 Hijria)
Hiki pia ni katika vitabu vilivyojumuisha hadithi za Nabii ambacho mwandishi wake hakuandika humo isipokuwa hadithi sahihi. Lakini masharti ya kusahihisha hadithi zake yalikuwa mepesi zaidi kuliko yale ya Al-Bukhari. Kwa hivyo hiki ndicho kitabu cha pili baada ya Kitabu cha Al-Bukhari.
3. Sunan Abi Daudi (aliyekufa mwaka wa 275 Hijria)
Nacho ni katika vitabu vya Sunna, ambacho mwandishi wake alikipanga katika milango ya fiqh. Na aliingiza katika kitabu chake hiki hadithi sahihi na zile ambazo ni Hasan, lakini hakuingiza humo hadithi dhaifu isipokuwa mara chache tu.
4. Sunan Tirmidhi (aliyekufa mwaka wa 279 Hijria)
Ni miongoni mwa vitabu vilivyokusanya vyote vilivyomfikia mwandishi miongoni mwa Hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuhusiana na itikadi, ibada, miamala, vita, tafsiri na fadhila mbalimbali. Lakini hakuandika humo hadithi sahihi peke yake, bali humo mna hadithi sahihi, hasan, na hata dhaifu.
5. Sunan Al-Nasai (aliyekufa 303 Hijria)
Hiki pia kimepangwa kulingana na milango ya fiqh. Na ndani yake kuna hadithi sahihi, hasan, na hata dhaifu.
6. Sunan Ibn Majah (aliyekufa 273 Hijria)
Hiki pia kimeandikwa kulingana na milango ya fiqh. Na ndani yake kuna hadithi sahihi, hasan, na hata dhaifu ambazo baadhi yake zimekataliwa.
Imam Al-Hafidh Abu Al-Hajjaj Al-Mizzi (aliyekufa 742 Hijria) alisema:
“Ama Sunnah, Mwenyezi Mungu ameijaalia wenye kuzihifadhi, wenye elimu, mabwana wasomi, na wakosoaji shupavu, ambao wanaziondolea upotoshaji wa watu wenye msimamo mkali, na tafsiri ya wajinga. Kwa hivyo wakaziandika kwa njia mbalimbali wakijitahidi sana kuzihifadhi na kwa kuogopa zisipotee. Na miongoni mwa vitabu vya hadithi vilivyoandikwa vyema sana, kilicho sahihi zaidi, chenye makosa machache, chenye manufaa ya jumla zaidi, chenye baraka kubwa zaidi, kilicho rahisi zaidi, kilichokubalika zaidi na wenye kukubali na wapinzani, na kinachoheshimika zaidi mbele ya watu maalumu (wasomi) na watu wa kawaida ni: Sahih Bukhari, cha Abu Abdullah Muhammad bin Ismail al-Bukhari.Kisha Sahih Muslim cha Abu al-Hussein Muslim bin Hajjaj an-Naysaburi.Kisha baadaye ni vitabu vya Sunan kama vile Sunan Abu Dawud Suleiman bin Al-Ash'ath As-Sijistani, kisha kitabu cha "Al-Jami'" cha Abu Isa Muhammad bin Isa At-Tirmidhi, kisha kitabu cha "As-Sunan" cha Abu Abdur-Rahman Ahmad bin Shuaib an-Nasai, kisha kitabu cha "As-Sunan" cha Abu Abdullah Muhammad bin Yazid, anayejulikana kwa jina Ibn Majah Al-Qazwini, hata kama hakufikia kiwango chao.
Kila moja ya "Vitabu sita" hivi kina sifa yake maalumu ambayo watu wa nyanja hii wanaijua. Vitabu hivi ni maarufu miongoni mwa watu na vimeenea katika nchi zenye Uislamu, na ni vyenye faida kubwa, na wanafunzi wamefanya bidii ya kuvisoma." (Tahdhib Al-Kamal 1/147)
Mwisilamu anaweza kujua kiwango cha usahihi wa hadithi; je, ni hadithi inayokukubaliwa au dhaifu yenye kukataliwa kwa kuwarejelea wanazuoni ambao wanajishughulisha na elimu ya Hadithi ambao ni wataalamu katika hilo. Walizisoma hadithi hizo kwa kuzingatia hali za silisili ya wasimulizi wake na maneno yenye katika hadithi hizo, na kwa kuzingatia kukubalika kwake na kukatalika kwake.
Kuna vitabu vingi vilivyoandikwa katika hilo, na vile kuna programu nyingi na majukwaa mbalimbali ya kuaminika ya kielektroniki yanayosaidia katika kujua Hadithi sahihi kutoka kwa dhaifu.
Miongoni mwa programu na majukwaa ya kielektroniki ambayo husaidia kujua kiwango cha usahihi wa hadithi ni:
Ensaiklopidia ya kisasa katika tovuti ya Durar Siniyya, ambayo inajumuisha mamia ya maelfu ya hadithi, pamoja na hukumu za wasimulizi wa hadithi (wa zamani, wa nyuma, na wa kisasa), na inawezekana kuifikia kupitia kiungo hiki: https://dorar.net/hadith